Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametoa wito kwa Halmashauri ya jiji la Dodoma na Kamati ya ardhi kufanya kazi kwa weledi ili kuutendea haki Mpango Mkakati wa kutokomeza kero za migogoro ya ardhi ambayo imekuwa mwiba mchungu kwa wananchi na kuchafua taswira ya jiji hilo kwa muda mrefu.

Wito huo umetolewa Julai 18, 2023 wakati akizundua Mpango Mkakati wa Mkoa wa kushughulikia migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma halfa iliyohudhuriwa pia na Watumishi wa Halmashauri ya Jiji hilo, Madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa na Kamati ya Amani yenye wajumbe kutoka (dini mbambali) na vyombo vya habari.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na washiriki wa kikao katika hafla ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Mkoa wa kushughulikia migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma. Uzinduzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mkutano Jengo la Mkapa tarehe 18. 7. 2023.

“Kwa muda mrefu Mamlaka mbalimbali za Serikali zimekuwa zikijitahidi kutatua migogoro hii lakini imekuwa haiishi na wananchi kuendelea kulalamikia Serikali. Kwa uchunguzi tuliofanya kama Mkoa tulibaini malalamiko mengi ni ya fidia na watu walioahidiwa kupewa viwanja mbadala. Kimsingi maelekezo mbalimbali yalikuwa yanatolewa ili kutafuta ufumbuzi wa suala hili.

“Napenda kuujulisha umma huu kuwa tarehe 27/06/2023 niliunda Kamati Maalumu ya kushughulikia tatizo hili na mnamo tarehe 7/7/2023 Kamati imewasilisha Mkakati ambao pamoja na hatua nyingine kama Mkoa tumejipanga kuutekeleza ili kutatua migogoro ya ardhi mkoani Dodoma. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiagiza kusikiliza kero za wananchi na kutoa ufumbuzi lakini pia dhamira ya kutaka kuona Jiji la Dodoma linakuwa Jiji bora na lenye hadhi” ameeleza Senyamule

Pia,Senyamule amesema mkakati huo wa muda mfupi na muda mrefu utaenda kuhakikisha migogoro katika jiji la Dodoma inamalizika na kuwafanya wananchi wa Dodoma kuishi kwa Amani, utulivu na kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki katika hafla ya Uzinduzi Mpango Mkakati wa kushughulikia migogoro ya ardhi namna walivyojipanga kutekeleza mkakati wa kutokomeza migogoro ya ardhi inayoikumba jiji la Dodoma uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jengo la Mkapa Julai 18, 2023.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Uongozi wa Jiji wamejipanga vizuri katika kuhakikisha wanatatua changamoto za ardhi zilizopo kupitia Mkakati huo uliopangwa kutekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja ambao utekelezaji wake unaanza Julai 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo juni 2024.

‘’Nikuhakikishie Mkuu wa Mkoa mimi na timu yangu tumejipanga vizuri kutekeleza Mkakati huu tutafanya vizuri kwasababu tumepanga sisi wenyewe kwahiyo kwa kujiamini tutasimamia na tutakuwa wakali kwa wote watakaotaka kutukwamwisha katika zoezi hili” Amesema Shekimweri

Kwaupande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma Jabir Singano amesema katika kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa wataendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma katika kuongeza idadi ya watumishi wa ardhi ili kuongeza nguvu kazi ya kutatua kero hizo.

Katika kikao hicho Senyamule amezitaja changamoto zitakazopatiwa ufumbuzi ni pamoja na Madai ya viwanja mbadala, Madai ya fidia, Madai ya upimaji shirikishi wa asilimia 70 kwa 30, Uvamizi wa viwanja, ucheleweshaji wa Hati miliki, ukosefu wa huduma bora kwa wananchi, Miliki pandikizi na mabadiliko katika Usimamizi wa Sekta ya Ardhi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizindua Mpango Mkakati wa Mkoa wa kushughulikia migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jengo la Mkapa tarehe 18/07/2023.
Katika picha ni baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wa kutokomeza migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma uliozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tarehe 18/07/2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi yake Jengo la Mkapa.
Please follow and like us:
Pin Share