Viongozi mbalimbali wa bara la Afrika na Umoja wa Mataifa wamekemea vikali kauli iliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu mataifa ya Afrika, Haiti na El Salvador alipokuwa katika kikao na wabunge wa nchi hiyo kilichofanyika White House.
Katika kikao hicho, Rais Trump alishangaa Marekani kupokea wahamiaji kutoka katika nchi hizo huku akitumia neno ‘shithole’ (tundu la choo) akimaanisha ni nchi za Afrika Haiti na El Salvador na kwamba Marekani haihitaji wahamiaji kutoka katika nchi hizo, badala yake inataka wahamiaji kutoka Norway.
Kufuatia kauli hiyo, serikali ya Tanzania imetoa msimamo wake na kueleza kwamba inaunga mkono maazimio ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mtaifa kwani ni moja wapo wa nchi wanachama wanaounda jumuiya hizo za kimataifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amesema kwamba kauli ya Tanzania juu ya Rais Trump imewakilishwa vizuri na Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU).
UN imeeleza kwamba, hakuna namna nyingine ya kuelezea kauli iliyotolewa na Rais Trump zaidi ya ubaguzi wa rangi huku AU nayo ikisema kauli hiyo ni ya kibaguzi.
Kwa upande wake Rais Trump, amekanusha kutumia neno hilo na kuzihusisha na nchi za Afrika, Haiti na El Salvador huku akikiri kwamba alitumia lugha nzito lakini siyo tusi hilo (shithole).
Botswana ndio taifa la kwanza Afrika kuzungumzia kauli hiyo ya Rais Trump ambapo serikali ilimuita Balozi wa Marekani nchini humo na kutaka aeleze kama Botswana ni miongoni mwa nchi alizozitusi Rais Trump.
Idara ya Mambo ya Nje ya Chama cha ACT Wazalendo imesema kuwa, kauli ya Rais Trump iwe ni kengele ya kuwaamsha viongozi wa kiafrika waweze kuhakikisha wanajitegemea kiuchumi na kutokomeza umasikini.