Wiki mbili zilizopita tumechapisha habari za uchunguzi juu ya mradi wa e-passport. Tumeeleza katika habari hizo kuwa kuna ufisadi unaokadriwa kufikia Sh bilioni 90, fedha ambazo waliokabidhiwa jukumu la kutafuta mzabuni kama wangetenda kwa masilahi ya taifa basi zingeokolewa. Katika habari tulizochapisha tumebainisha kuwa kampuni ya DeLaRue ilikuwa tayari kuchapisha hati za e-passport kwa gharama ya pauni 6, 989,468, sawa na dola za Marekani milioni 16 au shilingi za Tanzania bilioni 35.84.
Kwa mujibu wa mkataba tuliouona, kiasi hiki kingetumika katika kipindi cha miaka 8 tangu siku ya kuingia mkataba. Tumenasa mawasiliano kati ya kampuni hii na wakubwa na pia kampuni HID Global iliyopewa zabuni kwa njia zisizoeleweka hali inayoashiria utovu wa uadilifu kwa watendaji walioshughulikia suala hili kutoka Ofisi ya Rais Ikulu. Si hilo tu, tumesema bayana kuwa dola milioni 57 zilizotajwa na Rais John Pombe Magufuli wakati wa kuzindua hati za kielektroniki watendaji walimtegeshea.
Tumesema katika habari hizo kuwa masharti ya zabuni yalitaka mzabuni awe na mitambo yake, awe na uzoefu wa kutengeneza hati za kusafiri kwa angalau nchi 10 na 5 kati ya hizo ziwe ePassport kuwa yamekiukwa. Kampuni iliyopewa ya HID Global haina uzoefu wa kutengeneza ePassport ukiacha passport ya nchi moja tu Ireland, ambayo nayo iliungana na Kampuni ya DLRS Group kutekeleza mradi huo.
Tumebainisha kuwa gharama ya dola milioni 57 karibu Sh bilioni 129, ni kubwa mno. Gharama hii inawafanya Watanzania kukamuliwa Sh 150,000 kupata hati ya kusafiria, gharama ambayo ni mara tatu zaidi ya gharama iliyokuwa inatozwa awali ya Sh 50,000. Tumesema Kenya wanatumia ePassport, lakini gharama wanayolipishwa ya Ksh 4,550 ni sawa na Sh 81,900 za Tanzania. Tumebainisha kuwa idadi ya hati zinazotarajiwa kutengenezwa 400,000 hata zikiuzwa zote nchi bado itapata hasara ya Sh bilioni 68.
Pia katika habari hizo za uchunguzi tumezitaja baadhi ya nchi za Afrika ambazo kampuni ya DeLaRue iliyonyang’anywa zabuni ya kutengeneza passport zetu inazitangenezea hati za kielektroniki na vitambulisho mbalimbali. Nchi hizo ni Angola, Ghana, Mali, Swaziland, Lesotho, Botswana, Rwanda, Somalia, Kenya, Sudan, Mauritania, Cameroon na Guinea Bissau. Kampuni ya HID Global iliyopewa zabuni haijawahi kutengeneza hati hata moja ya kielektroniki kwa nchi yoyote ya Afrika.
Baada ya kuchapisha habari hizi, Gazeti la JAMVI LA HABARI, likaamua kutumika kutushambulia. Likaitangazia dunia kuwa tumenunuliwa kusema ukweli huo. Likasema kampuni iliyopewa zabuni ya HID Global ina teknolojia ya kisasa na bei nzuri kuliko DeLaRue ya Uingereza. Likaonyesha kuwa DeLaRue tuliyoitaja ilipanga kutoa huduma hii kwa mikoa 8 ndani ya mkataba na iwapo Tanzania ingetaka kuingiza mikoa mingine iliyosalia basi kila mkoa ungelipiwa Sh milioni 341 na kuunganisha Balozi za Tanzania zote 41 ingeitoza nchi Sh bilioni 13.
