Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
SERIKALI ipo mbioni kutengeneza mfumo wa kitaifa wa kielekroniki wa Taarifa za soko la ajira utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 346.9 kwa ajili ya kuwezesha ukusanyaji wa taarifa kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa.
Hatua hiyo imelenga kupunguza taarifa za upotoshaji wa nafasi za ajira ambazo mara nyingi zimekuwa zikisambazwa mitandaoni na kuleta taharuki kwa wahitaji wa ajira na kusababisha kutapeliwa na wakati mwingine kuingizwa kwenye majanga mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Desemba 14,2023 Jijini hapa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na wenye ulemavu Patrobas Katambi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa baadhi ya shughili zinazotekelezwa kwenye Wizara hiyo.
Aidha amesema kwa upande wa huduma za watu wenye ulemavu Serikali
imetoa kiasi cha shilingi bilioni 3.46 za kitanzania kwa ajili ya ukarabati vyuo vya ufundi stadi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu vilivyopo Sabasaba-Singida,Yombo-Dar Es Salaam ,Mtapika- Masasi na Luanzari-Tabora na Mirongo -Mwanza .
Amesema Vyuo hivyo vina Vijana wenye ulemavu watapao 774 na kiasi cha shilingi milioni 568 kimetumika kuwezesha mafunzo husika.
“Serikali imeendelea kutoa mafunzo kupitia vyuo vipya vinne vya ufundi stadi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu vya Songwe,Mwanza ,Kigoma na Ruvuma na kiasi cha shilingi bilioni 3.4 kimetumika kwa kwaka wa fedha 2023/2024 kiasi cha shilingi bilioni 3 kimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi kwa vyuo husika,”amesema
Pamoja na hayo Naibu Waziri Katambi ameeleza kuwa katika kuwaenzi zaidi wenye ulemavu Serikali inazindua mfumo wa taarifa za watu wenye ulemavu (PD-MIS)utakaoweza kusaidia upatikanaji wa taarifa zao na kurahisisha utoaji huduma kwa kundi hili maalumu.
“Pamoja na mambo hayo yote Serikali pia imeendelea kusimamia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu kila ifikapo Desemba 3,2023,wiki ya viziwi ambayo huadhimishwa September 2023,na siku ya watu wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Oktober 25,lengo ni kuengeza uelewa wa haki na ustawi wa watu wenye ulemavu kwa jamii,”amesisitiza.