Na Angalieni Mpendu
Salaam aleikum! Na wasio Waislamu Tanzania nzima. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) leo linatimiza miaka 51 tangu liundwe tarehe 17 Desemba, 1968 jijini Dar es Salaam baada ya kuvunjwa kwa Jumuiya ya Waislamu wa Afrika ya Mashariki (East African Muslim Welfare Society) mwaka huo.
BAKWATA ni Baraza la Waislamu nchini, malengo na madhumuni yake ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za imani ya dini ya Kiislamu. Ni Baraza linalowaunganisha Waislamu wote na wasio Waislamu kuishi pamoja kwa usalama na amani hapa nchini.
Leo ni siku ya BAKWATA. Ninatoa kongole kwa viongozi wa BAKWATA kwa kuliongoza baraza hili katika hali ya hekima na busara hadi kufikia miaka 51. Aidha, ninatoa hongera kwa baraza kudumu nusu karne na kuwahudumia Waislamu wa Tanzania kwa upendo, usalama na amani.
Katika kuadhimisha miaka 51, Waislamu hatuna budi kupongeza na kulisifu baraza kwa kazi zilizofanywa, zikiwemo za kutoa elimu ya dini, kutanzua migogoro dhidi ya imani na dini yenyewe, kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu na kushirikiana kwa upendo na dini nyingine.
Ama ni wajibu kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla wao kuwarehemu viongozi wote walioanzisha na walioendesha BAKWATA hadi sasa, ambao hatunao, wametangulia mbele ya haki. Amin! Na tutoe baraka zetu kwa viongozi waliopo sasa, Mwenyezi Mungu azidi kuwabariki na kuwaangazia hekima na nuru katika uongozi wao. Amin!
Wakati tunaadhimisha mwaka wa 51, ni vema tukaitazama BAKWATA katika majira matatu. Ilikotoka na harakati zake za kuanzishwa. Kuanzishwa kwake hakukuwa kwa heri, kwani baadhi ya waanzilishi walifikwa na mitikisiko. Lakini chombo kiliundwa na baharini kilitiwa. Safari ilianza.
Katika kufanya kazi na kuifikisha BAKWATA ilipo leo, imekutana na mitihani kadha wa kadha katika kuimarisha Uislamu. Inamudu na kupita. Hakuna safari isiyo na mazongezonge. Inafanya vema katika kutoa daawa na mafunzo ya dini. Hongera BAKWATA. Heri na shari zote zinatokana na Mwenyezi Mungu.
Tangu kuanzishwa na kuendeshwa, BAKWATA imesimamia kikamilifu imani ya Uislamu na kuhakikisha sheria na haki za Waislamu zinapatikana. Imejenga ushirikiano na serikali pamoja na vyombo au taasisi za dini nyingine ndani na nje.
Mambo yote mema na yale yote si mazuri ambayo yamepata kufanywa na BAKWATA, tuseme alhamdullilah. Yote hayo yamepita na tuanze mambo mapya. Madhumuni ni kujenga si kuharibu na kubomoa.
Wakati tunaadhimisha mwaka wa 51 wa BAKWATA, tutazame kaulimbiu isemayo: BAKWATA MPYA. Kuwa mpya ina maanna ya kufanya mabadiliko ya hali na mali, kwa nia ya kuwapatia Waislamu wote maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Dhamira ya uongozi wa BAKWATA ni kufanya mabadiliko, kujitambua na kuacha mazoea. Waislamu hawana budi kubadilika, kujitambua na kuacha mazoea. Mabadiliko haya yanahitaji ukweli wa viongozi na Waislamu wenyewe.
Mkazo mkubwa katika kutoa elimu dunia na elimu ahera. Sheria zinafuatwa na haki zinapatikana, zinalindwa na zinaheshimika. Maendeleo ya kweli yanahitaji haki si dhuluma.
BAKWATA mpya ifanye mabadiliko ya kweli ndani, kuweka viongozi wenye elimu ya juu, wenye utambuzi na uchambuzi wa dini na wenye uthubutu katika kukabili hitilafu au uonevu pindi utokeapo ndani na dhidi ya Uislamu.
Ninawatakia heri na baraka Waislamu wote katika kuadhimisha mwaka wa 51 wa BAKWATA. Tukubali BAKWATA MPYA ilete mambo mapya kwa manufaa ya Waislamu. Uadilifu wa viongozi wa BAKWATA ndiyo mafanikio ya Waislamu wote Tanzania.
……………….MWISHO……….