Haikuwa kazi rahisi kwa Serengeti Boys kutawala mchezo kwa kiwango cha asilimia 58 dhidi ya asilimia 42 ya wapinzani wao, Nigeria, katika mechi ya ufunguzi wa Michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Ingawa Serengeti Boys ilinyukwa mabao matano kwa manne katika mchezo huo wa Jumapili iliyopita, Kocha wa timu hiyo ya Nigeria, maarufu The Golden Eaglets, Manu Garba, hakuwa na hiyana isipokuwa kukiri kuwa vijana hao wa Tanzania si haba, vipaji vipo na matumaini yapo.
Ni kweli Serengeti Boys imeanza vibaya safari yake katika michuano hii lakini hiyo haina maana ndoto za kufanya vizuri zimetoweka.
Serengeti Boys kwa namna fulani wameonyesha kiwango cha soka cha kuridhisha ingawa yanahitajika marekebisho maeneo kadhaa ili kuimarisha timu hiyo.
Maeneo yanayohitaji marekebisho kwenye kikosi hicho ni pamoja na safu ya ulinzi, eneo la kati na langoni.
Katika mchezo huo golikipa Mwinyi Yahya hakuwa kwenye kiwango cha juu cha ubora, na hapa ndipo kocha pamoja na wasaidizi wake wanapohitaji kuwekeza zaidi nguvu na maarifa.
Timu ya Serengeti Boys si ya kubeza, hasa kwa kuzingatia rekodi yake wakati wa maandalizi kabla ya michuano hii.
Lakini ukiondoa marekebisho hayo yanayohitajika, mchezo huo wa ufunguzi haukuwa na mahudhurio mazuri.
Licha ya kuwapo kwa uhamasishaji lakini mashabiki wa soka hawakuweza kujitokeza kwa wingi kama ilivyotarajiwa.
Kwa sasa Serengeti Boys wamebakiza mechi mbili, dhidi ya Angola na Uganda. Endapo watafanikiwa kushinda michezo yote watajihakikishia nafasi ya kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali na hata kupata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Maelezo ya Kocha wa Serengeti, Oscar Milambo, kwamba wamekuwa wakiwafundisha watoto wadogo hivyo hawawezi kuelewa vitu vingi kwa muda mfupi ni changamoto nyingine katika kuzidi kuiboresha timu hiyo kisaikolojia.
Bila shaka bado Watanzania wanayo matumaini makubwa kwa Serengeti Boys, hasa nyota wake kadhaa akiwamo Kelvin John.
Ukiondoa ushindani kati ya timu zinazoshiriki michuano hii, kwa upande mwingine inapambanisha wasifu (CV) za makocha. Kwa mfano, Kocha Garba ni mwenye mafanikio makubwa katika michuano ya aina hii, akiwa ameiwezesha The Golden Eaglets kubeba taji hili mara tatu, na Kombe la Dunia kwa vijana mara mbili.
Hii ni mara ya pili kwa Serengeti Boys kushiriki mashindano haya, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2017 nchini Gabon, lakini timu hiyo iliishia hatua ya makundi.
Michuano ya mwaka huu inahusisha timu nane zilizopangwa makundi mawili, kundi ‘A’ likijumuisha timu za Tanzania, Nigeria, Uganda na Angola, na kundi ‘B’ likihusisha Morocco, Senegal, Cameroon na Guinea.