Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea.

TATIZO la udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi katika Mkoa wa Ruvuma linatarajiwa kupungua baada ya Kampuni ya Sanku – Project Healthy Children Tanzania Limited inayojishughulisha na teknolojia ya urutubishaji kuanza kufunga mashine za kukoboa nafaka zinazochanganywa na virutubishi kwenye chakula.

Mkurugenzi wa Sanku upande wa Mashirikiano na Serikali Gwao Omari Gwao alisema, Sanku iliingia nchini Tanzania mwaka 2015 kwa ajili ya kuisaidia Serikali katika kupambana na tatizo la udumavu na ukosefu wa madini na vitamini na kwa sasa inafanya shughuli zake katika Mikoa 26,Halmashauri 157 na wafanyabiashara zaidi ya 1,000.

Sanku imefungua ofisi zake nchini Kenya na Ethiopia, ikiwa na jukumu kubwa la kutoa teknolojia kwa wazalishaji ili kuongeza virutubishi muhimu kama madini ya chuma, asidi ya foliki, madini ya zinki, na vitamins. Lengo kuu ni kupambana na changamoto za lishe duni na kusaidia Serikali katika jitihada za kuboresha afya ya wananchi.

“katika Mkoa wa Ruvuma tuna wazalishaji 36 wanaofanya urutubishaji kwa kutumia teknolojia yetu lakini mafanikio haya tunayoyaona hapa nchini ni kutokana na mashirikiano mazuri ya Serikali na kampuni yetu, Sanku inatoa teknolojia na Serikali inatoa elimu na kutengeneza sera ambazo ni rafiki kwa ajili ya mashirikiano haya”alisema Gwao.

Gwao alisema,suala la urutubishaji ni njia mojawapo ya kutatua tatizo la lishe hasa upungufu wa damu,kuzaliwa watoto wenye mgongo wazi na watoto wenye udumavu na magonjwa mengine yanayosababishwa na ukosefu wa lishe bora.

Aidha, alieleza kuwa lengo la Sanku ni kufikia kila kijiji nchini kwa kueneza teknolojia hiyo. Tangu kuanza kwa juhudi hizi, mafanikio yamekuwa makubwa, kutoka mashine 25 mwaka 2015 hadi 1,000 hivi sasa.

Ametoa ushauri kwa jamii, hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kama shule, kuanza kutumia vyakula vyenye virutubishi ili kuboresha hali ya lishe kwa Watoto na jamii nzima.

Alisisitiza kuwa vyakula hivyo vina manufaa makubwa, ikiwa ni pamoja na kusaidia wajawazito kuzuia kuzaliwa kwa watoto wenye mgongo wazi na kusaidia wanaume kuimarisha misuli na kinga ya mwili.

Kwa upande wake Msimamizi wa Maendeleo ya Biashara wa Sanku, Christian Lutaja alisema, mpaka sasa wamefunga mashine zaidi ya 36 Mkoani Ruvuma na mwitikio wa wazalishaji ni mkubwa na mashine hizo zimeongeza utendaji kazi kwa wazalishaji.

Mmoja wa wazalishaji waliofungiwa mashine Gaddaf Mgomi alisema,kabla ya kupata mashine hizo changamoto kubwa ilikuwa idadi ndogo ya wateja, lakini baada ya kupata mashine zenye uwezo wa kuchanganya nafaka na virutubishi wateja wameongezeka kutoka 25 wa awali hadi 100 kwa siku.

Alisema,wanajivunia kupata mashine za virutubishi kwani zimesaidia kuongeza idadi ya wateja hasa kwa shule zinazotoa chakula kwa wanafunzi ambazo zinatambua umuhimu wa virutubishi kwenye chakula.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Sanku upande wa mahusiano na Serikali Gwao Omari Gwao akiwaonesha Waandishi wa Habari Moja kati ya mashine za virutibishi kwenye chakula iliyofungwa kwa Mmoja wa wazalishaji katika Mtaa wa Ruhuwiko Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma jana

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt Lois Chamboko alisema,Mkoa huo ni miongoni mwa Mikoa yenye hali duni ya lishe kutokana na takwimu za utafiti wa afya na viashiria vya malaria za mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Chomboko,takwimu zinaonyesha kuwa hali ya udumavu ni asilimia 35.6,uzito pungufu asilimia 12.2,upungufu wa damu kwa watoto asilimia 45 na upungufu wa damu kwa akina mama wajawazito asilimia 30