Pazia la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA) linafunguliwa rasmi leo kwa msimu wa 2019/2020 ambapo timu 16 zitakuwa uwanjani zikipepetana na nyingine idadi sawa na hiyo zitapambana kesho katika hatua ya kwanza ya kutafuta bingwa.

Katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, KRC Genk ambayo anachezea Mtanzania Mbwana Samatta imepangwa kundi ‘E’, ambalo linajumuisha bingwa mtetezi wa michuano hiyo, Liverpool, Napoli na timu ya Salzburg.

Genk inayoongozwa na mfungaji bora wa Ligi Kuu nchini Ubelgiji msimu uliopita, Mbwana Samatta, leo itakuwa ugenini kucheza na timu ya Salzburg ya Austria kwenye dimba la Stadion Salzburg.

Mchezo mwingine wa kundi ‘E’ utakuwa kati ya timu ya Italia, Napoli inayonolewa na Kocha mwenye historia kubwa katika michuano hiyo, Carlo Ancelotti, ambaye ametwaa kombe hilo mara tatu akiwa na AC Milan msimu wa 2002/2003; 2006/2007 na Real Madrid 2013/2014. Napoli wanawakaribisha mabingwa watetezi Liverpool katika dimba la San Paolo nchini Italia.

Msimu huu Genk imeanza vema katika Ligi Kuu nchini Ubelgiji baada ya kuvuna pointi 10 katika michezo minne waliyocheza msimu huu dhidi ya wapinzani wao. Msimu huu Samatta ameendeleza wimbi lake la kufunga magoli katika ligi hiyo baada ya kufumania nyavu mara tano hadi sasa katika mechi nne alizocheza.

Timu ya Salzburg imeuanza msimu vizuri katika Ligi Kuu ya Austria baada ya kushinda michezo yote sita waliyocheza na kuongoza ligi hiyo baada ya kuvuna pointi 16. Timu ya Salzburg ni miongoni mwa timu zinazofuzu kushiriki mara nyingi michuano ya UEFA lakini huwa haifiki mbali.

Samatta ataingia uwanjani usiku wa leo huku akiweka rekodi kubwa kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA).

Timu ya Genk inashiriki michuano hiyo baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji msimu wa 2018/2019.

KRC Genk inayonolewa na Kocha Felice Mazzu itashuka dimbani usiku wa leo huku historia ya UEFA ikiwaonyesha mara ya mwisho kushiriki michuano hiyo ni msimu wa 2002/2003.

Msimu wa 2016/2017 Genk ilifanikiwa kushiriki Ligi ya Europa, kombe ambalo ni la pili kwa ukubwa baada ya Ligi ya Mabingwa.

Samatta amerejea Ubelgiji hivi karibuni kujiunga na Klabu yake ya Genk akitoka kuichezea timu ya Taifa Stars, ambapo wamefanikiwa kuingia katika hatua ya makundi baada ya kuifunga timu ya taifa ya Burundi kwa mikwaju ya penalti, katika michuano ya kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia, mashindano yatakayofanyika nchini Qatar mwaka 2022.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Samatta pamoja na Victor Wanyama, aliyekuwa akiichezea Klabu ya Tottenham  ndio wachezaji pekee wa ukanda huo ambao klabu zao zinashiriki katika michuano ya UEFA. Michuano inayopendwa zaidi kwa upande wa klabu duniani.

Samatta alijiunga na Genk mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya kufanya vizuri katika klabu yake hiyo ya awali, ambako aling’ara na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa barani Afrika.

Samatta alikuwa mfungaji bora na mchezaji bora katika fainali hizo za mwaka 2016.