Na Edward Kondela,JamhuriMedia

Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametimiza ndoto ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kujenga upya bwawa ambalo Mwalimu Nyerere alilijenga mwaka 1975 na kupasuka mwaka 1978.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, kukagua bwawa la Kaiwang katika Kijiji cha Ndedo ambalo likikamilika maji yake yatatumiwa na mifugo, wanyama wa porini pamoja na matumizi ya kibinadamu.

Naibu Waziri Ulega amesema ni fahari kubwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutimiza ndoto ya Hayati Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufuata maono yake kwa kuhakikisha bwawa hilo linaanza upya kufanya kazi mara baada ya kujengwa ambapo tayari mkandarasi ameshalifanyia tafiti mbalimbali na kwamba muda wowote ataanza kufanya kazi ya ujenzi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (katikati) akiwa na baadhi ya wananchi jamii ya wafugaji katika Kijiji cha Ndedo Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara na kuzungumza nao juu ya umuhimu wa kulitunza bwawa linalojengwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kufurahi nao namna walivyopokea taarifa ya ujenzi wa bwawa hilo lililopasuka Mwaka 1978, ambapo wananchi wameomba likikamilika liitwe Mama Samia Kaiwang. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anakuja kutimiza ndoto ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere anafanya mengi yaliyootwa na kuwazwa na Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwamba tayari fedha zimetengwa.” amesema Ulega.

Aidha,amewataka wakazi wa Wilaya ya Kiteto watakaolitumia bwawa hilo ambao wameomba liitwe Mama Samia Kaiwang kwa kushukuru jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kuhakikisha wanalitunza ili liweze kuleta tija kwao kwa kuwa watapata maji mengi na kuondokana na adha hiyo kwa mifugo yao.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Kiteto Edward Ole Lekaita akizungumza kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, amesema mradi huo utawafanya wananchi wa eneo hilo kumkumbuka Rais Dkt. Samia maisha yao yote kwa kuwa asilimia 90 ya wakazi wanaozunguka bwawa hilo ni wafugaji.

Ameongeza kuwa wanashukuru namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyoshughulika na changamoto zinazowakumbuka wananchi wakiwemo wafugaji hususan katika suala la mabwawa, malisho na majosho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto John Nchimbi ameelezea kuwa hadi sasa ujenzi wa bwawa hilo umefikia hatua ambayo eneo limeshafanyiwa tafiti mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya bwawa na uimara wa udongo ambapo matarajio ya ujenzi wa bwawa hilo utagharimu zaidi ya Shilingi Milioni 500.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (Mb), (wa kwanza) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mhe. Edward Ole Lekaita (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara Mhe. Mbaraka Al Haji Batenga (wa kwanza kushoto), wakati Mhe. Ulega akikagua maeneo ya bwawa la Kaiwang lililopo katika Wilaya ya Kiteto ambalo serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya Shilingi Milioni 500 kulijenga upya baada ya kupasuka na kutofanya kazi tangu Mwaka 1978. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Please follow and like us:
Pin Share