đź“ŚWaziri Mavunde asisitiza wanawake washiriki zaidi katika uchumi wa madini
đź“ŚSTAMICO yapongezwa uwezeshwaji wanawake
đź“ŚMhandisi Mbenyange wa STAMICO apokea tuzo Mwanamke wa pekee
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa, Wizara ya Madini imevutia ushiriki wa wanawake katika uvunaji wa rasilimali hiyo muhimu katika uchumi wa Madini nchini.
Hayo yamebainishwa Machi 1, 2023 na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Jerry Slaa akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa wanawake wanaoshiriki kwenye Sekta ya Uziduaji kama Sehemu ya maadhimisho ya wiki ya wanawake jijini Dar es Salaam.
“Wanawake wanaojishughulisha kwenye shughuli za Sekta ya Madini wamekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uchumi wao na Pato la Taifa,” amesema Dkt. Slaa.
Aidha, ameipongeza wizara kwa kuendelea kubuni sera mbalimbali zinazowawezesha wachimbaji wadogo hususani wanawake kwa kuwa mstari mbele kusimamia na kuchimba kwa teknolojia inayowawezesha kulipa kodi za Serikali na kusaidia jamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa, wanawake wanaweza kushiriki katika shughuli mbalimbali zilizomo katika mnyororo mzima wa thamani madini ikiwemo, utafiti, uchimbaji, uchakataji, uongezaji thamani, uuzaji wa madini na utoaji huduma katika sekta ya madini.
“Uchimbaji wa madini unahusisha shughuli nyingi sio lazima mwanamke akashiriki moja kwa moja kuchimba bali kufanya kazi zinazoenda sambamba na uchimbaji na kiweza kujikwamua kiuchumi katika jamii yetu.” Alisisitiza Waziri Mavunde
Alibainisha kuwa kupitia dira ya Sekta ya Madini ya 2030, Madini ni Maisha na Utajiri, Serikali imeweka mazingira wezeshi katika kuhakikisha kila mtanzania hususani wanawake wananufaika na rasilimali madini ikiwemo kuweka mazingira ya upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji, masoko na mikopo.
Alisema tayari Serikali imetoa leseni za maeneo ya uchimbaji kwa zaidi ya makundi 15 huko mkoani Geita, sambamba na kuwekwa kwenye mpango wa kufanyiwa utafiti na kupatiwa vifaa vya uchimbaji kupitia STAMICO.
Mhe. Mavunde amesema Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa STAMICO imeendelea kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele na kuwezeshwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za madini zikiwemo uchimbaji madini, utafitaji masoko, uongezaji thamani yakiwemo madini ya makaa ya mawe.
“STAMICO inafanya kazi kubwa sana katika kuwalea na wachimbaji wadogo hususani akina mama, na kupitia Uzalishaji wa Mkaa Mbadala wa Rafiki Briquettes tumechagua vikundi vya kina mama katika mikoa tofauti na kuwapa uwakala ili waweze kuuza mkaa huu na kujiinua kiuchumi” aliongeza Mavunde
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji (TAWOMA) Bi. Semeni Malale ameishukuru wizara ya madini kupitia STAMICO kwa kuweka sera zinazomwezesha mwanamke kuingia katika shughuli za uchimbaji.
Amesema kwa sasa Serikali imeweka sera zinazohasisha usimamizi mzuri wa rasilimali madini zinazomuwezesha mwanamke kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uchimbaji madini wanawake kusaidia jamii.
Aidha ametoa rai kwa serikali kuweka mpango wa kurudisha ruzuku kwa wachimbaji wadogo itakayojikita katika kulipia gharama za utafiti na uchorongaji moja kwa moja ili kuwasaidia kupata taarifa sahihi za Maeneo yao ya uchimbaji.
Sambamba hilo Wizara ya Madini kupitia STAMICO imemtoa mshindi Mhandisi Happy Mbenyange aliyejinyakulia Tuzo ya Mwanawake wa Pekee katika Sekta ya Uziduaji 2024, tuzo zilizoandaliwa kwa kushirikiana, kampuni ya Ecograph, Kampuni ya Azurite Management and Consultancy pamoja na PreIWD ili kutambua mchango wa Mwanamke katika sekta ya uziduaji nchini ikiwa na kauli mbiu ya Twende Pamoja Haraka; Moja kwa Moja
Hafla ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kiwemo, katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju, Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Mkuu wa Mkoa wa Iringa na viongozi mbalimbali wa Serikali.