Jamii ya wafugaji wa Kimasai ni miongoni mwa jamii zilizo nyuma katika mambo mengi ya kimaendeleo, hasa elimu.
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kulitambua hilo, imeamua kuwekeza kwa nguvu kubwa kwenye elimu. Kutokana na jiografia ya Wilaya ya Ngorongoro, shule zinazofaa ni za mabweni ambazo uendeshaji wake una gharama kubwa.
Hata hivyo, NCAA imekuwa ikitenga mamilioni ya fedha kila mwaka kwa ajili ya kuwapa ukombozi wa fikra watoto wa Ngorongoro. Matunda hayo yameanza kuonekana.
Kuna shule nyingi za msingi na sekondari zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa katika vijiji na kata mbalimbali.
Shule ya Sekondari Nainokanoka ni miongoni mwa shule za kupigiwa mfano katika dhana nzima ya NCAA ya kuwapatia elimu watoto wa jamii ya wafugaji ndani na katika eneo la vijiji vinavyozunguka Mamlaka hiyo.
Sekondari ya Nainokanoka ilianzishwa na serikali mwaka 2012. Ni shule ya bweni inayohudumia wanafunzi wa Ngorongoro na wengine kutoka pande zote za nchi. Jina Nainokanoka ni la Kimasai, lenye kumaanisha ‘ukungu’. Eneo hili lina baridi kali kwa takriban kipindi chote cha mwaka.
Mwalimu wa Taaluma, Leonard Martin, anasema Sekondari ya Nainokanoka ina wanafunzi 1,100; kati yao wasichana ni 466. Ilianza na wanafunzi 300 pekee na vyumba vinne vya madarasa. Ina kidato cha kwanza hadi cha sita. Kidato cha sita ni wavulana pekee. Shule ina walimu 23 waajiriwa.
“Tunashukuru kuwa NCAA ilianza kuweka mkono wake hapa mapema sana shule ilipoanzishwa. Walijenga jengo la utawala, nyumba mbili za walimu (two in one), vyumba vinne vya madarasa na mabweni.
“Kwa sasa vyumba vya madarasa vimeongezeka hadi 23 na hii yote ni kazi ya NCAA – huenda mwakani mahitaji ya vyumba yakaongezeka kutokana na mpango wa serikali wa kutoa elimu bure kwa watoto. Nyumba za wafanyakazi zipo tano na kwa kweli zinatosha kwa sasa,” anasema Mwalimu Martin.
Kwa kutambua mahitaji ya shule hii, NCAA tayari wameanza ujenzi wa bwalo kubwa la chakula kwa mahitaji ya wanafunzi wote. Pamoja nalo, pia kuna mpango wa ujenzi wa maktaba. Kwa sasa chumba cha darasa ndicho kinachotumiwa kwa huduma hiyo.
“Tunao upungufu wa hapa na pale, lakini kwa kweli kwa yote unayoyaona hapa Nainokanoka, asilimia zaidi ya 90 ni kazi ya NCAA. Tunawashukuru sana,” anasema.
Sekondari hii inazo maabara za kisasa pamoja na vifaa. “NCAA wamejenga maabara za Fizikia, Kemia, Baiolojia…naweza kusema kwa wilaya yetu sisi ni wa kwanza kwa kuwa na maabara nzuri na za kisasa.
“Mfumo wa maji upo – ulijengwa mwaka 2013-2014 kutoka mbali na hii shule hadi kwenye matangi yetu. Maji yapo ya uhakika kabisa hadi yanatumiwa na wanavijiji. Umeme tunao wa jenereta na wa jua. Yote hii ni kazi ya NCAA.
“NCAA wanatupatia mafuta ya jenereta lita 400 kila mwezi, matengenezo yanafanywa na wao wenyewe. Wanajenga na kukarabati barabara.
“NCAA walitumia nguvu kubwa sana kujenga mabweni. Awali, wanafunzi walitumia darasa moja kama bweni, lakini wakawa wanaongeza madarasa kulingana na mahitaji, mwaka 2013 kidato cha pili walikuwa 277; waliofauli ni 270.
