Wiki iliyopita nilieleza chanzo na sababu za kuwapo kwa udini nchini, jinsi ulivyopandwa na kupaliliwa hadi kumea na kuwa mgumu kama kisiki cha mti aina ya mpingo.
Kwanza, napenda kuungana na waandishi wa habari katika kulaani udini usiwepo na utokomee kuzimu. Pili, nawakubali viongozi wa dini na wa Serikali wanaokemea vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani chini ya kivuli cha udini.
Tatu, nawapa kongole wale wanasheria na wanasiasa wapevu na wananchi waadilifu, kwa kuona athari za kupuuzia kuchukua hatua za mazungumzo kunakofanywa na Serikali na viongozi wa dini. Iwapo hatua za mazungumzo zitachukuliwa zitawezesha kubaini bila shaka chanzo cha udini, nani ana udini na vipi suluhu itapatikana dhidi ya udini.
Nne, nasema kitendo cha kunajisi Qur’an Tukufu kilichofanywa na kijana chipukizi Emmanuel Josephat (14) wa Mbagala, Dar es Salaam, kimezua sokomoko ndani ya jamii ya Watanzania.
Vyombo vya habari nchini vimezungumzia sokomoko hilo kwa maono tofauti – ya utetezi wa hatia, ya udini na yasiyo ya udini, ya ushawishi na yasiyo ya ushawishi, ya mafunzo na yasiyo ya mafunzo. Ni mtoto na si mtoto. Bado kitendo kile kimeonekana kusimama pale pale kwenye udini.
Tambua na kumbuka mayowe yote ya dini yanayopigwa yanatoka ndani ya kambi mbili: Kambi ya kwanza ni ile inayotuhumiwa na kulalamikiwa kutumia udini katika baadhi ya uamuzi na vitendo vyake vya kuionea kambi ya pili.
Kambi hiyo ya kwanza inadaiwa kuundwa na Ukristo na kuongozwa na madhehebu ya Ukatoliki. Pia inasaidiwa na kutetewa na vyombo vya Serikali yenyewe katika matendo na uamuzi dhidi ya kambi ya pili. Kambi ya pili ni ile inayotuhumu na kulalamika kuwa inaonewa na haisikilizwi juu ya madai yao dhidi ya kupuuzwa na kunyimwa haki zao za kidini, kijamii, kikatiba katika kuabudu, kupata elimu sawa na dini nyingine na hivyo kuonekana kama raia wa daraja la pili nchini mwao.
Kambi hii inaundwa na kuongozwa na Waislamu wenyewe. Inadai haina mshirika wala mtetezi kutoka nje ya kambi. Kambi hii inakosa mshikamano (solidarity) kwa sababu ya kurubuniwa na maadui wa Uislamu. Kwa mtazamo wangu, Watanzania wengi wametumbukia ndani ya kambi hiyo bila kujijua na kushiriki mijadala ya udini bila ya kutambua maana halisi ya udini. Ni sawa na Msukuma kucheza ngoma ya gombe sugu ya Wazaramo.
Nimefuatilia maandishi na matamko katika vyombo vya habari nchini (si vyote) katika muktadha huu, nimeona vyombo hivyo navyo vimejigawa katika kambi hizo na kuimba nyimbo mbili tofauti zinazoshabikia kambi.
Kuna vyombo vya habari vinavyoimba: Waislamu hawana malalamiko ya msingi, wanafanya fujo tu, ni wahuni, wasulubiwe kwa sababu wanaleta udini na Serikali ikomeshe udini.
Vyombo vingine vya habari vinavyoimba: Mfumo Katoliki/Kristo unadhulumu Waislamu haki za kijamii, vyombo vya dola – polisi, inawanyanyasa, Serikali haiwasikilizi Waislamu, inawapuuza katika madai yao ya kikatiba, Serikali iache upendeleo wa dini moja – Ukiristo.
Kwa nukta hiyo, msomaji wa makala haya nakuomba chonde chonde uwe mdini wa Kikristo au mdini wa Kiislamu, tumia haki uliyopewa na Mwenyezi Mungu kuliangalia suala la udini kwa mapana yake, kwa kina chake na madhara yake.
Wakati wote uwe mtulivu, makini, mkweli, shupavu na mwenye busara katika tafakari ya udini. Utoke na msimamo wa dhati ndani ya nafsi yako usio na sura mbili (double standard).
Katika kuweka kadhia ya mada hii, nimeona ni vema tukawasoma viongozi wanne wa dini waliobobea katika masuala ya dini na ya jamii kwa falsafa na kauli zao mbele ya Mwenyezi Mungu, kuhusu haki na udini.
Padre Vic Missaen katika kitabu chake cha ‘Mafunzo ya Kanisa kuhusu jamii, Teolojia kwa Walei’ uk. 2, anasema, “Tunachotamani wote ni ufalme wa HAKI, AMANI NA UPENDO, na kwa maana hiyo jitihada zetu daima ni katika kupambana na mambo yote yanayojaribu kuangamiza ufalme huu tunaoutamani.”
Anaendelea, “Tunapinga mambo yote yanayokiuka haki, yanayoleta chuki na uhasama, hali ya kutokujaliana na kukosekana kwa huruma katika uhusiano wetu.”
Padre Vic anamaliza kwa kusema (uk. 5), “Haki za watu hazikuwekwa na kanisa wala Serikali bali ni matakwa ya Mungu ndani ya mpango wake, kwamba kila maisha yapate haki na wajibu wake kwa kadiri ya mastahili kutokana na asili yake binadamu.”
Kiongozi mwingine wa dini ni Sheikh Mohammed Idd. Imam wa msikiti wa kwa Mnyamani, Buguruni, Dar es Salaam. Katika gazeti la Kisiwa Toleo Na. 43, Oktoba 5-7, 2012 anasema, “Katika mambo ya dunia, Mwislamu akiendesha maisha yake kwa kufuata utaratibu ulioelekezwa na Qur’an na Sunna, huyo ndiye mdini, yaani ameshika dini.
“Hiyo ni sifa nzuri inayoweza kusifiwa. Mwislamu anatakiwa kuwa mdini, mshika dini, asiwe na udini.
Anaongeza, “Tanzania haina dini lakini Watanzania wana dini zao. Hii ina maana kuwa hakuna dini maalumu ya Serikali ya Tanzania.
Lakini baadhi ya Waislamu kwa kutofahamu tafsiri halisi ya dini na udini, wamekuwa wakiogopa kufanya ibada kwa kuogopa kuambiwa wana udini.
Sheikh Mohammed Idd anamaliza kwa kutoa mfano, “Mwislamu yuko kazini ofisi ya Serikali au binafsi, ana msahafu wake uko pembeni, lakini anaogopa kusoma aya mbili tatu wakati wa mapumziko kwa kuhofia ataonekana ana udini. Huu si udini.
Itaendelea