WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumaliza changamoto zinazohusu masuala ya kodi.
Majaliwa amehimiza jumuiya za wafanyabiashara ziendelee kuwa na imani na Rais Samia.
Alisema hayo alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na mwakilishi wa wafanyabiashara wa Halmashauri ya Makambako aliposimama na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo jana.
Majaliwa alisema Rais Samia anajali changamoto za wafanyabiashara, kwamba ndiyo maana ameunda timu mbalimbali kwa ajili ya kufanya mapitio ya kero za wafanyabiashara ili wafanye kazi kwa uhuru.
“Nataka niwatoe mashaka, mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan baada ya mapendekezo yenu wafanyabiashara yale kumi na tano, kufuatia mkutano na wafanyabiashara Kariakoo, ameunda tume inayofanya mapitio ya mfumo wa kodi Tanzania na inaendelea kuzunguka nchi nzima kufanya kazi hiyo,” alisema.
Majaliwa amempongeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda kwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato.
Pia, amempogeza kwa kuchukua hatua kwa watendaji wa TRA wanaokiuka maadili ya kazi.
Hivi karibuni, Mwenda alisema kuanzia Julai 2024 mpaka Februari mwaka huu, TRA ilikusanya Sh trilioni 21.20 sawa na ufanisi wa asilimia 104 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 20.42.
Alisema ukusanyaji huo ni sawa na ongezeko la Sh trilioni 9.28 na ni ukuaji wa asilimia 78 ikilinganishwa na Sh trilioni 11.92 zilizokusanywa Julai 2020 mpaka Februari 2021.
Pia, Mwenda alisema katika kipindi cha miaka minne, TRA imefukuza kazi watumishi 14, sita walishushwa mishahara, 12 walishushwa vyeo na kupunguzwa mishahara na 22 walionywa kwa maandishi.
Majaliwa ameiagiza TRA iendelee kuboresha programu za utoaji wa elimu kwa mlipakodi ili kuondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi.
“Serikali hii inamtaka kila Mtanzania ajue umuhimu wa kulipa kodi na tunajua kuwa sasa Watanzania wengi wanajua umuhimu wa kulipa kodi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alitembelea kiwanda cha uchakataji zao la parachichi cha Avo Afrika kilichopo mkoani Njombe.Alitoa wito kwa wakulima wa zao hilo waendelee kulilima kwa kuwa lina soko la uhakika.
