Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Serikali wilayani Kibaha, mkoani Pwani, imeeleza dhamira yake ya dhati ya kuunga mkono juhudi za wawekezaji katika sekta ya ufugaji nyuki ili kuhakikisha wafugaji wadogo waliopo vijijini wananufaika kiuchumi na kielimu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nikkison Simon, aliyewakilishwa na Ofisa Tarafa wa Kibaha, Catherine Njau, april 24,2025 wakati wa uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya Kibaha Environmental Conservation Action (KECA), shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utoaji elimu ya ufugaji wa nyuki na utunzaji wa mazingira, kata ya Mkuza.
Njau anaeleza, kwa muda mrefu wafugaji wa nyuki wanaoishi pembezoni mwa miji wamekuwa wakikosa elimu sahihi ya ufugaji wa kisasa na pia kukosa masoko ya uhakika kwa bidhaa zao.
Njau amelipongeza shirika la KECA ,akilitaja kama daraja muhimu kwa wafugaji wa nyuki kupata elimu ya kitaalamu na fursa za kibiashara.
Mjumbe wa Bodi ya KECA, Mzee Shunda, aliwahimiza wananchi na wadau wa mazingira kujitokeza kwa wingi kujifunza mbinu za ujasiriamali na ufugaji wa nyuki wa kisasa.
Nae Mkurugenzi wa KECA, Ibrahim Hussein Mkwiru, alieleza kuwa alianzisha shirika hilo baada ya kupata uzoefu, lengo likiwa ni kufikia wananchi wa kawaida kwa njia ya uhifadhi wa mazingira na ufugaji nyuki.
“Nia yangu ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa mazingira na kukuza uchumi wa wananchi kupitia ufugaji wa nyuki,” alisema Mkwiru.
Katika hatua nyingine, Mkwiru aliiomba Serikali kuwapa kibali cha kupanda miti ya mianzi katika maeneo ya wazi karibu na chanzo cha Mto Ruvu, ili kusaidia kuhifadhi mazingira na kuchochea maendeleo ya kijamii.
Hata hivyo, Ofisa Tarafa Njau alisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kitaalamu kabla ya kupanda mianzi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji,huku akisema baadhi ya miti ina uwezo wa kutumia maji mengi na hivyo inaweza kuhatarisha uhai wa vyanzo vya maji kama mito.
