Samia atafuna mfupa wa mishahara mipya
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Hatimaye Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeongeza mishahara ikiwamo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Mei 14, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Zuhura Yunus, ni kwamba Rais Samia ameridhia mapendekezo hayo baada ya kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alichokifanya mjini Dodoma hivi karibuni na kupokea ripoti ya wataalamu kuhusu nyongeza ya mishahara.
Taarifa hiyo imesema nyongeza hiyo imefanyika kwa kuzingatia Pato la Taifa (GDP) na mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 na hali ya uchumi wa ndani na nje ya nchi.
Vilevile taarifa hiyo imesema kutokana na hatua hiyo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, serikali imepanga kutumia Sh trilioni 9.7 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala za Serikali.
Pia taarifa hiyo imesema bajeti ya mishahara ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 ina ongezeko la Sh trilioni 1.59 sawa na asilimia 19.51 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Katika hatua nyingine, taarifa hiyo imesema Rais Samia amepokea mapendekezo ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni kama Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) lilivyoomba Mei Mosi, 2022.
“Rais Samia ameridhia na kuieleza wizara yenye dhamana na masuala ya hifadhi ya jamii kuendelea kushirikiana na Tucta na Chama cha Waajiri (ATE) ili kukamilisha taratibu za kuhakikisha malipo ya mkupuo ya asilimia 25 yaliyokataliwa na wadau mwaka 2018 yanapandishwa hadi asilimia 33,” imesema taarifa hiyo.
Ahadi yatimia
Akizungumza katika sherehe za wafanyakazi duniani (Mei Mosi, 2022) zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Rais Samia, alitoa ahadi na kuwahakikishia wafanyakazi kuwa serikali yake katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 itaongeza mishahara.
Aidha, akasema nyongeza ya mishahara haitakuwa kwa kiasi kilichopendezwa na Tucta cha Sh milioni 1.01 kwa mwezi kwa sababu uchumi wa nchi na dunia kwa sasa si mzuri.
“Uchumi wetu ulishuka chini sana, tumejitahidi sana kwa sababu nilishatoa ahadi mwaka jana (ya kupandisha mishahara), nimeagiza liwepo, hesabu zinaendelea na tutajua lipo kwa kiasi gani?
“Ulezi wa mama unaendelea. Lile jambo letu lipo, si kwa kiwango kilichosemwa na Tucta cha kima cha chini cha Sh 1,010,000 kwa sababu hali ya uchumi wa nchi yetu na uchumi wa dunia si nzuri kwa sasa,” amesema.
Kuhusu wafanyakazi waliofukuzwa kwa vyeti feki lakini walifanya kazi kwa muda mrefu, Rais Samia ameagiza Wizara ya Fedha wakae na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufanya uchambuzi ni kiasi gani walikatwa katika mishahara yao na kuchangia katika mifuko ya jamii ili walipwe.
“Waangalie walitoa kiasi gani lakini nasisitiza ile asilimia tano waliyochangia kutoka katika mishahara yao na kuacha ile asilimia 10 ya mwajiri,” amesema.
Pia ameziagiza wizara hizo mbili kuangalia kiasi gani kitagharimu kuwalipa wafanyakazi waliofanya kazi kwa muda mrefu lakini wakabakisha mwaka mmoja ama miwili kustaafu.
“Waangalie ni kiasi gani kitatugharimu kama tutawapa mafao yao baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu na tunayafanyia uamuzi baada ya kuona ni gharama kiasi gani serikali itaingia,” amesema.
Kuhusu kiwango cha kikokotoo, amesema kimekuwa na mvutano lakini Tucta imetaka wakutane katikati ya 25 na 50.
“Serikali itakwenda kukaa katika utatu wetu ama sisi na Tucta kuangalia jinsi tutakavyokwenda kufanya. Lakini wazo mlilokuja nalo si baya. Ombi langu kwenu Tucta mtoe ushirikiano wa kutosha ili kwa mwaka huu ukimalizika lifanikiwe,” amesema.
Pia amesema hakuna mshahara wala mafao yanayotosha lakini walau kikokotoo kiwe kwa kiwango cha kuridhisha.
Wadau wapongeza, watoa maoni mbadala
Baadhi ya wadau wakiwamo wanasiasa, wanaharakati, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya wafanyakazi wamepongeza kitendo cha Rais Samia kuridhia nyongeza ya mishahara.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amepongeza kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter kwa kusema: “Kwa mara ya kwanza katika miaka saba watumishi wa umma wamepandishiwa mishahara! Mungu ni mkubwa sana.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema, amesema suala la wafanyakazi wa umma kuongezewa mishahara na kupandishwa madaraja kila mwaka ni takwa la kisheria.
