Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es

SEKTA ya Uchukuzi na Usafirishaji imetakiwa kushirikiana na kujadiliana mara kwa mara, ili iweze kuongeza tija na ufanisi kwa nchi.

Mkutano huo mkubwa wa siku moja uliwakutanisha wadau wa sekta ya uchukuzi kwa njia ya maji, anga, reli na barabara, kujadaliana pamoja changamoto zinazowakabili na utatuzi wake pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji kupitia sekta hiyo na kuikuza zaidi.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Masoko Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Fatma Adadi ambaye alimuwakilisha, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa mamlaka hiyo Dkt. George Fasha kwenye Mkutano wa pili wa Uchukuzi na Usafirishaji – East Africa Cargo Connect Summit uliofanyika mwishoni jijini Dar es Salaam.

Fatma aliwapongeza wadau wa uchukuzi na usafieishaji kuandaa mkutano huo, hivyo kuwasisitiza umuhimu wa kukutana mara kwa mara na kujadili sekta hiyo ambayo imekuwa na mchango mkubwa kwenye kukuza uchumi na maendeleo.

“Nitumie nafasi hii kuwasisitiza umuhimu wa kukutana mara kwa mara na kuzungumzia sekta yenu ambayo imekuwa na mchango mkubwa kwenye kukuza uchumi, sisi TPA tutaendelea kushirikiana na nyie kila wakati,” alisema.

Ofisa Masoko huyo alisema kupitia vikao hivyo vya majadiliano watakuwa wanatoka na maazimio chanya yatakayoleta mchango mkubwa wenye kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za uchukuzi zikiwemo za kibandari.

Aidha, Fatma amewataka wadau wa sekta ya uchukuzi na usafirishaji kuiboresha sekta hiyo na kuhakikisha utoaji huduma unaendelea kuwa bora zaidi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya EB Maritime, Emmanuel Mallya ambaye alipewa Tuzo ya Lifetime Achievement, alisema katika mnyororo wa sekta hiyo kuna maeneo manne muhimu yanapaswa kutambulika, ambayo ni wamiliki wa meli, mamlaka ya bandari, wamiliki wa mizigo na mamlaka za kikodi.

Mallya alisema kupitia maeneo hayo manne sekta ya bandari hasa Tanzania imekuwa nzuri, hivyo kuwezesha sekta zingine kama reli, barabara na bandari kavu kufanya kazi vizuri na kwa faida.

Alisema mkutano huo una nafasi kubwa ya kuwafanya wajadiliane na kutoka na matokeo chanya ambayo yataleta mabadiliko kwa haraka.

“Sisi tumekutana hapa kwa siku moja tunapaswa kutoka na suluhisho ambalo litaleta mabadiliko kwenye sekta hii muhimu kwenye uchumi wa nchi,” alisema.

Kupitia mkutano huo ambao umedhamiwa na TPA na kushirikisha wadau wa sekta ya uchukuzi na usafirishaji kutoka nchi za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Ksini mwa Afrika ( SADC) na Afrika Magharibi, tuzo mbalimbali za umahiri zilitolewa.

Moja ya tuzo ilitolewa kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, ambayo ni Tuzo ya Umahiri kwa Kiongozi mwenye Maone katika Sekta ya Uchukuzi kwa Njia ya Maji “The Tanzania Maritime Visionary Leadership Award”