Mwishoni mwa Agosti mwaka huu
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa
Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) imeikataa
rufaa ya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) kupinga hukumu ya kuilipa Benki
ya Standard Chartered Dola za Marekani
milioni 148.4 (sawa na Sh bilioni 336).
Akiongoza jopo la wajumbe waliosikiliza
rufaa hiyo, Rais wa ICSID, Claus von
Wobeser, ametupilia mbali hoja za Tanesco
za kuitaka mahakama hiyo kutengua
uamuzi wa awali ulioipa ushindi Benki hiyo
ya Standard Chartered ya Hong Kong.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Tanesco
kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa
mwaka 2016 ikilitaka shirika hilo kulipa kiasi
hicho cha fedha.
Fedha hizo ni madai ya malipo ya umeme
baina ya Tanesco na Kampuni ya
Independent Power Tanzania Limited (IPTL)

iliyopewa zabuni ya kufua umeme wa
dharura kuanzia Mei 26, 1995 huku ikidaiwa
na benki hiyo.
Tanesco kwa kushirikiana na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu ni muhimu kuhakikisha
wanakata rufaa tena kutetea masilahi ya
Tanzania, maana endapo jambo hilo
litaachwa hivyo, nchi italazimika kutumia
fedha za walipa kodi kutokana na historia
mbaya ya fedha za IPTL zilizokuwa kwenye
akaunti ya Escrow kuliwa.
Tunafahamu kutokana na ubishi wa
uwekezaji, yalifikiwa makubaliano baina ya
Tanesco na wamiliki wa mitambo ya IPTL
kwamba fedha zitakazotokana na malipo ya
ankara za umeme ziwekwe katika akaunti
ya Escrow.
Kampuni ya PAP, ambayo ndiyo inadai
kununua mali na madeni ya IPTL, ilinunua
mali na madeni ya mfilisi IPTL. Tunatarajia
kwamba mbali na kukata rufaa ni wakati
sahihi kujipanga sawasawa na kuhakikisha
fedha zilizoliwa kutoka kwenye akaunti ya
Escrow zinarejeshwa.
Kampuni ya IPTL ilikuwa ikidaiwa na benki
hiyo kutokana na mkopo iliochukua
kununua mitambo na kutekeleza mkataba
wa kufua na kuuza umeme kati yake na

Tanesco.
Tanesco katika nakala ya hukumu hiyo ya
Agosti 2, imeagizwa kulipa gharama zote za
uendeshaji wa shauri hilo ikiwamo ada ya
kesi na malipo ya wajumbe wa kamati
waliolisikiliza.
Mbali na kukata rufaa ni wakati sahihi
serikali kutafuta mawakili ambao wataweza
kusaidia nchi na kuinasua Tanesco katika
mtego ambao kwa namna moja ama
nyingine utakuwa na athari kwa nchi.

Mwisho