Serikali imesema kuwa haikuruhusu mikutano ya hadhara ili watu wakavunje sheria, kutukana, kukashifu, kuchambua dini za watu.
Hayo yamesemwa na Rais amesema Rais, Samia Suluhu leo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Hali ya Siasa nchini.
Rais Samia amesema Serikali iliruhusu mikutano ya hadhara kwa lengo la kuwezesha vyama kuzungumza na kukua.
Alisema, “Tulitaka vyama vizungumze, wananchi wasikie sera zao, mada zao, mipango yao ili vyama vikue na virudishe watu wao walio wapoteza … vyama viwe madhubuti tukienda kwenye uchaguzi kila chama kimejijenga vya kutosha.”
Mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa vilizuiliwa kwa zaidi ya miaka sita kabla ya Rais Samia kutoa ruhusa ya shughuli hizo kufanyika.
Sambamba, alisema kuwa kuna uhuru wa maoni lakini uhuru huo una mipaka yake sio tu kisheria hata kibinadamu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba amemshauri Rais kuanzisha mabadiliko ya Katiba na kuibeba hiyo kama ajenda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025
Hata hivyo Rais Samia amesema Katiba ni mali ya Watanzania na kwamba viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kutoa maoni ili kuwezesha mchakato huo kufanyika.