Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 51.66 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali katika Sekta ya Mifugo kwa ujenzi wa miundombinu ya minada ya mifugo ya kisasa 51 shilingi bilioni 17.5 , ujenzi wa Majosho 746 kwa gharama ya shilingi bilioni 15.92 katika Halmashauri mbalimbali nchini na kuchangia kuongezeka kwa idadi ya mifugo inayoogeshwa.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 16,2024 Jijini hapa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdala Ulega wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa hatua hiyo itapunguza magonjwa ya mifugo yaenezwayo na kupe kutoka asilima 72 hadi asilimia 48.
Ujenzi wa Vituo 10 vya kukusanyia Maziwa kwa shilingi bilioni 2.5
Mbali na hayo amesema Serikali imejenga U Mabwawa 15 kwa shilingi bilioni 8.04 kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na kuchangia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa mifugo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu katika vyuo vya mafunzo ya mifugo shilingi bilioni 4.4 ambao umehusisha ujenzi wa Hosteli mbili (2) zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 424 kila moja na kumbi 10 za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 hadi 150 kila mmoja.
Licha ya hayo ameeleza kuwa katika kuhakikisha kwamba Wanawake na Vijana wanajikwamua kiuchumi, Serikali kupitia Wizara hiyo ilianzisha Program ya Jenga Kesho iliyobora (maarufu kama BBT) kwa kuwawezesha Vijana na Wanawake 200 kupata mafunzo ya ujasiliamali, mbinu bora za uvuvi na ukuzaji viumbe maji ambao wamehitimu kwenye awamu ya kwanza.
Aidha, vijana na wanawake 300 wanaendelea na mafunzo katika awamu ya pili ambapo kati ya hao Vijana 50 ni kutoka Zanzibar na kwamba itahakikisha kuwa rasilimali za uvuvi zinasimamiwa ipasavyo ili kuwa na uvuvi na ukuzaji viumbe maji endelevu, maendeleo ya viwanda, ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla.
Ulega pia amesema katika kuendeleza uzalishaji wa zao la mwani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inashirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kuendesha kiwanda cha kuchakata mwani kilichopo Zanzibar chenye uwezo wa kuchakata tani 30,000 kwa mwaka kwa kuongeza upatikanaji wa malighafi ya mwani kutoka Tanzania Bara ambapo kwa sasa uzalishaji wa zao hili kwa Tanzania Bara umefikia tani 8,343.75.
Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukitumia Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Machui Tanga kupata vifaranga vya samaki na viumbe maji wengine wakiwemo jongoo bahari kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa buluu.
“Kutokana na uwepo wa kiwanda hicho, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Maendelo ya Kilimo (TADB) imewakopesha wakulima wa mwani mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba kwa kuwapatia vifaa na pembejeo za kilimo cha mwani ambapo jumla ya shilingi 447,000,000 zilitumika kwa kukopesha kamba za mwani 22,983, tai tai 102,911 na mbegu za mwani kilo 228,805, mambo/vigingi 137,215 na viroba/mifuko 1,029,”amesema
Amesema Sekta ya Mifugo ikiwa ni miongoni wa Sekta za Kiuchumi na Uzalishaji ambayo inatoa ajira kwa wananchi wengi wa Tanzania, inaendelea kukua kwa asilimia 5.0 na mchango wa Sekta katika pato la Taifa (GDP) ulifikia asilimia 6.7 kwa mwaka 2022 huku Idadi ya mifugo nchini ni ng’ombe milioni 36.6, mbuzi milioni 26.6 na kondoo milioni 9.1. Pia, kuku waliopo ni milioni 97.9 ambapo kuku wa asili ni milioni 45.1, kuku wa kisasa milioni 52.8 na nguruwe ni milioni 3.7.
Kuhusu Uzalishaji wa nyama amesema umeongezeka kutoka tani 97,000 mwaka 1964 hadi tani 738,166 mwaka 2023. hii imetokana na kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama kutoka kiwanda kimoja mwaka 1964 (Tanganyika Parkers) kilichokuwa na uwezo wa kuchinja ngombe 800 kwa siku hadi viwanda 11 vyenye uwezo wa kusindika tani 337 kwa siku.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya hivi karibuni, Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/21 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2022/23. Hivyo kufanya jumla ya tani 35,297 zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 146.43 zilizouzwa nje ya nchi, “amesisitiza.
Waziri huyo pia amesema uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 334,000 mwaka 1964 hadi lita bilioni 3.4 mwaka 2022/2023 na usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka wastani wa lita 41,026,000 kwa mwaka 1964 hadi wastani wa lita milioni 75.9 kwa mwaka 2023. Aidha, Viwanda vya kusindika maziwa pia vimeongezeka kutoka viwanda saba (7) vya umma mwaka 1974 hadi kufikia viwanda vya sekta binafsi 105 mwaka 2023.
” Wizara pia imekuwa na ushirikiano na sekta binafsi katika kukuza sekta ya maziwa nchini. Kwa mfano Shirika la Heifer International limeweza kuimarisha mnyororo wa thamani kwa kuwapatia wafugaji wadogo kote nchini jumla ya mitamba bora wa maziwa 282,000, kuku 62,000 na kondoo 57,200 na kujenga vituo 22 vya kukusanyia maziwa vyenye uwezo wa kukusanya lita 70,000 za maziwa kwa siku, “amesema.