Hatimaye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amewasilisha  kiwango na ukomo wa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017. Waziri ameliambia Bunge kuwa  mwaka ujao wa fedha zitatumika Sh trilion 29.53. Kati ya fedha hizo, mapato ya ndani ni Sh trilioni 17.79 zitakazopatikana kutokana na kodi ya Sh trilioni 15.1 itakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); wakati mapato yasiyo ya kodi yakiwa Sh trilioni 2.69.

Sh trilioni 17.72 zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati Sh trilioni 11.82 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Hii ni sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima.

Katika bajeti iliyopita, shughuli za maendeleo zilipangiwa Sh trilioni 5.76; sawa na asilimia 25.9.

“Asilimia 40 kwenda kwenye mipango ya maendeleo, hili ni jambo jema,” alisema Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alipozungumza na waandishi.

Bajeti hii ni kubwa kuliko zote katika historia ya nchi yetu. Na matumizi nayo yataongezeka. Wananchi kwa hiyo wawe tayari kulipa kodi zaidi ili kukidhi mahitaji ya Serikali. Bila shaka wale matajiri na madalali wao waliokuwa wanakwepa kodi (au wanaosamehewa kodi) huenda wakakamuliwa ili walipe. Lakini na wananchi wa kawaida nao wawe tayari kulipa kodi zaidi kupitia njia mbalimbali kama vile vinywaji, sigara, sukari, usafiri na kadhalika.

Kwani tunaelezwa kuwa, ili Serikali iweze kufikia kiwango cha bajeti hii, itapaswa ifanye jitihada kubwa ya “kubuni vyanzo vipya vya mapato”. Kwa kiasi kikubwa mzigo huu utabebwa na wananchi, kwa vile bidhaa zitaongezewa kodi na ushuru ili kuziba nakisi ya wastani wa Sh trilioni 2.  Hii ni pamoja na TRA kwa sasa kukusanya wastani wa Sh trilioni 1.1 kwa mwezi, yaani Sh trilioni 13 kwa mwaka.

Kiwango hicho cha makusanyo cha mwaka mmoja, hakiwezi kufikisha Sh trilioni 29.53 zinazopangwa na Waziri Mpango kutumika katika kipindi chote cha mwaka mzima. Ndipo zitahitajika “jitihada za ziada” katika ukusanyaji mapato.

Katika bajeti hii, Serikali inatarajia kupata Sh trilioni 3.6, ikiwa ni misaada ya “wahisani” kupitia bajeti kuu pamoja na ufadhili wa miradi moja kwa moja.

Hivyo, hii ni bajeti ambayo itategemea misaada ya kigeni kama ilivyokuwa siku zote, ingawa mwaka huu Dk. Mpango amesema kuna uwezekano wahisani wakapunguza misaada yao ikafikia Sh trilioni 2.1; yaani tutalazimika kujitegemea badala ya kuwa ombaomba.

Sababu ya kupunguza misaada yao ni kuwa hao wanaojiita wafadhili hutoa kwa masharti. Pale ambako wanaona utawala bora au demokrasia imevurugwa, basi hupunguza au huzuia misaada yao. Na ndivyo walivyofanya mara hii baada ya kuona kuwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yamefutwa na kura kurejelewa “bila ya sababu za kimsingi”.

Marekani imetangaza kuifutia Tanzania misaada ya Shirika la Changamoto za Milennia (MCC). Hivyo nchi yetu imekosa Sh trilioni 1.03 ilizokuwa ipewe. Umoja wa Ulaya (EU) nayo ipo katika hatihati ya kutoa Sh trilioni 1.56.

Tayari baadhi ya wabunge wa Uingereza nao wanaishauri serikali yao kuifutia Tanzania msaada wa Sh bilioni 622.

Zaidi ya hayo, Wizara ya Fedha imeshatangaza kuwa wahisani 10 kati ya 14 wanaosaidia bajeti kuu ya serikali wanatarajia kujitoa.

Kwa serikali tegemezi kama yetu ambayo siku zote imekuwa ikifurahia misaada ya kigeni, hili si jambo la kufurahisha. Tutakumbuka wakati Waziri wa Fedha anapowasilisha bajeti yake, huwa anasoma orodha ya wafadhili kwa kuwashukuru, huku wabunge wakishangilia kwa furaha. Inaonekana mwaka huu hawatapata fursa hiyo ya kugonga meza.

