Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na kauli kuwa Tanzania ni ghali sana katika Sekta ya Utalii kwa maana ya gharama anazotumia mtalii kuanzia safari ya anakotoka hadi gharama atakazotumia awapo nchini.
Kwanza, ieleweke kuwa gharama hizi zitumiwazo na watalii zimegawanyika katika maeneo makuu matatu ambayo ni:
1. Gharama za tiketi za ndege ya anakotoka na kurudi mtalii.
2. Gharama za mtalii awapo nchini kupitia anayeratibu safari yake, ambazo ni pamoja na usafiri wa ndani, malazi na chakula.
3. Gharama zinazotozwa na maeneo ya hifadhi kama vile TANAPA, TAWA, NCAA, TFS na yale ambayo pia yanasimamiwa na sekta binafsi.
Inavyoongelewa mara zote ni kama vile eneo la tatu la maeneo ya utalii ndiyo kana kwamba yanafanya utalii uwe ghali nchini na kusababisha kuwa na maombi ya mara kwa mara ya kutaka maeneo haya yanayosimamiwa na serikali yapunguze tozo zake, kitu ambacho si kweli.
Leo nitajaribu kwa uchache kabisa kuainisha gharama hizi na kuona kile ambacho kinakwenda mfukoni mwa serikali na kile ambacho kinakwenda mfukoni mwa sekta binafsi na kuona ni upande upi unatakiwa kuangalia namna bora ya kurekebisha gharama hizi kwa mustakabali mwema wa sekta ya utalii nchini mwetu.
Nitaanza na mfano mmoja wa gharama za kupanda Mlima Kilimanjaro. Gharama zinazotozwa na makampuni ya watalii kwa mtalii anayetaka kupanda Mlima Kilimanjaro ni kati ya *dola za Marekani 1,900 hadi 2,800* kwa mtalii mmoja.
Gharama hizi hazihusishi tiketi ya kwenda na kurudi anakotoka mgeni, ambazo zinatofautiana kulingana na mgeni anatoka wapi.
Ukichukua wastani wa chini wa dola 1,900 anazolipa mtalii, kiasi kinachokwenda kwenye gharama za Kilimanjaro ni kama ifuatavyo:- Kwa njia ya Marangu ya siku tano ni tozo ya kiingilio dola 82.6 kwa siku 5, ambayo ni sawa na dola 413; Hut fees anapolala mgeni ni dola 70.8 kwa siku 5, ambayo ni sawa na dola 354; Gharama za uokoaji ambayo ni dola 23.6. *Jumla ya gharama hizi pekee kwa njia ya Marangu ni dola 790.6*.
Hii inamaanisha kuwa katika dola 1,900 anazochajiwa mgeni ukiondoa hizi 790.6, zinazobaki kwa kampuni ni dola 1,109.4. *Hii maana yake ni kuwa ukiwa na wageni 10 wanaopanda mlima unapata faida ya dola za Marekani 11,094*
Katika mazingira haya ambapo pamoja na kuwa bado kuna gharama za kulipa wapishi na waongoza wageni na kodi nyinginezo, bado kiasi kinachotozwa kinabakiza sehemu kubwa ya faida kwa sekta binafsi na kile kinachoingia kwenye serikali kupitia tozo za hifadhi ni kidogo sana.
Ukichukua mfano mwingine wa kawaida sana wa safari ya siku tano ya Arusha, Ziwa Manyara, Serengeti na Ngorongoro, safari hizi huchajiwa kati ya *dola za Marekani 2,500 hadi 3,000* ambazo pia hazihusishi gharama za tiketi ya mgeni kuja na kuondoka nchini.
Katika tozo hizi gharama kwa maana ya tozo za hifadhi kwa siku zote hizo tano ni kiasi cha dola 751 tu, ambazo zitalipwa kwa Hifadhi za Arusha, Ziwa Manyara, Serengeti pamoja na Ngorongoro.
Utaona wazi kuwa ukiondoa dola 751 kati ya zile 2,500, kiasi kinachobaki chote cha dola 1,749 kinabaki kwenye sekta binafsi.
Hapa pia tukumbuke kuwa hizi ni gharama kwa kichwa kimoja, maana yake kwa wageni 10, hii ni sawa na faida ya dola za Marekani *17,490*
Aidha, huduma za malazi katika baadhi ya hoteli za sekta binafsi ambazo hutoza wakati wa Msimu wa Juu wa Utalii au (High Season) kiasi cha dola kati ya 400 hadi 600 kwa kichwa kwa siku, kwa siku 90 au miezi mitatu ya msimu ambayo ni Julai, Agosti na Septemba hujikusanyia kiasi cha dola wastani wa *36,000 hadi 54,000* kwa chumba kimoja.
Katika mazingira haya, je, ni kweli gharama zinazotozwa na wadau wa sekta binafsi si kubwa sana kulinganisha na kile kinacholipwa kwa maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya utalii?
Mifano hii michache hapo juu inalenga kuibua mjadala juu ya nini kifanyike ili sekta binafsi nazo zishiriki kuhakikisha kuwa gharama zetu kwa wageni zinakuwa katika mazingira rafiki ya kuvutia watalii wengi zaidi nchini.
*Lakini pia ufike wakati sasa hata kilio cha muda mrefu cha watalii kutaka gharama hizi ziwe wazi kifanyiwe kazi, kwani kwa hivi sasa bado gharama nyingi zinazotozwa na sekta hizi binafsi ni siri baina ya kampuni hizi na wageni. Bado kuna mazingira ya usiri mkubwa sana tofauti na biashara nyingine zinavyofanyika*
*Nkolosikazi wa Ungindoni*