“Mwaka 2013 umeme ukawa tatizo kubwa. NCAA wakaleta jenereta. Wanafunzi walisoma kuanzia saa 1 hadi saa 4 usiku. Baadaye wakaleta umeme wa jua kwa ajili ya madarasani. Umeme umesaidia sana kwani mwaka 2018 waliofanya mitihani kidato cha nne walikuwa 123 na waliofaulu ni 113. Tukashika nafasi ya 57 kimkoa na 975 kitaifa miongoni mwa shule 3,488 nchini kote. Kidato cha sita mwaka 2019 wanafunzi walikuwa 71. Wote walifauli kwa daraja la kwanza hadi la tatu. Daraja la kwanza walikuwa 8, daraja la pili 34 na daraja la tatu 29. Kwa kidato cha tano tumeongeza HKL, hivyo tuna HKL na CBG. Asilimia zaidi ya 50 ya wanafunzi wote ni wenyeji wa hapa hapa Ngorongoro,” anasema Mwalimu Martin.
Mazingira mazuri ya kusomea na kuishi yamekuwa kivutio kwa wazazi na wanafunzi. Kwa sababu hiyo, uongozi wa Shule ya Sekondari Nainokanoka unasema idadi ya wanaokimbia masomo imepungua mno.
“Dropout imeshuka sana kutokana na hamasa ya mahitaji ya msingi. NCAA kupitia Baraza la Wafugaji Ngorongoro kila muhula linatoa Sh 50,000 kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya mahitaji madogo madogo. Hali hiyo imewafanya wapende kusoma,” anasema Mwalimu Martin.
Pamoja na mafanikio yote hayo, Sekondari ya Nainokanoka bado ina mahitaji. “Hatuna maktaba ya kompyuta pamoja na kompyuta. Kwa sasa tuna kompyuta 20 pekee zinazotumiwa na wanafunzi 1,100. Hazitoshi.
“Hapa tulipo ni porini, tunaomba tupate uzio ili kuwakinga watoto dhidi ya wanyamapori wakali na pia kudhibiti wanafunzi wachache wanaokuwa na mawazo ya kutoroka, lakini pia ukitazama bwalo linalojengwa unaona linahitajika kubwa zaidi ili kumudu idadi ya wanafunzi,” anaomba Mwalimu Martin.
Kwa upande wao wanafunzi, pamoja na kusifu huduma wanazopata kutoka NCAA na serikalini, wanashauri bwalo likamilishwe mapema ili wapate fursa ya kutazama vipindi vya televisheni.
“Tunahitaji kuangalia taarifa ya habari. Utashangaa kusikia kuwa ajali ya Morogoro iliyoua watu zaidi ya 100 tumeijua wiki mbili ikiwa imekwisha kutokea.
“Tulijua baada ya mwanafunzi mwenzetu wa kidato cha nne kutoka huko alipokuja kuripoti hapa shuleni,” anasema mwanafunzi Playgod Mainoya wa kidato cha tano.
Mwanafunzi mwingine anasema: “Hapa tunachokosa ni entertainment, hakuna. Hapa ni kanisani na darasani tu; hali hiyo inatufanya tukose mengi yanayoendelea nchini mwetu. Tunapenda kumsikia Rais wetu (John Magufuli) anasema na anafanya nini.
“Nitakupa mfano, amefariki mzee Mugabe [Robert Mugabe wa Zimbabwe] hatukujua. Tulijua baada ya mwenzetu mmoja kumuuliza mwalimu kwanini bendera ya taifa inapepea nusu mlingoti, ndipo akasema Mugabe amefariki dunia. Tunahitaji bwalo la chakula na humo tuwekewe televisheni tuwe tunatazama na kusikiliza taarifa ya habari,” anasema.
Changamoto nyingine inayosemwa na wanafunzi hao ni idadi ndogo ya vitanda; pia wanaomba umeme jua uwekwe mabwenini na madarasani ili wanafunzi wapate muda mrefu wa kujisomea nyakati za usiku.
Ofisa Maendeleo ya Jamii katika NCAA, Bashiru Nchira, anasema Shule ya Sekondari ya Nainokanoka ni miongoni mwa maeneo ambayo Mamlaka hiyo imekusudia kuyafanya ya mfano kwa upande wa utoaji elimu.
“Tunajua changamoto haziwezi kumalizwa kwa asilimia 100 lakini ni wajibu wetu kuhakikisha tunazikabili ili kuendana na dhana nzima ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha watoto wanapata elimu.
“Changamoto za ukubwa wa bwalo tumezisikia, lakini tunadhani wasubiri kwanza hili tunalojenga likamilike. Likishakuwa tayari hapo naamini uongozi wa shule utawawekea televisheni. Changamoto hizi ni za kawaida, muhimu ni kwa watoto kusoma kwa bidii ili baadaye waje kulitumikia taifa na sisi NCAA tutafanya kila linalowezekana ili mazingira ya upatikanaji elimu yawe bora,” anasema Nchira.