Septemba 9, mwaka huu Rais John Magufuli alipokuwa akizungumza na wananchi akiwa Meatu mkoani Simiyu aligusia uzazi wa mpango.

Baada ya kuona, kusikia na kusoma mitazamo na maoni ya watu mbalimbali juu ya hoja aliyoitoa Rais Magufuli, nimeona nami nichangie mawazo kidogo juu ya hili; na kwa kweli kukazia maarifa juu ya kile alichokisema na mtazamo wake thabiti kwa masilahi ya taifa letu.

Kimsingi, Rais Magufuli alionyesha kukerwa na upangaji wa uzazi kwa mwelekeo wa kupunguza idadi ya watu, ambao tumeletewa na nchi za Magharibi ambazo zimekwisha kuachana na sera hiyo na sasa zinaongeza watu wao.

Rais Magufuli alisema: “Tunatakiwa Watanzania kuchapa kazi ili utakaowazaa uwalishe… wale ambao hawafanyi kazi – wavivu wavivu, ndio wanaopangiwa watoto.”

Akasema mtu ambaye anategemea mnazi mmoja kwa mwaka mzima atawezaje kuzaa [uwezo wa kuwa na nguvu za kuzalisha kwa mwanaume] au kupata maziwa ya kumnyonyesha mtoto [kwa wanawake].

Hapa anahimiza na kusisitiza juu ya umuhimu wa watu kufanya kazi kwa bidii ili waweze kumudu maisha yao na wanaowategemea kwa ustawi wao, kwa maana kwamba si kuzaazaa tu, bali kuzaa watoto ambao mtu anaweza kuwahudumia. Ndiyo maana anasisitiza juu ya hoja yake kwa kusema: “Ninachowaambia limeni, fanyeni kazi; ukiwa na chakula cha kutosha zaa.”

Anamaanisha mtu azae kadiri ya uwezo wake na si kupangiwa azae wangapi. Rais Magufuli, ni wazi kwamba anaonyesha fikra na mtazamo wake juu ya kupanga uzazi kwa mwelekeo wa kuongeza idadi ya watu kwa maendeleo ya nchi.

Idadi ya watu katika familia/nchi huathiriwa na sera ya idadi ya watu ya nchi husika. Sera ya idadi ya watu hutengenezwa na nchi husika kwa ajili ya kuratibu mambo mbalimbali kuhusu idadi ya watu. Mfano, kama nchi inataka kuwa na wanaume wengi kuliko wanawake au kinyume chake; pengine nchi inahitaji kuwa na idadi kubwa ya watu au kinyume chake, kushusha idadi ya vifo nchini, kuongeza kiwango cha umri wa watu kuishi [Life expectancy] na kadhalika.

Kuna aina mbili za sera za idadi ya watu: Mosi, sera ambayo haiko wazi juu ya idadi ya watu, [Implicit population policy], upangaji wa uzazi hauko wazi. Hii ni sera ambayo huwa haiandikwi [hakuna nyaraka iliyo katika maandishi] juu ya idadi ya watu katika nchi; bali mipango mbalimbali ya kimaendeleo na ustawi wa watu, mfano utoaji elimu bora, kuboresha afya, kupunguza utegemezi, kilimo bora, kupunguza umaskini na mambo kama hayo husisitizwa na serikali. Tulikuwa tunatumia aina hii ya sera hadi mwaka 1992. Upangaji wa vijiji vya ujamaa, elimu kwa watu wazima na mipango mbalimbali iliyokuwa ikitekelezwa na serikali ni mifano halisi katika hili.

Pili, ni sera ya wazi juu ya idadi ya watu [Explicit population policy]: Hapa upangaji wa uzazi uko wazi kabisa. Hii ni sera ambayo huandikwa [huwa kuna nyaraka iliyo katika maandishi] kuratibu mambo mbalimbali juu ya idadi ya watu katika nchi husika. Mfano, ukuaji wa idadi ya watu [Population growth], wastani wa miaka ya kuishi kwa watu katika nchi [Life expectancy], uhamiaji wa watu katika nchi [immigration], kiwango cha kuzaliana [Fertility rate] na kadhalika. Tanzania iliingia kwenye mfumo wa sera ya namna hii mwaka 1992 na ilifanyiwa marekebisho mwaka 2006.