Sisi tunalishukuru Gazeti la JAMVI LA HABARI kuwa kuthibitisha tulichokisema kuwa mradi huu kwa dola milioni 57 nchi ‘imepigwa’ hela ndefu. Tulisema nchi ingeweza kuokoa zaidi ya Sh bilioni 90, wao hilo wakajaribu kulipinga ila mtu akikamatwa ugoni hutoa kauli zisizopimika na kuishia kuthibitisha ukweli. Tanzania ina mikoa 31. Ina maana DeLaRue kwa kudai ilipwe Sh milioni 314 kama lilivyosema gazeti hilo, ukichukua kiasi hicho ukazidisha mara mikoa 23 iliyosalia unapata Sh bilioni 7.84. Kiasi hiki ukiongeza bilioni 13 za kuunganisha Balozi zetu kinakuwa Sh bilioni 20.84.
Hii ina maana kuwa ukichukua Sh bilioni 35.84, ambazo DeLaRue iliomba katika mradi huu kutengeneza ePassport ukajumulisha na Sh bilioni 20.84 za nyongeza, nchi ingetumia Sh bilioni 56.68 kukamilisha mradi huu. Kwa sasa tunatumia dola milioni 57 kuilipa HID Global ambazo ni sawa na Sh bilioni 129 hivi. Kwa dhana ya Gazeti tunaloamini linatumiwa bila kujua la JAMVI LA HABARI, bado nchi ingeokoa Sh bilioni 72.32. Wametoa madai ya kitoto kuwa DeLaRue ilitaka kutumia teknolojia inayolingana na karatasi za kuchapia magazeti. Hii ni aibu kwa Mhariri aliyepitisha habari hiyo au amethibitisha umbumbumbu wake, maana hata hati za sasa za kusafiria gamba lake ni gumu zaidi ya kurasa za magazeti.
Sisi tulichapisha habari hizi tukijua gharama yake. Tunafahamu baadhi ya wanaohusika kuwa wana utaalam wa kung’oa kucha, kutoboa macho na hata kuua watu wanaokwaza matamanio yao. Tumejitoa muhanga kwa ajili ya uzalendo na upendo kwa taifa letu. Tulichokifanya hakina tofauti na askari anayekwenda mstari wa mbele vitani akafia nchi yake. Tanzania walimu wanadai Sh bilioni 44 tu, deni ambalo Serikali ya Rais Magufuli imelirithi kutoka Serikali ya Awamu ya Nne. Fedha hizi zinazoelekea kuchezewa zingeweza kulipa deni lote hili na zikaongeza hata Sh bilioni 13 kwenye Bodi ya Mikopo, wanafunzi wote wa vyuo vikuu wakapata mkopo.
Tunapata uchungu kuona Rais Magufuli anakesha akitafuta fedha, akipambana kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato, kudhibiti rushwa, lakini wasaidizi wake wachache kwa tamaa binafsi wanafuja fedha tulizopata kwa jasho na damu kama nchi. Tunataka ufanyike uchuguzi wa kina katika tunachosema kuwa mfumo huu unapoanza unakuwa sawa na baiskeli. Passport ni nyaraka ya mwisho kwa mtengenezaji kama ilivyo baiskeli kiwandani. Kwamba huwezi kuzalisha baiskeli isiyo na usukani ikaitwa baiskeli.
Hivyo madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba kuwa e-Passport ni hatua ya kwanza, baadaye itakuja e-visa, e-boarder, e-migration na e-permit tunasema yachunguzwe ni kichochoro cha kuibia hela kwa kuhalalisha/kutakatisha dola milioni 57. Mfumo huu unapoingia mkataba wa e-passport vitu vyote hivyo vinakuwa ndani ya ‘software’ moja tunayoamini tayari hata HID Global wakiwa wakweli imeishafungwa.
Mwisho tunasema kwa sasa hatutaendelea na habari hii. Tunaipa Serikali nafasi ya kuchunguza na kuwawajibisha wahusika. Sisi tutaendelea kufuatilia kwa karibu na kila linapotokea jambo jipya kuujulisha umma kuhusiana na e-Passport. Tunaomba Serikali ifanye uchunguzi wa kina na wa haraka kuokoa fedha za walipa kodi. Pia, tunalisihi gazeti hilo linalotumika, ambalo ghafla limekuwa la kila siku wakati liliishaacha kutoka hata mara moja kwa wiki Mhariri wake aheshimu taaluma. Mwisho wa ubaya ni aibu. Mungu ibariki Tanzania.