Na WAF –Kagera,JamhuriMedia,Bukoba

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hadi kufikia Machi 25,2023 hakuna wagonjwa wapya wa Marburg walioripotiwa licha ya kupokea tetesi sehemu mbalimbali mkoani hapa.

Hayo ameyasema jana alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari nakusema kuwa ugonjwa huo unaendelea kudhibitiwa ambapo ameambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Zabron Yoti na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UNICEF Shalini Bahuguna

“Tangu kuanza kwa ugonjwa huu hadi leo tumeendelea kuwa na jumla ya wagonjwa walewale Nane waliothibitika ambapo Watano kati yao walifariki na Watatu wanaendelea na matibabu katika vituo vya kutolea huduma vilivyoainishwa.” amesema Waziri Ummy.

Aidha, waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Wadau mbalimbali inaendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu kwa kutekeleza mikakati mbalimbali.

“Miongoni mwa hatua ni kuwaweka sehemu maalumu watu wote waliohudumia wagonjwa ambao ni wanafamilia waliouguza wagonjwa na watumishi wa Afya waliohudumia wagonjwa kwa siku 21 ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu kama watabainika na maambukizi.” amesema Waziri Ummy

Katika kuendelea kudhibiti ugonjwa huo Serikali kupitia Wizara ya Afya imeongeza wataalam Sita wa afya ikiwemo daktari bingwa bobezi wa magonjwa ya Figo, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na wauguzi waliopata mafunzo maalumu kutoka maeneo mengine ili kusaidiana na wataalamu wa afya Mkoani Kagera.

Pia, Waziri ummy amewatoa hofu wananchi kuwa waendelee na shuhuri zao na amewakumbusha juu ya kuendelea kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara, kupeana nafasi na kuacha kugusana.

Waziri Ummy ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Kagera na wataalamu wote wa afya kwa kuwa mstari wa mbele kukabiliana na ugonjwa huo kwa jitihada zote zilizochukuliwa kwa kushirikiana kikamilifu na Wizara ya Afya katika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu.