Wiki iliyopita hapa nchini umekuwapo mjadala wa kiuchumi, unaohoji mpango wa kuharakisha matumizi ya sarafu moja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mjadala huu umehusisha wadau mbalimbali, akiwamo Balozi wa Tanzania nchini Ubeligji, Dk. Diodorus Kamala.
Kwanza nimpongeze Dk. Kamala maana wiki hii amehitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) nyingine katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, baada ile ya awali aliyoipata kutoka Commonwealth University kuzua maneno na kutiliwa shaka na baadhi ya wanahaharakati. Hongera Dk. Kamala.
Katika PhD hii ya pili, Dk. Kamala sasa ametafiti madhara na faida za ushuru wa pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sitatumia fursa hii kuelezea nini alichokibaini, lakini kwa kuwa wakati anahitimu ameliasa taifa la Tanzania kutokimbilia suala la sarafu moja, hivyo nami napenda kujikita katika eneo hili. Nikijaribu kudurusu mwenendo wa ushuru na soko la pamoja la Afrika Mashariki, binafsi napata wasiwasi. Kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamefikia hatua hii ya ushuru wa pamoja.
Usiniulize kama Tanzania imo kwa kiwango hicho, ila ninachofahamu ushuru wa pamoja kwa SADC (SACU), nchi hizi zimepiga hatua kubwa. Afrika Kusini inazifidia nchi kama Lesotho, Botswana na nyingine pale zinapopata hasara itokanayo na ushuru wa bidhaa mbalimbali kukusanywa katika bandari ya Jumuiya (port of entry to the community).
Hii inamaanisha nini? Kwa mfano, tulivyo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki chini ya Mkataba wa Ushuru wa Pamoja kwa mizigo inayoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam na Mombasa, yote inapaswa kutozwa ushuru na kuondoa utaratibu wa transit.
Chini ya utaratibu wa transit, mizigo inayokwenda kwa nchi kama Rwanda, Burundi na Uganda, hutolewa bandarini bila kulipiwa ushuru na kulipiwa ushuru inapoingia katika nchi husika. Madhara ya utaratibu huu ni makubwa. Kwa mfano, mafuta kama petrol na dizeli, mara kadhaa mafuta ya kwenda Rwanda, Burundi na Uganda yanauzwa katika soko la Tanzania bila kulipiwa ushuru.
Wafanyabiashara wajanja wanaidanganya au wanashirikiana na serikali kudai kwamba mafuta yanapelekwa nchi za nje, hivyo yanatolewa bandarini bila kulipiwa ushuru, kisha yanaishia kwenye utitiri wa vituo vya mafuta vilivyopanga msururu kati ya Kibaha na Chalinze.
Kwa kufanya hivyo, wafanyabiashara hawa wanapata faida kubwa huku taifa letu likipoteza mapato ambayo fedha zingekusanywa zingesaidia ujenzi wa barabara, hospitali, shule, mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa vyuo, afya na mambo mengine mengi ambayo yanakwama hapa nchini kutokana na ukosefu wa fedha.
Ushuru wa pamoja ukitekelezwa kwa ufasaha, kunakuwapo utaratibu wa kukusanya kodi kwa bidhaa zote, kwa mfano, zinazokwenda Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam kisha fedha zilizokusanywa zinapunguzwa gharama ya usimamizi tu na kukabidhiwa kwa Rwanda. Je, hiyo tunaiweza sisi?
Sitanii, suala la sarafu moja halipaswi kuwa la kisiasa. Linagusa uchumi mpana na wa mtu mmoja mmoja. Kwa nchi zetu hizi za Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na Tanzania kufikia hatua hii si la kukurupukia. Tunahitaji si chini ya miaka 15 kuanzia leo kufikia hatua hii. Nchi hizi zinapaswa kukaa pamoja zikaweka vyombo vya kusimamia suala sarafu moja. Hatuwezi kuanzisha sarafu moja kabla ya kuwa na Benki Kuu ya Afrika Mashariki inayofanya kazi kwa miaka mitano hadi 10 tukajiridisha kuwa inaweza kuendesha uchumi wa nchi tano.
Hatuwezi kuanzisha sarafu moja kabla ya kuwa na sera zinazofanana katika masuala kama ya deni la taifa, maduka ya fedha (bureau de change), jinsi ya kukokotoa mfumko wa bei, kiwango cha juu cha mfumuko wa bei, urali wa malipo, fidia kwa uchumi utakaopoteza, gharama za uchapishaji wa fedha na viwango, mpango shirikishi wa maendeleo kwenye jumuiya, vipaumbele vya uwekezaji, gharama za uendeshaji wa serikali, sheria ya ununuzi, miundombinu na mambo mengine mengi.