Kuzuiwa kwa misaada hakujatokana na huu mgogoro wa Zanzibar tu, bali hata kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/2015 wahisani walitarajiwa kuchangia Sh trilioni 1.09, lakini wengi walikataa kutoa fedha kutokana na ile kashfa ya Tegeta Escrow ambayo vigogo walijichotea mabilioni bila ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Matokeo yake kuanzia Julai 2015 hadi Februari 2016 misaada ya kigeni iliyopatikana ilikuwa asilimia 62 tu ya matarajio ya bajeti. 

Sasa iwapo tutakosa ufadhili, basi kuna uwezekano wa kuongezeka kwa ukopaji ili kuziba pengo. Dk. Mpango anasema Serikali inatarajia kukopa mikopo ya kibiashara takriban Sh trilioni 2.1 kutoka vyanzo vya nje na Sh trilioni 5.37 kutoka vyanzo vya ndani.

Na hii mikopo ya ndani imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 2014/2015 Serikali ilikopa dola takriban bilioni 2 za Marekani. Hii ni asilimia 35 zaidi ya kiwango kilichowekwa katika bajeti.

Na mara hii labda mikopo ya ndani itaongezeka kutokana na kukosa misaada ya nje. Ikumbukwee kuwa sehemu kubwa ya mikopo hii ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, yaani kulipa mishahara na posho.

Na kama tunavyoelewa, mikopo ya kibiashara ina masharti yake-ikiwamo kima cha riba, muda wa kulipa na dhamana. Mara nyingi tunapochelewa kulipa madeni, basi tunachukua mikopo mipya ili kulipa madeni ya zamani. Tumekuwa tukichukua mikopo ili kulipa riba peke yake. Matokeo yake nchi yetu inaingia katika madeni makubwa.

Ndipo leo deni letu la kitaifa limefikia dola karibu bilioni 20 za Marekani. Wakati wa Mwalimu Nyerere tulikuwa na deni la dola bilioni 3. Leo zimefika karibu bilioni 20, licha ya madeni tuliyofutiwa chini ya mpango wa kile kinachoitwa “kufufua” uchumi.

Na wakati huo huo ukusanyaji wa kodi utabidi uendelee, pamoja na ukwepaji (au ukwapuaji) wa hali ya juu uliozoeleka. Mfano mmoja ni ukwepaji unaofanywa na kampuni za simu. Waziri Mpango aliliambia Bunge kuwa Serikali inalielewa jambo hili. Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, naye amesema hatua zinachukuliwa kuziba mianya. Tunasubiri kuona iwapo hizo hatua zitazaa matunda.

Tunaambiwa kampuni za simu zimekuwa zikikusanya zaidi ya Sh trilioni 5.5. Kati ya hizi ni Sh bilioni 35 tu zimelipiwa kodi. Yaani zaidi ya Sh trilioni 5.4 hazilipiwi kodi! Huu si ukwepaji wa kiwango cha juu mno.

Hapa tunazungumzia sekta moja tu ya mawasiliano. Hatujui sekta nyingine zinakwepua kiasi gani. Kwa mfano, kuna sekta ya usafirishaji wa anga, nchi kavu na majini. Kuna biashara ya mafuta, kuna halaiki ya mabenki, kuna majengo yanayochepuka kama uyoga kila mahali. Kuna hoteli za kitalii. Wote hawa wanakusanya matrilioni. Serikali inaambulia ngapi kati ya hizo?

Hata Mkaguzi na Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) anatuambia kuwa mwaka jana Serikali ilishindwa kukusanya kodi ya Sh trilioni 6.9. Hii inatokana na walipa kodi wakubwa kupinga makisio ya kodi zao mahakamani na katika Bodi ya Rufaa za Kodi. Kiwango hiki kinaongezeka kila mwaka.

Yaani mwaka 2013/2014 walikataa kulipa Sh trilioni 1.7 na mwaka 2014/2015 zikafikia hizo Sh trilioni 6.9. Mwaka huu hatujui, labda tusubiri ripoti ijayo ya CAG.

Ndio maana nikasema mwananchi wa kawaida awe tayari kufidia kodi hizi zinazokwepuliwa na wawekezaji wa ndani na wa nje.