“Kuwa mbali na umaskini, ni hali iliyo njema mno.
Na afya kama haba mwilini, ni taabu haina mfano.
Kuwa na rafiki sheriani, uborawe si wa mlingano.
Hushinda fedha ya mfukoni isiyoweza kutenda neno.
Na laiti si machukiano, tungalikuwa wote peponi!
Amani yetu haba moyoni, kwa uadui na magombano.
Kama hatuna matumaini, na ukunjufu na tangamano.
Tunao ukufi wa imani, katika pori la makindano.
Fahari yetu duni thamani, kwa kukosa masikilizano.
Ubora wetu ni mapatano, na leo huwaje nuksani?
N
imenukuu tungo mbili hizo za ushairi kutoka kitabu ‘KIELEZO CHA FASIHI’ cha mtunzi na gwiji wa lugha ya Kiswahili, Sheikh Shaaban Robert, nikiwa na lengo la kuweka mkazo na msisitizo kuhusu fikira na moano katika falsafa na itikadi ya siasa Tanzania, hasa wakati huu vyama vya siasa vinapovutana na Serikali katika mustakbali wa uhuru, haki na ukweli katika maisha.
Naamini ukitambua thamani na ubora wa uhuru wako, haki zako na ukweli wa kauli yako, kamwe huwezi kutia nuksani katika utawala na uongozi wako binafsi, au wa kikundi fulani wala wa Serikali. Ukifanya kinyume cha hayo ni dhahiri shahiri kujitia mashakani. Hilo si jambo jema.
Yapata sasa ni siku arobaini, Watanzania tumeona na kusikia mvutano kati ya chama cha siasa Chadema na Serikali kuhusu siasa inayobeba dhana ‘demokrasia na utawala bora’ hauko kwenye reli yake.
Chadema wanatoa maelezo kuwa hawakubali ‘mchepuko’ huo wa reli unaofanywa na Serikali. Una dalili ya kufifilisha haki na demokrasia nchini. Serikali inajibu kuwa hakuna ‘mchepuko’. Inataka kufanya kazi. Watanzania hawana budi kurudi kwenye kutii na kufuata sheria za nchi na kuheshimu mamlaka iliyoko madarakani.
Kaulimbili hizo zimezua ubishi wa kisheria, kiburi na ubabe wa kisiasa, kati ya Chadema na Serikali kuvimbishiana msuli na kutia hofu baadhi ya watu. Laiti tafsiri na maana sahihi ya sheria na matumizi ya maneno ya kisiasa yangeenziwa ipasavyo, kamwe mtafaruku usingetokea.
Kuzungumzia Katiba maana yake ni kuzungumzia sheria. Kuzungumzia haki maana yake ni kuzungumzia sheria. Kubisha na kuvimbisha msuli katika hili ni kukiuka sheria zilizopo na kutoheshimu mamlaka husika.
Unapotambua, unapochambua na unapozingatia sheria ipasavo, huwa unajiweka salama mikononi mwa sheria. Hapa, utendaji na ufanisi wa kazi huonekana na kupiga teke umaskini na kukaribisha utajiri (uchumi). Si chama cha siasa wala serikali duniani isiyopenda maendeleo ya kiuchumi.
Kadhalika, watu wengi duniani wanapenda amani na maisha bora katika chakula, mavazi na makazi. Ni wachache ambao hudiriki kuwarubuni na kuwasaliti wenzao wasiwe na maisha bora ila ni wao tu ndiyo wanaostahiki. Ni busara jambo kama hilo kuepukwa.
Mamlaka zenye kutambua na kufuata sheria huwa daima zinaelekeza jamii kujenga imani ya upendo na uelewano. Hufanya kazi na kutii imani ya roho na kamwe haziendi kinyume mbele ya makasisi na masheikh.
Tungo za marehemu Shaaban Robert zinatuhimiza na kututaka tuwe wachapakazi, tuwe karibu na sheria, tuthamini afya zetu na tujenge utangamano. Tuepuke machukiano ili tuingie kwenye pepo; na kwenye ufalme wa mbinguni.
Kuahirisha UKUTA ni jambo jema, kuuondoa ni bora zaidi na usalama. Viongozi wa siasa, dini na Serikali tumieni muda huu kuweka mambo sawa.
Linalowezekana leo halingoji kesho. Inawezekana timizeni wajibu wenu.