Serikali imesema kuwa haitafuta tozo inayotozwa katika daraja la Kigamboni kwa kuwa fedha hizo zinatumika kulipa sehemu ya deni la mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Juni 22,2018 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu Antony Mavunde akisema kwa sasa utaratibu unaandaliwa ili wavukaji wawe na hiyari ya kulipa kwa siku, wiki au mwezi kulingana na uwezo wa mtu.
Alikuwa anajibu swali la mbunge wa Viti Maalum (Cuf) Zainab Mndolwa Amir ambaye ameomba kujua tangu kujengwa kwa daraja hilo Serikali imekusanya kiasi gani cha fedha kinachotokana na malipo kwa wanaovuka pamoja na vyombo vya moto.
Mbunge huyo pia amehoji iwapo Serikali itaweka utaratibu wa kutumia kadi maalum (smart card) kulipia kwa mwezi malipo kwa wanaovuka daraja huku akihoji ni lini wananchi wataanza kupita bure darajani hapo.
Mavunde amesema Serikali kupitia NSSF ndio wanaosimamia daraja hilo.
“Hadi kufikia Machi mwaka huu, NSSF ilishakusanya Sh 19.73bilioni tangu daraja hilo lilipoanza kutumika Mei 2016,” amesema Mavunde.
Amesema kwa sasa NSSF ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi wa kuweka mfumo utakaotumia kadi maalum ‘Smart Card’ kwa malipo ya wanaovuka darajani hapo.