Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema atalipia gharama zote za matibabu kwa mtoto aliyekatwa na kitu chenye ncha kali shingoni
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema mtoto huyo Maliki Hashimu (5) mkazi wa Goba mkoani Dar es Salaam anatibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na majeraha yalitenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti hivyo kusababisha ashindwe kupumua vizuri.
Aliongezea kuwa wataalamu bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili -MNH wamemfanyia upasuaji mkubwa mtoto huyo uliochukua saa nne ili kurekebisha njia ya hewa, sanduku la sauti, matezi aliyopata changamoto kwenye shingo na kutibu jereha la nyuma ya shingo.
“Jeraha la mbele ya shingo liliharibu tezi la mbele kwa kulikata katikati na kusababisha mtoto huyo kuvuja damu kwa wingi” alisema Waziti Ummy.
Pia mtoto huyo anapata maumivu kutokana na jeraha alilokatwa mbele ya shingo ambako hewa inayotoka kwenye mapafu hupita ili iweze kwenda kwenye sanduku la sauti kumuwezesha kuhema na kuzungumza.
Hospitali ya Taifa Muhimbili ilimpokea mtoto huyo usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii na kwa sasa yupo chini ya uangalizi maalumu akiendelea kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali hiyo Ummy amewapongeza watoa huduma kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhudumia wananchi kwa weledi.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ilisema mtoto huyo alijeruhiwa Julai 15 mwaka huu saa 12 jioni katika eneo la Goba Kinzudi, Kinondoni. Kamanda Muliro alisema mtuhumiwa ambaye alikuwa ni msichana wa kazi, Clemensia Cosmas alikimbia baada ya kutenda kosa hilo na sasa amekamatwa na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.
Baba wa Malick, Hashim Mohammed alisema Malick ndiye aliyemtaja binti huyo wakati mama yake alipomuuliza ni nani alimjeruhi. Inadaiwa kuwa Clemensia ni mkazi wa Kasulu mkoani Kigoma na amefanya kazi kwenye familia ya Mohammed kwa miezi saba.