Amesema kitendo cha serikali kwa miaka saba iliyopita kutowaongeza mishahara wafanyakazi wake ni kuvunja sheria.
“Kwa hiyo ni wajibu wa serikali kuendelea kufanya jambo hilo na kwa hatua ya sasa hatuwezi kupongeza huo wajibu kwa sababu hatujui kama mwakani bado utakuwapo au ndiyo mwaka huu tu halafu wasubiri miaka mingine saba au minne ijayo,” amesema Mrema.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, amesema walimu waliielewa vizuri kauli ya Rais Samia aliyoitoa Mei Mosi, 2022 kuhusu ahadi ya nyongeza ya mishahara na wamemshukuru kwa kuitimiza kwa kuongeza asilimia 23.3.
“Tulisema tuna imani na mama, naona jambo limekamilika. Baada ya kauli yako ya Mei Mosi, walimu tulikuelewa na tukasema tupo pamoja nawe, tunachapa kazi. Kama uliweza kuwapandishia madaraja (vyeo) katika kipindi cha mwaka 2021/2022 pekee sawa na asilimia 92.9 ya walimu wote ambao ni takriban 260,000 na hata hili la kuongeza mishahara tulijua tu litafanikiwa.
“Kama umetoa ajira kwa awamu kadhaa, ya kwanza walimu 13,000, ya pili 7,000 na ya tatu ni hii ya juzi ya 12,000 ambayo ni sawa na asilimia 15 ya walimu waliopo na kuwapandisha madaraja mwaka jana walimu 127,000 na mwaka huu zaidi ya 60,000 watakaonufaika na daraja la mserereko ni walimu 52,000. Na jumla walionufaika na madaraja ni sawa na asilimia 92.9 na hili tulijua litakamilika tu,” amesema Mwalimu Seif.
Kwa upande wake, Mratibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Mohamed Iddi Mohamed (Abuu Iddi), amesema Rais Samia amelifanya suala la kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kwa utaalamu mkubwa.
“Jambo la kupandisha kiasi cha mishahara ya kima cha chini kwa asilimia 23.3 na kupunguza baadhi ya kodi za makato kwa wafanyakazi halikufanyika kwa muda usiopungua miaka sita. Katika hilo, tumpongeze Rais Samia,” amesema Sheikh Abuu.
Awali, wadau wengine walikuwa na mtazamo tofauti kuhusu kupanda kwa mishahara pindi waliponukuliwa na vyombo vingine vya habari hivi karibuni.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa, amesema ni makosa kwa wafanyakazi kukaa miaka saba bila nyongeza ya mishahara huku gharama za maisha zikizidi kuongezeka.
“Huko nyuma ilikuwa kila mwaka mishahara inaongezeka, makosa yalifanyika awamu iliyopita kuwaacha wafanyakazi miaka mingi bila nyongeza ya mishahara, kwa kuwa kunadhoofisha ari na tija katika kazi zao,” amesema.
Pia amesema nia iliyoonyeshwa na Rais Samia ya kuongeza mishahara iwe endelevu kila mwaka na watumishi walipwe kuendana na uhalisia wa gharama za maisha.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amesema pamoja na nyongeza hiyo lakini inapaswa kuendana na mfumuko wa bei na serikali haina budi kuongeza mishahara ya watumishi kila mwaka ili kutekeleza haki yao.
“Nyongeza ni wajibu wa serikali kila mwaka, lakini mimi si muumini wa kutangaza, waongeze mishahara wapitishe waraka kimya kimya, watu wawe na uchumi endelevu. Ukitangaza kuna watu watapandisha bei za bidhaa,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, amewapongeza wafanyakazi kwa kumuunga mkono Rais Samia kuhusu nyongeza ya mishahara.
“Katibu Mkuu wa Tucta amesema walikutana na Rais siku moja kabla ya sherehe za Mei Mosi na kukubaliana juu ya ajenda ya nyongeza ya mishahara.
“Kwamba Rais Samia aliwahakikishia kuwa serikali itapiga hesabu na nyongeza hiyo itapatikana katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai, 2022,” amesema.
Shaka amesema uamuzi wa Rais Samia kukubali wafanyakazi waliofukuzwa baada ya kukutwa na vyeti feki kulipwa stahiki zao unapaswa kuungwa mkono kwa sababu wengi waliathirika.
“Rais Samia anasimamia masilahi mapana ya wafanyakazi nchini, alichokifanya si porojo ama utashi wake, bali ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kuhusu kutetea masilahi ya wafanyakazi nchini,” amesema.
MWISHO