Sera ya wazi juu ya idadi ya watu [Explicit population policy] imegawanyika katika mitazamo ya aina mbili kiutekelezaji kuhusu uratibu wa idadi ya watu. Upande mmoja ni ule wenye mtazamo wa kupunguza idadi ya watu [Restrictive population policy]. Nchi takriban zote za Ulaya na Marekani zilikwisha kutumia sera hii; kwa Asia ni Japan, China, Singapore na nyinginezo; kwa Afrika nchi nyingi zinatumia aina hii ya sera kama vile Nigeria na Tanzania [tangu mwaka 1992] hadi sasa.

Kwa upande mwingine, ni sera ya wazi juu ya idadi ya watu inayohamasisha kuongeza idadi ya watu [Pro-notary population policy]. Hii ndiyo aina ya sera ya idadi ya watu ambayo kwa sasa imekuwa ikikimbiliwa na takriban nchi zote za Ulaya, Marekani, Asia na nyingine zilizokwisha kukumbwa na madhara ya kupunguza idadi ya watu wao. Nchi hizi zote zinafanya hivi kuhami mustakabali wa maendeleo yao.

Kulingana na fundisho tunalopata kutokana na historia ya idadi ya watu duniani, hasa kuhusu maendeleo ya nchi na idadi ya watu, uzoefu kutoka Magharibi na Mashariki kuhusu kupanga uzazi kwa mtazamo/mwelekeo wa kupunguza idadi ya watu si hatua rafiki hata kidogo kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.

Nchi nyingi duniani kama vile China, Marekani, Canada, Urusi, Ufaransa na kadhalika zimekwisha kuachana na sera za mrengo wa kupunguza idadi ya watu – kwa muda mrefu sasa baada ya kuona madhara yake.

Ni kwa msingi huo, bila kusitasita wala kupepesa macho, napendekeza kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa kupitia Bunge; kufanya marekebisho kama si mabadiliko ya msingi kabisa katika sera yetu ya idadi ya watu ya mwaka 1992 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 ili tuendane na hali halisi ya mahitaji yetu kama nchi.

Sera yetu ya idadi ya watu kwa sasa ina mrengo wa kupunguza idadi ya watu [Restrictive population policy] ambayo kwa kweli imepitwa na wakati kwa masilahi ya nchi. Kwa sasa tunahitaji sera inayohimiza kuongeza idadi ya watu [Pro-notary population policy] kama Rais Magufuli anavyotamani.

Rais wangu, Dk. Magufuli asiishie tu kusema “zaa”, badala yake aende mbele zaidi kuhakikisha kuwa sera ya idadi ya watu inabadilishwa kama si kurekebishwa ili ielekeze kuongeza idadi ya watu nchini [mkazo uwe kwa njia ya asili ya kuzaana, si kujaza wahamiaji kutoka nje] kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu la Tanzania.

Hoja ni kwamba tunaongeza idadi ya watu [tunasisiza kuzaana sana] ili kuhami maendeleo ya nchi yetu kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Na kwamba, tutaendelea kufanya mabadiliko, na au marekebisho kadiri tutakavyoona inatufaa kwa wakati husika.

Ukweli ni kwamba, kwa namna yoyote ile iwayo; ongezeko la idadi ya watu nchini halikwepeki – iwe kwa njia ya asili ya kuzaliana au njia isiyokuwa ya asili ya kuwapa uraia wahamiaji kutoka nchi mbalimbali kuwa Watanzania.

Haitashangaza kwa baadaye [hata sasa imeanza] kusikia au kuona timu fulani ya michezo ikiwakilisha nchi, huku wengi wa wachezaji wakiwa watu kutoka nchi nyingine [Watanzania kwa uraia, ila wananchi wa nchi nyingine].

Ndipo hapo tutaendelea kusikia tu – Mtanzania mwenye asili ya China, Mtanzania mwenye asili ya India, Mtanzania mwenye asili ya Rwanda, Mtanzania mwenye asili ya Kenya na kadhalika.

Mwandishi wa makala hii, Gorwe Waryoba, ni msomaji wa JAMHURI na kitaaluma ni mwalimu. Anaishi Mwanza. Anapatikana kwa simu: 0762 380 283; barua pepe: [email protected]