Sitanii, namaanisha nini hapa? Leo Kenya wanakusanya kodi wastani wa asilimia 24 ya pato la taifa. Tanzania tunajidai tumeongeza kiwango kutoka asilimia 16 katika mwaka huu wa fedha tunalenga kukusanya asilimia 18 ya pato la taifa. Uganda, Rwanda na Burundi usiniulize. Sarafu ya Kenya na Rwanda ina nguvu mara 20 ya madafu yetu. Kenya walikuwa na mfumuko wa bei asilimai 29 miezi mitatu iliyopita, lakini leo ninavyoandika makala haya mfumko wa bei kwa Kenya ni asilimia 4.2, hapa kwetu tunakisia asilimia 15.7.
Tena kuna tetesi kuwa viwango vya mfumko wa bei vya hapa nchini havihusishi chakula, ambacho kwa nchi nyingi ikiwamo ya kwetu huchangia asilimia 48 ya mfumuko. Suala la deni la taifa si la kufanyia mchezo. Taarifa nilizonazo Kenya mwaka huu wamefikia asilimia 39 ya pato la taifa kama deni la taifa.
Tanzania iliingia chini ya Mpango wa Kusamehe Madeni nchi zinazodaiwa mno (HIPC) baada ya uwiano wa deni na pato la taifa (External Debt Ratios (NPV/XGS) kuwa asilimia 250 mwaka 2002.
Sitanii, takwimu za mwaka 2012 zinaonesha uwiano wetu wa deni la taifa ni kati ya asilimia 84. Kikomo kinachokubalika kwa nchi kuendelea kukopa bila tatizo ni asilimia 40 ya pato la taifa. Hata Kenya kwa kuwa na asilimia 39, wachumi wake tayari wanapambana kuona jinsi gani wanaweza kuirejesha katika asilimia 20 hadi 25. Kwa maana nyingine sisi hatuna uwezo wa kulipa madeni yetu kama taifa. Ndiyo maana tukaangukia katika kundi la HIPC. Kwa nchi za Ulaya, tumeshuhudia Ufaransa na Ujerumani zinavyotoa mabilioni kuziwezesha nchi kama Ugiriki na Hispania ambazo uchumi wake unayumba.
Uchumi unayumba kwa sababu nchi nyingi ikiwamo ya kwetu zimezoea kupata fedha za dezo. Mara nyingi nchi hizi zinachapa hati fungani (Treasury Bond) na kuziuza. Kwa mfano, deni la ndani la Tanzania hadi sasa asilimia 47 ya deni linatokana na hati fungani ambazo zinaiva katika muda wa mwezi mmoja hadi miaka 25.
Hati fungani hizi ni mikopo ya fedha inazochukua serikali kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali kwa njia ya kuuza makaratasi yaliyobatizwa thamani. Mbaya zaidi nchi nyingi duniani zinapopata shida ya ukwasi hufanya dhambi ya kuchapisha noti na kulipa mishahara.
Swali langu linakuja, je, nchi zetu hizi za Afrika Mashariki zimejiandaaje kuhakikisha hakuna nchi mwanachama atakayechapa fedha na kuziingiza kwenye mzunguko bila kuzifanyia kazi? Kenya katika chuo chao cha Kenya Monetary School of Studies Nairobi wana mitambo ya kuchapisha fedha. Shilingi ya Kenya inachapishiwa palepale Kenya. Uganda, Rwanda na Burundi sijui, ila hapa kwetu tunachapa fedha zetu mara Uingereza, Ujerumani na kuna wakati zilikuwapo tetesi kuwa tulitaka kuchapisha fedha zetu Ufaransa.
Ninachosema hapa, si nia yangu kuwakatisha tamaa watawala wetu kwenye huu mpango wao wa sarafu moja. Tunazo tofauti nyingi kuliko maelezo. Hapa sijataja hata robo ya matatizo tuliyonayo. Ushauri wangu ni kwamba tuunde chombo cha wataalamu, wafanye uchunguzi, waweke vigezo, tuanze kutekeleza vigezo hivyo ikiwamo hiki cha kufidia uchumi unaopata hasara, tuone kama Kenya au Rwanda watakuwa tayari kuifidia Tanzania au Uganda sawa na wafanyavyo Wajerumani na Wafaransa Ugiriki uchumi wao unapoyumba.
Sitanii, tukishatekeleza vigezo hivyo tukahakikisha tuna viwango vya mfumko wa bei vinavyolingana, uwezo unaokaribiana wa kulipa madeni ya nje na ya ndani, na mengine mengi, tufikirie sarafu moja. Tamaa ya viogozi wetu; Yoweri Kaguta Museveni (Uganda), Mwai Kibaki (Kenya), Jakaya Kikwete (Tanzania), Pierre Nkurunziza (Burundi) na Paul Kagame (Rwanda) kutaka tuwe na shirikisho la kisiasa ifikapo mwaka 2014 itatutokea puani.
Mpango ulikuwa tupate sarafu moja ifikapo 2012, leo tunainusa Krismasi na Mwaka Mpya bila dalili. Tukilazimisha, tutajenga shirikisho la majukwaani kisha yale ya mwaka 1977 tutayashuhudia kwa macho yetu. Mungu ibariki Afrika Mashariki.