Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha kiongozi wa kiroho wa madhehebu ya Ismailia duniani na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan.
Rais Samia amesema amepokea kwa huzuni taarifa ya kifo cha Mwanamfalme Karim Al-Husseini, Aga Khan IV.
“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutoa rambirambi zetu za dhati na za moyoni kwa familia ya Mwanamfalme Karim, Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, na Jumuia ya Waislamu wa Ismailia,” amesema.
Rais Samia amesema Tanzania inaungana na jumuiya hiyo kuomboleza kifo cha kiongozi huyo mashuhuri na mwenye maono, ambaye kazi yake imegusa na kubadilisha maisha ya mamilioni ya watu kote ulimwenguni na kwamba fikra na maombi ya Watanzania yako nao katika kipindi hiki kigumu.
Kwa upande wake Rais Mwinyi amesema kwa niaba ya Serikali na Watu wa Zanzibar, anatoa pole kwa familia ya kiongozi huyo, Jumuia ya Waismailia, na wote walioguswa na alama aliyoacha.
“Tunapoomboleza msiba huu mkubwa, pia tunasherehekea kiongozi ambaye mazuri aliyofanya katika maisha yake yataendelea kuhamasisha vizazi vijavyo,” amesema Rais Mwinyi.
Aga Khan amefariki dunia huko Lisbon, Ureno akiwa na umri wa miaka 88.