Profesa Anna Tibaijuka

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kuanzia sasa inachofanya ni vitendo tu katika kukabiliana na wavunjifu wa sheria za ardhi, wakiwamo wavamizi wa maeneo yasiyoruhusiwa kujengwa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema hayo bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF).

Mbunge huyo, pamoja na mambo mengine, alitaka kujua kama Wizara hiyo haioni busara sasa kuwa na polisi maalumu wa kudhibiti vitendo vya uvamizi wa ardhi unaofanywa na baadhi ya wananchi, hasa wenye ukwasi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, akijibu maswali hayo, alisema, “Tumeshakutana na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kukubaliana kwamba sasa imefika wakati wa vitendo. Maana yake matatizo mengi yanayoeleweka kama matatizo ya ardhi kimsingi ni matatizo ya kiutawala -ni sheria ya TOT siyo sheria ya ardhi, sheria inayosimamia trace passes yaani mtu kuingilia mali ambayo siyo ya kwako.

“Kwa hiyo, nichukue nafasi hii katika kujibu swali hilo kusema kwamba tunakubaliana kabisa na ushauri Land Rangers (walinzi wa ardhi) tumeanza Dar es Salaam na tunahimiza halmashauri zote kuwa na kitengo hiki. Hii kada ya watumishi ambayo ilikuwepo, lakini sasa mambo yaliyopita watu wakafikiria siyo muhimu athari zake zimejitokeza. Hilo ni la kwanza.

“La pili, kwamba maafisa wengi wa Serikali siyo tu wa ardhi hata walimu, hata madaktari hata wauguzi wote wako chini ya himaya ya halmashauri za wilaya. Sasa inapokuja kwenye sekta ya ardhi kwa sababu sekta hii ni lazima iendeshwe kisheria na kitalaamu ni kweli kwamba zimetokea nyakati maafisa wenyewe wa ardhi wakati mwingine wameogopa wakaanza kutekeleza mambo kinyume na maadili na matakwa ya kazi yao . Mimi nimekuwa nikiwahimiza kwamba atakayeogopa hata akisema madiwani wameniagiza hili au lile yeye mwenyewe ndiyo atawajibishwa.

“Kwa hiyo, inabidi wawe na ujasiri wafanye kazi yao bila kutishwa na mtu yeyote. Kiongozi yeyote awe kiongozi wa Serikali au sisi wenyewe viongozi kama wabunge awe kiongozi wa namna yeyote ile, kwa kweli hatufanyiwi haki wanapowatishia maafisa ardhi. Na wenyewe imeonekana kwamba wamechukua nafasi hii sasa kufanya vitendo vingine ambavyo wanajua hatimaye watasema mimi niliambiwa na halmashauri nifanye hivyo, mimi niliambiwa na madiwani nifanye hivyo.

“Nasema visingizio hivi tunavikomesha na kikosi cha askari ardhi sasa hivi kitawezeshwa kuwa na askari ndani ya Jeshi la Polisi ambao sasa watakuja kuangalia ‘trace passes’, nitoe tu mfano kama ifuatavyo; watu wengi wanakwenda kwa maafisa ardhi kulalamika kwamba viwanja vyao vimevamiwa, kwani mtu ukienda dukani ukanunua kitanda, ukakuta sasa mtu ameshakalia kitanda chako, unarudi dukani kupiga kelele? Si unaita polisi?

“Kwa hiyo naomba tuelewe sheria inavyokwenda kwamba uvamizi ni suala la polisi, kama wewe una hati halali, unakuta mwenzako hana karatasi yoyote anaanza kujenga, unakwenda kutafuta polisi, usimtafute ofisa ardhi; na maafisa ardhi wengine wamejifanya na wenyewe mahakimu, hatuna madaraka sisi ya kuamua vitu ambavyo siyo vya kwetu.”