Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Saratani ya mlango wa kizazi bado imeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya wanawake nchini ambapo kila mwaka, zaidi ya wanawake 100,000 huambukizwa, huku zaidi ya 6,000 wakipoteza maisha.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kuwa takriban asilimia 36 ya vifo vinavyotokana na saratani nchini husababishwa na aina hiyo ya saratani.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Lodalis Gadao wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wiki ya chanjo kitaifa.
Amesema Saratani hiyo huanzia kwenye mlango wa kizazi – sehemu inayounganisha mfuko wa uzazi na uke kutokana na seli kukua kwa kasi isiyo ya kawaida.
Gadao ameeleza kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo na mwitikio hafifu wa wanawake kujitokeza kwa uchunguzi na kupata chanjo ya HPV.
” Zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho, hali inayopunguza mafanikio ya matibabu”amesema.

Aidha, ametaja wanawake wanaoishi na VVU na watoto wa kike wanaoanza ngono katika umri mdogo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huo. Uchunguzi umebainisha kuwa kati ya wasichana wanne wanaojihusisha na mapenzi mapema, watatu huambukizwa.
Mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo inahusisha utoaji wa chanjo kwa watoto wa kike kuanzia miaka 9 na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kuwa na wapenzi wengi.

Dk. Tumaini Haonga, Afisa wa Programu ya Elimu kwa Umma, amesema baadhi ya walengwa wanashindwa kupata chanjo kutokana na changamoto kama kuhama hama kwa wakulima na wafugaji, au wazazi wa mijini kukosa muda wa kuwapeleka watoto wao.
Wizara imehimiza jamii kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya afya ya uzazi, na kuwasisitiza wanawake kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara ili kugundua ugonjwa huo mapema na kupata tiba stahiki.


