Mapigano yameingia wiki ya pili nchini Sudan, kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa RSF, ambayo yamesababisha watu zaidi ya 400 kupoteza maisha na maelfu kujeruhiwa.
Licha ya pande zote kukubali kuacha mapigano wakati wa sikukuu ya Eid, wakabiliano yameendelea, huku jeshi la Sudan likitangaza kuwa limekubali kusaidia mipango ya kuwaondoa nchini humo raia wa kigeni.
Saudi Arabia imekuwa nchi ya kwanza kufanikiwa kuwaondoa raia wake 50 baada ya kutumia usafiri wa boti ambao wamewasili kwenye mji wa bandari wa Jeddah.
Wachambuzi wa mizozo kutoka Shirika la International Crisis Group, wanaonya kuwa iwapo suluhu ya haraka haitapatikana, huenda ukasambaa na kuwa wa kikanda.
Haya yanajiri wakati huu jeshi la Sudan likisema kuwa wanadiplomasia na raia kutoka katika nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa na China wataondolewa nchini humo kwa ndege wakati huu huku mapigano yakiendelea kati ya wanajeshi wa serikali na vikosi maalum vya RSF.