Septemba 23, mwaka huu Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu Tanzania wamemwandikia barua Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kupinga utaratibu mpya wa mitihani na upangaji madaraja kuhusu masomo ya dini ya Kiislamu, kompyuta, lugha za Kiarabu, Bible Knowledge na Kifaransa. Masomo haya sasa yamegeuzwa ya hiari.

Wakuu wa shule wanasema kwa mujibu wa tangazo la Serikali lililotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania, kuanzia Machi mwaka huu, ni kwamba hata mwanafunzi akifaulu masomo hayo katika kupanga madaraja ufaulu wake hautahesabiwa. Hii ina maana kuwa hata mwanafunzi akipata alama A kwa somo la kompyuta ni sawa na kupata sifuri.

 

Bila kuuma maneno sisi tunasema tunasikitishwa na kushangazwa uamuzi huu. Tunawaunga mkono wakuu wa shule za Kiislamu kama Mwenyektii wao Hamisi A. Togwa, tunakubaliana nao kwa asilimia 100 kuwa uamuzi huu unakwenda kuua elimu nchini. Tunajiuliza nini kimepungua au kupunguza uwezo wa kufikiri kwa viongozi wetu waliopewa jukumu la kusimamia elimu, hatupati jibu.

 

Leo dunia ni ya sayansi na teknolojia. Dunia inaongozwa kwa Tehama. Hata mkutano wa Smart Partnership uliomalizika mwezi Juni hapa nchini maudhui makuu ya mkutano huo ambao Tanzania ilikuwa mwenyeji yalihusu matumizi ya teknohama. Dunia inapambana kujikita katika matumizi ya kompyuta sisi tunataka kuua morali wa wanafunzi kusoma kompyuta.

 

Masomo ya dini yamekuwa nguzo ya kujenga maadili kwa vijana wengi waliokuwa shuleni. Leo tunaona tumekwishapata maadili ya kutosha kwa kiwango ambacho hatuhitaji tena kuwafundisha vijana wetu masomo ya dini? Tunashuhudia kashifa nyingi zinaibuka kila kukicha na ilitarajiwa kuwa walau dini ndio pekee ingeweza kuepusha mmomonyoko wa maadili, ila leo viongozi wetu wanaona hapana.

 

Ukiacha hilo makanisa na misikiti vinaongezeka mwaka hadi mwaka kadri dunia inavyozidi kuwa na watu wengi. Uchungaji na Usheikh kwa sasa ni ajira. Vijana hawa wakifundishwa dini mapema shuleni na ikawaingia akilini, hakika nchi yetu inaweza ikarejea katika enzi za uadilifu ambazo zinapoteka kwa kasi.

Kuhusu masomo ya lugha kama Kifaransa, Kiarabu na mengine, tunasikitika kuona nchi yetu haiyapi umuhimu. Nchi zilizotuzunguka zimeanza kufundisha haki Kichina kwa watu wao. Watanzania tunashindwa kufanya biashara kimataifa kutokana na kutozifahamu lugha za kigeni. Tunasema lugha za kigeni ni ajira si tu katika biashara, bali hata sekta ya utalii.

 

Kinachotusikitisha zaidi, hawa watunga sera waliopitisha uamuzi huu baadhi ni wanufaika wa masomo haya. Kuyaona masomo haya kuwa si muhimu, ni kujidanganya kwa kiwango cha hali ya juu na haikubaliki kwa kila hali. Tunaungana na wakuu hawa wa shule kuitaka Serikali kurekebisha upungufu huu. Tunasema mpango huu usitishwe, masomo haya yaendelee kuhesabiwa katika alama za ufaulu, vinginevyo tunavuruga elimu yetu nchini.