Serikali sasa imeamua kumtumia Mbwana Samatta katika kuuza utalii wa Tanzania duniani. Samatta anasakata soka katika klabu ya Genk, Ubelgiji.
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii, imetangaza nia ya kuanza kumtumia mchezaji huyo pekee anayecheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii, Devota Mdachi, anasema bodi yake imejiwekea malengo ya kuhakikisha mchango wa utalii katika pato la Taifa unafikia asilimia 20 kutoka asilimia 17.5 ya mwaka jana.
Anasema juhudi za kuhakikisha mchezaji huyo anakuwa balozi wa kutangaza utalii nje ya nchi, zimeanza Juni, mwaka huu, bada ya ofisi yake kumualika mchezaji huyo na kumuomba ushirikiano katika kuutangaza utalii nje ya nchi.
Mdachi anasema katika mazungumzo na mchezaji huyo, bodi ilimuomba awe balozi wa hiari wa utalii na alikubali lakini kwa kutokana na uchache wa muda aliokuwa nao, hakuweza kwenda kutembelea vivutio vya utalii.
Anasema bodi kwa kushirikiana na wadu wa utalii wanaweza kupanua wigo wa utalii endapo juhudi za pamoja zitapatikana kwa kuwashirikisha Watanzania waishio ndani na nje ya mipaka katika kuutangaza utalii.
“Tulimuomba Samatta awaambie ukweli watu wote anaokutana nao katika shughuli zake za kawaida kuwa Tanzania kuna vivutio vya aina mbalimbali ikiwamo mbuga za wanyama pamoja na uwepo wa Mlima Kilimanjaro…awaambie mlima huo uko Tanzania na si Kenya kama inavyofahamika kwenye baadhi ya mataifa Ulaya na kwingine,” anasema Mdachi.
Anaongeza kuwa wanatarajia kukamilisha mazungumzo na mchezaji huyo atakaporudi likizo mwenzi Desemba, na atapatiwa elimu zaidi baada ya kuona vivutio vilivyopo na awape mialiko wachezaji wenzake kuja kuitembelea Tanzania.
Mdachi anatoa wito kwa Watanzania mahali popote walipo kuendelea kuunga mkono juhudi za Bodi ya Utalii, kuvitangaza vivutio utalii kwa kujibu na kusahihisha papo hapo bila woga mara tu taarifa ya upotoshaji kuhusu vivutio vilivyopo nchini inapotolewa – iwe ni kwenye mikutano ya ndani ya nchi au ya kimataifa.
Anasema ni jukumu la kila Mtanzania kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii badala ya kuiachia TTB kazi hii peke yake, huku baadhi ya watu wasiotutakia mema wakiendelea kueneza uongo kila kukicha dhidi ya sekta yote ya utalii hapa nchini.
Anasema ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau wengi wa utalii hapa nchini, halijaathiri sekta hiyo na badala yake mapato yameongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Anasema lengo la kuweka mkazo huo ni kuhakikisha robo ya fedha za kigeni zinazoingia nchini zinatokana na pato la utalii na hilo linawezekana kwa kuwa hadi sasa kuna kasi ya ongezeko la watalii nchini.
“Msimu mkubwa wa utalii umeanza na tumeona matokeo ya kazi tulizofanya, watalii wanaokuja Tanzania mwaka huu ni wengi sasa, mfano kutoka Juni hadi Agosti mwaka huu ikilinganishwa na kipindi hiki kwa mwaka jana, kuna ongezeko la asilimia 20 la watalii,” anasema Mdachi.
Anasema ongezeko hilo si tu kwa watalii wanaokuja nchini, bali pia limeongeza mapato ya utalii kwa asilimia 22, na kusisitiza kuwa ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani inayotozwa kwenye huduma za utalii nchini haijaathiri watalii wanaoingia nchini.
“Ni jambo zuri kuona kuna ongezeko la watalii wanaoingia nchini, lakini pia kuna ongezeko la mapato kwa zaidi ya asilimia 22, licha ya watu kuzungumza matatizo mambo wasiyoyajua vizuri ukweli wake,” amesema Mdachi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe anasema kwa mara ya kwanza Tanzania imebahatika kutoa mchezaji Mbwana Samatta mwenye kiwango cha kimataifa.
Anasema mchezo wa soka unaopendwa na watu wengi nchini na duniani kote, hali ambayo inaweza kutoa mwanya mkubwa kwa wizara kutumia nafasi hiyo kuwafikia watu wengi hapa nchini na duniani kote.
Anasema mataifa mengi yenye vivutio vya utalii barani afrika na duniani kote wamekuwa wakiwatumia wanamichezo wake wanaocheza ligi za nje au ndani kutangaza utalii wake na niyingi zimeonyesha kufanikiwa katika hilo.
“Tunaanzisha mikakati ya makusudi kuhakikisha tunawatumia wachezaji wetu walioko ndani na nje ya nchi kuutangaza Utalii wetu, tunaanza na Mbwana Samatta ambaye tunadhani atakuwa mwakilishi wetu mzuri huko aliko” anasema Magembe.
Profesa Maghembe anasema bajeti ya 2015/2016 urejeshwaji wa kodi hiyo ulijadiliwa na wadau waliomba kupewa muda wa kujiandaa kwa mwaka mmoja na kwamba mwaka huu kwenye bajeti ya 2016/17, Serikali ilirejesha kodi hiyo, na wadau walilalamika ilhali walikuwa wakijua hilo.
Anasema pamoja na changamoto mbalimbali Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika kunadi vivutio vya utalii vilivyoko hapa nchini, hii inatokana na hatu za makusudi katika suala zima la uhifadhi kwenye maeneo ya ulinzi wa maliasili.
Anasema uthubutu huo umezaa mafanikio makubwa kwenye mapambano dhidi ya ujangili kwenye hifadhi zetu kupitia njia mbalimbali ikiwamo uanzishaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na kusababisha idadi ya wanyamapori waliokuwa hatarini kutoweka sasa inaongezeka.
Anasema hata utafiti uliofanywa na mtandao wa kimataifa wa Uholanzi unaoshughulika na masuala ya utalii wa safaribookings.com, uliotumia takriban miaka miwili kukusanya maoni ya watalii maarufu na wataalamu wa masuala ya maliasili kote duniani, waliitaja Tanzania kuwa ni sehemu salama kwa utalii.
Anasema matokeo yalitaja watu 1,000 kutoka nchi 53 walihusishwa kwenye utafiti huo ambao kati ya jumla ya pointi zilizotolewa kwa wastani, na Tanzania ilipata pointi 4.8 ambazo ndiyo alama za juu ikifuatiwa na Botswana yenye pointi 4.75, Kenya 4.66; Zambia 4.58; Afrika Kusini 4.55; Namibia 4.54; Uganda 4.16 na Zimbabwe 4.14.
Anasema sababu zilizotajwa na watafiti hao kuwa siri ya ushindi wa Tanzania barani Afrika kwenye sekta ya utalii ni utajiri wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori ambayo mawili kati yao ni maeneo ya urithi wa dunia yanayotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO.
Anasema sababu nyingine ni maisha ya asili ya wanyamapori hifadhini Serengeti ambako kwa mwaka zaidi ya wanyama hasa nyumbu milioni mbili huhama kuelekea Mbuga ya Maasai Mara kwa upande wa Kenya kisha kurudi nchini.