Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imetangaza kufilisi kampuni za DOVETEL (T) Limited maarufu kama Sasatel na Hydrox Industrial Serivices Limited baada ya kujiridhisha kuwa kampuni hizo mbili kushindwa kujiendesha na kulipa madeni.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kutolea ufafanuzi kuhusu hatua hiyo, iliyofikiwa ya kufilisi kampuni hizo, Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi amesema inalenga kulinda haki za wanahisa, wabia,wadeni, wafanyakazi na pia kuwezesha kodi na tozo za Serikali kulipwa ipasavyo.
“Ningependa umma wa Watanzania ufahamu kuwa RITA mbali ya kusajili vizazi, vifo, ndoa, talaka na watoto wa kuasili pia katika ufilisi tunaangalia usimamizi wa kampuni na ufilisi wa kampuni, watu binafsi usajili wa bodi za wadhamini, kusimamia mali isiyokuwa na mwenyewe, kuandika na kutunza wosia na kusimamia mirathi,” amesisitiza Kanyusi.
Amesema RITA imepewa idhini na Mahakama, kuzibinafsisha kampuni hizo na kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari, kuutangazia umma na hasa wenye maslahi katika kampuni hizo, kujitokeza kabla ya kukamilisha mchakato wa ubinafsishaji.
“Kazi ya ufilisi nchini inaongozwa na sheria kutegemea biashara inayofanywa na kampuni inayofilisiwa. Sheria hizo ni pamoja na ya ufilisi, ya kampuni, ya benki na taasisi za fedha, ya vyama vya ushirika, ya bima, ya mashirika ya umma, ya hati za makubaliano na ya muunganisho wa wadhamini,” amesema.
Kanyusi amesema RITA imejipanga kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kufikia matarajio na malengo ya Serikali kupitia falsafa ya R nne (4Rs) yaani Maridhiano, Mabadiliko, Ustahimilivu na Ujenzi Mpya.
Akifafanua Kanyusi alisema ufilisi wa kampuni hizo ni hatua muhimu kwani endapo kampuni hizo zitaachwa bila kufilisiwa, zinaweza kutoweka huku makundi tajwa yakipoteza haki kisheria.
DEVETEL au Sasatel ilianzishwa kufanya biashara ya mawasiliano huku kampuni ya Hydrox Industrial Services Limited ikijihusisha na kuzalisha na kuuza dawa na kemikali za kusafisha maji.