Na Magrethy Katengu,JamhuriMedia Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema kamwe haikubliani na haitakubaliana na vitendo vya kihalifu wanavyofanyiwa baadhi ya watu wasio na utu wala ustaarabu dhidi ya watoto ikiwemo ubakaji,ulawiti, mauaji kwani itachukua hatua stahiki kwa wale wote watakaobainika kuhusika vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai,28, 2024 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamadi Masauni wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema vitendo hivyo viovu wanavyotendewa watoto vinaenda kinyume kabisa na utamaduni wa Taifa letu lenye sifa ya utu, ustaarabu , amani na utulivu hivyo wananchi wote ni budi kuungana kukemea vikali matukio ya aina hiyo na kuwafichua wahalifu kwani kufanya hivyo ni kusaidia watoto ambao ni taifa la kesho kuishi kwa amani .

” Niwahakikishie wananchi wote kuwa serikali kupitia vyombo vyake vya Usalama hususani Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi juu ya yeyote yule anayejihusika na vitendo hivi vya kihalifu kwani wanaotekeleza matukio haya ni watanzania na sio watu wanaotoka mbali na tunaishi nao wengine majirani,wazazi,walezi ikiwemo kaka, mjomba, babu, tuwafichue tusiwaache kwa kuwaogopa” amesema Waziri Masauni.

Sanjari na hayo Waziri Mhandisi Masauni amebainisha kuwa kupitia matukio hayo ya kihalifu dhidi ya watoto lakini kumeibuka tabia ya baadhi ya watu kutumia vibaya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kuzusha taarifa za uongo kwenye jamii zinazoleta taharuki na hofu kwa jamii wengine wakichukua video za zamani kuhusisha na sasa hivyo Jeshi la Polisi halitakaa kimya linaendelea kuwafutilia wahusika watakaobainika na kuchukulia hatua kali za kisheria.

Sambamba na hayo Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi kupitia Jeshi la polisi kwa kushirikiana Wizara ya nyingine imeweka mikakati madhubuti kutoa elimu kwa umma kuhusiana na utoaji malezi bora na ulinzi kwa watoto

” Kwenye hili tutaongeza nguvu zaidi kuanzia polisi kata nchi nzima pia kushirikisha Wizara ya Tawala.za Mikoa na Serikali za.mitaa , Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake.na makundi maalum , Wizara ya Katiba na sheria kufikia wananchi kwa kutoa elimu na kuimarika doria za mara kwa mara na kuongeza kasi ya ufuatiliaji na uchunguzi wa haraka pale matukio hayo yanaporipotiwa ili wahusika wawajibishwe kisheria ” amesisitiza Waziri

Aidha rai imetolewa kwa wananchi kushirikiana na serikali katika suala zima la ulinzi na usalama wa watoto kutambua kuwa jukumu hilo linaanzia katika ngazi ya familia .