Wiki mbili zilizopita katika safu hii niliandika makala nikieleza hisia zangu kuhusu hatua ya Kenya kutupiku kwenye fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini.
Siku chache baadaye, Rais John Magufuli, akawa na ziara katika mataifa matatu – Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe. Kama yapo mambo yaliyowafurahisha Watanzania wengi kwa ziara hiyo, lile la ‘kukieneza’ Kiswahili katika mataifa hayo linaweza kuwa lilitia fora. Mwitikio wa Watanzania kwenye mitandao ya kijamii ulithibitisha furaha iliyotokana na uhalali wa kazi iliyofanywa na Rais Magufuli.
Tumeona akiwakabidhi vitabu mbalimbali wenyeji wake katika mataifa hayo – Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe. Tumesikia namna wakuu hao walivyovutika na kutangaza utayari wa kuhakikisha Kiswahili kinafundishwa na kuzungumzwa katika mataifa hayo. Kwa hili hatuna budi kumpongeza Rais Magufuli na wote waliomshauri. Haya ndiyo mambo yenye tija kwa nchi.
Tunao maelfu ya Watanzania wenye sifa za kufanya kazi ya kufundisha Kiswahili katika mataifa hayo na mengine duniani kote. Kwa hatua iliyofikiwa hatutarajii kuona Watanzania wakisubiri kushikwa mikono kwenda kupata ajira.
Wala hakuna sababu ya kusubiri ‘mwongozo’ wa serikali kuhusu fursa hii. Muhimu ni kwa kila mwenye sifa kujitokeza na kuanza kufaidi fursa hii. Jambo muhimu ni kuhakikisha wale wanaokwenda kufanya kazi katika mataifa hayo wanafuata sheria na taratibu za ajira katika mataifa hayo. Wajuzi wa Kiswahili waende huko wakachume fedha, wazilete ili ziboreshe uchumi wao na wa taifa letu.
Kama nilivyosema katika makala hiyo, itakuwa fedheha kuona mambo mazuri kama haya yakitekwa na Wakenya ambao wakati sisi tukipambana na mabeberu ili kuwakomboa makabwela wenzetu wao walikuwa upande wa udhalimu. Huu ni wakati wa kufaidi matunda ya ukombozi tuliousimamia.
Bado natoa mwito kwetu sote kuhakikisha tunajadili na kutenda mambo yenye tija kwa nchi na wananchi. Tujadili mbinu na fursa zenye kulenga kutukwamua kutoka kwenye lindi la ulofa.
Tumeona kampeni ya uondoaji mifuko ya ‘rambo’ ilivyofanikiwa. Baada ya kauli ya serikali iliyotolewa na waziri mwenye dhamana ya mazingira na baadaye kukaziwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, tumeona mwitikio wa Watanzania wote kwa jambo hili lenye faida kubwa kwa mazingira na afya za wanadamu na viumbe hai wengine.
Porojo zilitawala kwa miaka mingi sana katika suala la kutokomeza mifuko hiyo. Mara zote biashara hii haikukoma si kwa bahati mbaya, bali kwa njama za wafanyabiashara na viongozi kwa kisingizio cha kulinda ajira. Ajira inayozalisha maafa si ajira.
Tulihoji mara zote iweje Kenya, Rwanda wafanikiwe, lakini sisi tushindwe? Ilikuwaje Zanzibar – sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – waweze, lakini upande wa Bara tufeli? Kulikuwa na namna.
Baada ya kufanikiwa kwenye ‘rambo’, nashauri tugeukie chainsaw. Mashine hizi zinazotumiwa kukata miti ni janga jingine kubwa mno kwenye mazingira yetu.
Mara kadhaa nimependekeza kwenye mamlaka husika kuwa umiliki wa chainsaw uwe wa mfumo kama wa umiliki wa silaha! Chainsaw ni janga kwa taifa letu. Hatari yake imekuwa kubwa kwa sababu upatikanaji ni mwepesi. Yeyote anayetaka kununua chainsaw anainunua kama anavyonunua panga mtaani.
Wapo wamiliki ambao kazi yao ni kuzikodisha kwa wenye mahitaji. Wapo wenye chainsaw walioajiri vijana ambao muda wote wako tayari kukodiwa. Tunaweza kusema uwepo wa mashine hizi ni matokeo ya maendeleo, na kwamba hatuwezi kurejea kwenye ujima. Sawa, hatuwezi kuendelea na misumemo ya kizamani, lakini kama ilivyo kwamba baada ya ujio wa bunduki haukuhalalisha bunduki zimilikiwe kama njugu; tuna kila sababu ya kuhakikisha chainsaw zinawekewa mwongozo wa umiliki. Kwa mfano, anayetaka kuwa nayo aeleze kama ana msitu.
Umiliki pekee si hoja, bali tuanze na wale wanaopata vibali vya kuziingiza nchini mashine hizo. Uwepo utaratibu wa waagizaji kuwa na vibali na wale wanaonunua kwao wajulikane, na kwa kweli waonyeshe wapi wanakozipeleka.
Chainsaw ikiingia msituni, hasa msitu wa hifadhi, madhara yake ni makubwa mno katika kipindi kifupi. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, akiwa DC wa Wilaya ya Butiama alidhibiti janga hili. Butiama yote ikawa ya kijani. Huyu anaweza kutumiwa kuchota mbinu alizotumia kudhibiti uhalifu huu.
Niombe tu kuwa baada ya kufanikiwa kwenye ‘rambo’, sasa iwe zamu ya vitu vingine vyenye kuharibu mazingira na afya zetu. Kwenye orodha hiyo, chainsaw iwe ya pili. Misitu inamalizwa. Inaonekana haina mwenyewe. Matunda pori yanatoweka. Waziri Mkuu hili analimudu. Aligeukie sasa.