Najua wengi wameandika mada hii. Ni karibu wiki sasa tangu kutokea kwa ugaidi kule Arusha. Wengi wameibuka na mijadala yenye kusisitiza kuwa kilichotokea Arusha ni mwendelezo wa udini. Baadhi wamefika mahali wanasema wazi kuwa Serikali imetunga majina ya watuhumiwa.
Mtuhumiwa Ambross Victor, inaelezwa kuwa ni bandia. Haya ameyasema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Mwanza, Padre Dk. Charles Kitima. Anawatuhumu wazi wafuasi wa dini ya Kiislamu kuwa wamehusika moja kwa moja na tukio hili.
Naelewa uchungu alionao Dk. Kitima. Naelewa tukio la Arusha linavyokumbusha machungu ya mauaji ya Padre Evarist Mushi aliyepigwa risasi huko Zanzibar. Padre Kitima inamkumbusha tukio la mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachira wa Buseresere katika mgogoro wa uchinjaji.
Sitanii, mabomu tulikuwa tunayasikia sehemu mbalimbali nje ya nchi. Tumezoea kuyasikia Somalia, Sudan na kwingineko. Binafsi nimejaribu kujifikirisha zaidi. Moja nimelibaini na nimelisema hili na naomba kuanza nalo. Serikali imelegea katika kusimamia sheria za nchi.
Wiki iliyopita nilihudhuria mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, na waandishi wa habari. Alisema, kuanzia sasa itakuwa ni marufuku mtu yeyote kuendesha mihadhara ya dini yenye mwelekeo na lengo la kukashifu dini nyingine.
Akasema yeyote atakayekutwa anauza kanda za uchochezi atachukuliwa sawa na muuza dawa za kulevya. Akasema vizuri tu, kuwa vipaza sauti vya misikitini na kanisani ni kwa ajili ya kuitwa waumini na si kuvitumia kutukana dini nyingine.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, yeye akasema sasa wataanza kuingia kwenye mitandao ya kijamii; twitter, facebook, jamiiforums na youtube, kufuatilia watu wenye kusambaza ujumbe unaochochea chuki za udini. Hata ujumbe mfupi (sms) kutoka kwenye simu zetu amesema utafuatiliwa.
Viongozi hawa wametoa msimamo huo, baada ya viongozi wa dini mkoani Dar es Salaam kukutana na kuitaka dola kutumia sheria za nchi zilizopo kudhibiti wachochezi kwa nia ya kurejesha amani nchini. Viongozi hawa katika tamko lao wametaka dini zote kuheshimiana.
Sitanii, nasema viongozi wetu wanapoteza muda. Ukienda Manzese unayakuta hayo maigizo ya Waislamu kutukana Wakristo. Badala ya kuhubiri uzuri wa dini yao, wanahubiri ubaya wa Ukristo na kusisitiza kuwa Yesu si Mtume na wala Yesu si Mungu.
Nasema ukiisikiliza mijadala hiyo na kanda mbalimbali zinazouzwa mtaani, kwa haraka unaweza ukasema Waislamu ndiyo wenye kusambaza chuki dhidi ya Wakristo. Mimi nasema tufunge breki kidogo kabla hatujawatuhumu Waislamu kuhusika na matukio haya.
Ukienda Sudan walipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe hadi nchi ikatengana na kuzaa nchi mbili; Sudan na Sudan Kusini, lakini pale halikuwa suala la Wakristo na Waislamu kama ilivyokuwa inaenezwa propaganda. Tatizo yalikuwa mafuta katika Jimbo la Abyei.
Baada ya nchi hizi kutengana na Jimbo la Abyei likaangukia chini ya Sudan Kusini, vita imekwisha. Ukienda Sudan Kusini asimia 75 ya watumishi wa Serikali ya nchi hiyo ni Wamarekani. Wanadai ‘wanawafundisha utawala bora’. Watakuwapo kwa miaka kadhaa na watawasaidia kuwafundisha jinsi ya kuchimba mafuta.
Miaka miwili iliyopita, tumeelezwa habari za uharamia (piracy) kukua katika mwambao wa Somalia. Al-Shabaab wakashika kasi nchini Somalia wakidaiwa kushirikiana na Al-Qaeda. Meli zikawa zinatekwa kama vile kuna kimbunga. Kwa bahati mbaya nyingi ya meli zilizokuwa zikitekwa ni zenye bidhaa kutoka China kuja Afrika.
Sitanii, inahitaji kutumia akili kidogo tu kujua kwa nini meli za kutoka China kuja Afrika zitekwe. Biashara kati ya China na Afrika ni tishio kwa Wazungu. Wazungu hawa waliokwishaligeuza Bara la Afrika kuwa shamba lao la kuchuma kila kitu watafurahije China ichukue nafasi yao? Kwa nini wasianzishe uharamia?
Leo, hapa kwetu Tanzania tumegundua gesi nyingi ajabu. Kuna kila dalili kuwa tutagundua mafuta. Kule Nantumbo tumeanza kuzalisha madini ya urani (uranium). Nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa urani ni Kazakhstan inayozalisha tani 19,000 kwa mwaka.
Nchi ya pili kwa uzalishaji wa madini hayo ya urani ni Canada inayozalisha tani 9,500 kwa mwaka. Pale Nantumbo Tanzania itazalisha tani 14,000 kwa mwaka. Hii ina maana itachukua nafasi ya Canada na kuwa ya pili kwa uzalishaji kwa wingi wa madini haya. Hatujataja urani inayopatikana Bahi na Singida. Unadhani Wazungu hawalikodolei macho hili?
Sitanii, ni lazima tuwe makini. Taarifa hizi za upatikanaji wa gesi, urani na mafuta Wazungu wanazo. Wameona njia rahisi ya kutufanya Watanzania tupigane vita ni kupitia udini. Kuna kila dalili kuwa wanaelekea kufanikiwa. Si muda mrefu tutaingia msituni, watakuja kwa mwavuli wa kutusuluhisha na kutujengea miundombinu iliyoharibika, na hiyo ndiyo itakuwa fursa kwao kupora urani, gesi, dhahabu, tanzanite, almasi, mafuta na mengine.
Nasema bila kuuma maneno. Labda kama Serikali ni sehemu ya mkakati huu, lakini kama si hivyo, basi inapaswa kutumia kila nguvu iliyonayo kudhibiti hali hii. Tusipofanya hivyo, miaka mitano tu ijayo, tutakuwa tunawaomba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuleta kwetu majeshi ya kulinda amani. Tukatae kugawanywa Watanzania. Wanaofanya haya ni kwa faida ya Wazungu na si zaidi ya hapo.