SamattaUshindi wa Mtanzania Mbwana Samatta umewafungua vinywa Watanzania na kutaka kiwekwe kwenye Katiba, kifungu kitakachotambua na kuwaenzi wanamichezo watakaoiletea sifa nchi katika kipindi chao chote cha maisha kama wanavyofanyiwa viongozi wa nchi.

Wametaka kifungu hicho kiwatambue wanamichezo hao kwa kuwapatia huduma mbalimbali muhimu kama vile mafao hadi mwisho wa maisha yao kuliko ilivyo hivi sasa.

Samatta, nyota wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ameuanza mwaka vizuri kwa kuchaguliwa kuwa Mwanasoka Bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN). 

Akizungumza katika kipindi cha ‘Asubuhi ya Michezo’ kinachorushwa hewani na Radio Tumaini ya Dar es Salaam, Michael Mtembezi anasema wanamichezo wengi wamekuwa wakiiletea sifa nchi lakini mwisho wa siku huishia kuwa na maisha mabaya.

“Kikubwa ninachoshauri ni kwamba Serikali iweke kwenye Katiba kipengele kitakachowatambua wanamichezo wanaoiletea sifa Tanzania na wapewe mafao hadi mwisho wa maisha yao,” alisema.

Alisema huko nyuma Taifa limeshuhudia wanamichezo wengi wakishinda katika mashindano mbalimbali, lakini mwisho wa siku wamekuwa wakiishia kupewa sifa tu na baadaye sifa huishia kuwa katika maisha magumu yasiyo na mfano.

“Hivi sasa tunashuhudia sifa anazomwagiwa Samatta na Serikali lakini baadaye hupotea. Nashauri iwekwe kwenye Katiba namna ya kuwahudumia maisha yao yote kama wanavyohudumiwa viongozi kwa kupewa mafao mbalimbali,” amesema Mtembezi.

Naye Ayoub Bakari anasema nchi nyingi duniani zimekuwa zikiwathamini wanamichezo wao kwa namna mbalimbali kutokana na kuziletea sifa nchi zo, lakini jambo hilo limekuwa ni ndoto kwa Tanzania.

Bakari, ambaye amezungumza na JAMHURI, anaeleza kuwa wakati sasa umefika kwa Tanzania kuachana na mazoea kwa kuishia kuwamwagia sifa pekee wanamichezo hao kisha baadaye kuwaacha katika hali mbaya kiuchumi.

Elizabeth Shirima anaeleza vyema wanamichezo hao kama wanasoka, wanamuziki pamoja na wasanii mbalimbali wakaenziwa kwa namna mbalimbali ili nao wajione ni watu muhimu, kuliko kuwaacha katika hali mbaya kama wanavyofanyiwa sasa.

Siku chache baada ya Samatta kutangazwa mshindi kwenye tuzo hiyo, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, amemteua Samatta kuwa nahodha mpya wa ‘Taifa Stars’.

Samatta anakuwa nahodha mpya wa Stars akichukua nafasi ya mkongwe Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho kwa muda mrefu tangu aliporithi kijiti hicho kutoka kwa Shadrack Nsajigwa.

Uamuzi huo wa Mkwasa umekuja kutokana na nyota huyo wa Tanzania kukidhi vigezo vyote vya kuwa nahodha wa timu ya Taifa kwa kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, sambamba na kujituma kila anapokuwa kwenye timu ya Taifa, uwezo wake wa kuzungumza na kila mchezaji lakini pia kupata mafanikio makubwa kwenye soka la Afrika.

Mkwasa amesema kuwa anafikiri ni mabadiliko ya kawaida baada ya kupata tuzo na heshima kubwa Afrika, wameamua kumuongezea majukumu mengine ili aweze kutuongozea timu yetu ya Taifa na Watanzania kwa ujumla. Ameweza kuiongoza vizuri TP Mazembe na kuwa Mabingwa wa Afrika, sasa tumeona tumpe fursa hii awaongoze wenzake kwa hizi mechi za AFCON zilizobaki.

“Ingawa tumechelewa lakini hatuna jinsi, tumempa nafasi hiyo akisaidiwa na John Bocco, Cannavaro tunampa jukumu la kusimamia timu ya CHAN lakini tunamtafutia nafasi nyingine katika Stars”.

Kupewa unahodha kwa Samatta hakumaanishi kwamba Cannavaro amepoteza sifa na vigezo vya kuwa nahodha, bali ni kuthamini heshima ambayo Samatta ameiletea Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo hiyo kwenye ukanda huu.

Cannavaro bado ataendelea kuwa kiongozi wa Stars kutokana na uzoefu alionao kwenye timu hiyo, lakini pia kutokana na mafanikio aliyoiletea Tanzania kupitia Stars pamoja na kudumu kwa kiwango chake kwa muda wote ambao amekuwa akikitumikia kikosi cha timu ya Taifa.

Jellah Mtagwa na Peter Tino ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kuiletea sifa Tanzania. Mtagwa, aliyewahi kucheza Yanga alikuwa pia nahodha na beki wa timu ya Taifa na Klabu ya Pan African ya Dar es Salaam, hivi sasa maisha yake ni dhooful hali.

Wanamichezo wengine waliowahi kuitangaza Tanzania kutokana na kuiletea heshima na medali mbalimbali ni wanariadha Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na wengine.

Kwa upande wa sanaa, wapo Wanne Star, Mrisho Mpoto na wengine huku kwenye filamu, Steven Kanumba naye akiiweka pazuri Tanzania kutokana na kujulikana kimataifa.