Vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji msukumo, mbinu na sheria mpya. Hii si vita ya Polisi, Usalama wa Taifa wala Serikali pekee. Wala vita hii hatuwezi kuishinda kwa kubaki tukioneana haya au tukiogopana.

Kwa wiki kadhaa, vyombo vya habari, tukiwamo sisi JAMHURI, tumeamua kwa dhati kabisa kuishiriki vita hii. Tumefanya hivyo kwa kutambua madhara makubwa yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana wetu.

Kama tutalegeza kamba, kama tutaogopa au kuoneana haya, muda si mrefu Tanzania itakuwa Taifa la mazezeta na watu wasioweza kushiriki kuukuza uchumi wetu.

 

Athari za dawa za kulevya ni kubwa mno, tofauti kabisa na baadhi yetu tunavyofikiri. Tunatoa wito kwa wazazi, vijana na watu wote wenye mapenzi mema kuzuru vituo vya afya na hospitali kujionea matokeo hasi ya matumizi ya dawa hizi.

 

Kuna dalili za wazi kwamba vita dhidi ya washiriki wa biashara hii haramu inakwazwa na mambo mengi. Miongoni mwao ni rushwa miongoni mwa watendaji katika vyombo vya usimamizi na utoaji haki; na jingine ni ubutu wa sheria.

 

Inasikitisha kuona mtu anayeuza au kusambaza sumu hii hatari kwa vijana wa Taifa letu, akipewa adhabu ya faini. Tumeona namna walivyo na ukwasi, kiasi kwamba faini kwao si lolote, si chochote.

 

Kukwama kwa kesi nyingi mahakamani kunatufanya tuishauri mamlaka inayohusika ione busara ya kufanya mambo makuu mawili. Mosi, kuanzisha Mahakama maalum itakayoshughulikia wasafirishaji na wauza dawa za kulevya; kuzipa makali sheria za sasa; na tatu ni kuwa na majaji waadilifu watakaosikiliza kesi hizo.

 

Tena basi, tunashauri Mahakama hiyo iwe pia na uwezo wa kushughulikia kesi za majangili ambao muda si mrefu watamaliza kabisa wanyamapori, hasa ndovu katika mapori yetu.

 

Tunapendekeza Mahakama hiyo kwa sababu kwa hali ilivyo sasa, ni vigumu sana kuendesha kesi zinazohusu dawa za kulevya na ujangili. Wanaoshiriki mambo haya haramu wanapaswa kufika mahali wakatambua kuwa Serikali ina nguvu za kuwadhibiti. Jeuri yao ya fedha, rushwa na hata mauaji wanayofanya hayawezi kuwa mambo ya kuwatisha wazalendo kulinda maadili na rasilimali za Taifa letu.

 

Tunarejea kuwaomba wananchi wote wenye mapenzi mema kujitokeza kushiriki vita hii halali. Wasafirishaji na wauza dawa za kulevya tunaishi nao. Tunawajua. Tuwataje, wajulikane na tufanye kila linalowezekana ili wasiendelee kukiteketeza kizazi hiki.

 

Tunawapongeza wale wote waliojitokeza kwa hali na mali kuvipatia ushirikiano vyombo vya dola na vyombo vya habari katika kuwaumbua wote wanaoshiriki uharamia huu.

 

Sifa ya Taifa letu imechafuliwa mno kwa biashara hizi za dawa za kulevya na pembe za ndovu. Tukidhamiria, tutaishinda. Tushirikiane kuijenga Tanzania ya leo na ya kesho. Inawezekana, timiza wajibu wako.