Kifo cha msanii maarufu hapa nchini, Juma Kilowoko, maarufu kwa jina la Sajuki, kimeigusa Serikali na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), miongoni mwa wadau wa sanaa na Watanzania kwa jumla.

Sajuki aliyetoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha sanaa, hususani michezo ya kuigiza na filamu nchini, alifariki usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mrefu tangu mwaka 2010.


Rais Kikwete ambaye aliongoza mazishi ya Sajuki jijini Dar es Salaam, amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, akielezea kusikitishwa na kuhuzunishwa mno na kifo hicho.


“Kwa hakika kifo cha msanii huyu ni pigo kubwa katika tasnia ya michezo ya kuigiza na filamu, ambayo inaendelea kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania,” amesema kiongozi huyo wa nchi na kuongeza:


“Nakuomba wewe Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara, unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Juma Kilowoko kwa kuondokewa na kiongozi na baba wa familia… Namwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aipokee na kuilaza Mahali Pema Peponi roho ya marehemu Juma Kilowoko, amina.”


Kwa upande wake, Basata imeeleza kushtushwa na kuhuzunishwa na taarifa za msiba huo, huku ikitoa pole kwa familia ya marehemu Sajuki na wasanii wote nchini kwa kuondokewa na msanii huyo.


“Pengo aliloliacha (Sajuki) ni kubwa kwani ubunifu wake bado ulikuwa unahitajika katika tasnia hii (ya sanaa),” amesema Katibu Mtendaji wa Basata, Gonche Materego. Kifo cha Sajuki kimetokea, ikiwa ni takriban mwezi mmoja baada ya vifo vya wasanii maarufu nchini, Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’, Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ na John Stephano Maganga.


Wasanii hao wa uigizaji, filamu, muziki na tamthilia walikufa katika kipindi cha wiki moja. Wakati Sharo Milionea alikufa katika ajali ya gari, Mlopelo na Maganga walikufa baada ya kuugua kwa muda mrefu.