Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema serikali inafanyia kazi malalamiko yanayotolewa na wananchi kuhusu huduma za mawasiliano.

Nape amesema hayo Arusha wakati anafungua kikao kazi cha siku tatu cha viongozi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Amesema Watanzania wanastahili huduma bora na rahisi za mawasiliano zinazopatikana kila mahali.

Nape amesema mwaka huu Tanzania imeahidi kurusha satelaiti yake na kusisitiza wakati wowote satelaiti itarushwa.

“Tulipokwama, tuliposuasua tutafanya tathmini ya kina na kuambiana hali ilivyo ikiwamo kufanya maboresho ili mwaka huu wa fedha 2023/24 tuweze kuendelea mbele,” alisema.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Khamis Abdulla amesema wizara hiyo imepata mafanikio kwa sababu ya upendo, umoja na amani walionao viongozi na watumishi kwa ujumla.

Abdulla amehimiza viongozi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo watumie nafasi zao za kimamlaka kwa kuwaelekeza kazi wafanyakazi wa chini ili nao wajitume zaidi.

“Watumishi tukiwa na umoja na kujituma ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu na ninaomba tufanye kazi kwa kujituma na si kushurutishwa kwa sababu hakuna haki bila wajibu,” amesema.

Abdulla ameagiza wakuu wa taasisi wasimamie utekelezaji wa sera, kanuni, miongozo na taratibu zinazohusu haki na utawala bora na wasimamie stahiki za wafanyakazi.

Please follow and like us:
Pin Share