Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Yanga umetoa maombi matatu kwa kamati ya TFF ya maadili na hadhi ya wachezaji kufuatia sakata la mchezaji wao Yusuph Kagoma ambaye anaendelea kucheza klabu ya Simba kinyume na sheria, ambapo kwa sasa amesafiri nao kuelekea Libya kwenye mechi ya kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli.
Yanga wameomba kamati itamke kwamba Yusuph Kagoma ni mchezaji halali wa Yanga, pili isimamie kanuni ya 41 (13) inayoeleza wazi mchezaji anayesaini mkataba kwa vilabu viwili afungiwe, pamoja na kutoa adhabu ya kumtaka mchezaji awalipe fidia kwa kosa la kuvunja mkataba wao ambao mpaka sasa upo hai kihalali.
Akizungumza na wanahabari leo, Mkurugenzi wa sheria wa Yanga, Simon Patrick ameanika hadharani mkataba wa Yanga na Kagoma waliousaini Mwezi Aprili, sambamba na kuelezea mchakato mzima wa usajili wa mchezaji huo ulivyofanyika.
“Ilikuwa tarehe 04, mwezi wa tatu, mwaka 2024, klabu ya Yanga kupitia kamati ya utendaji walianzisha mchakato rasmi wa maongezi wa kumsajili mchezaji Yusuph Kagoma kutoka Singida Fountain Gate, baada ya maongezi uongozi wa Singida FG uliipa Yanga masharti ya kulipa Milioni 30, kama ada ya kumnunua mchezaji”
“Klabu ya Yanga na Fountain Gate waliingia makubaliano rasmia ya kimkataba ya kumnunua mchezaji huyo Yusuph Kagoma, na sharti za mkataba huo ilikuwa ni Yanga kulipa Milioni 30, mkataba umesainiwa na pande zote mbili na kuwekwa na sahihi na klabu ya Singida Fountain Gate”.
‘Kipengele cha tatu cha mkataba kinasema Yanga watalipa hizo Milioni 30 kwa awamu mbili, awamu ya kwanza watalipa Milioni 15, mwisho wa mwezi wa pili, na awamu ya pili watalipa Milioni 15 mwisho wa mwezi wa sita, ambapo tarehe (30, 4, 2024) klabu ya Yanga ilifanya malipo kwa klabu ya Singida FG ya Milioni 30 ya kumnunua huyu mchezaji, kwahiyo kwa mujibu wa makubaliano yetu klabu ya Yanga tayari tumeshamnunua mchezaji na tukalipa”
“Baada ya kufanya malipo, klabu ya Yanga iliruhusiwa kukaa karibu na mchezaji ili kuanza maongezi ya kukubaliana maslahi binafsi, tarehe (27, 03, 2024) ilimtumia mchezaji Yusuph Kagoma tiketi ya ndege Air Tanzania kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam, alivyofika uongozi ulifanya nae mazungumzo na kisha tarehe (28, 03, 2024) tuliweza rasmi kusaini mkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Yusuph kagoma wa misimu mitatu akiwakilishwa na wakili wake, Leonard Richard, “
“Baada ya hapo klabu ya Yanga ikajiridhisha kwamba tumemaliza dili na huyu mchezaji, lakini masharti ya huu mkataba ni kwamba kwa sababu dirisha la usajili halijafunguliwa basi utaanza kufanya kazi kuanzia tarehe (1,07, 2024) na utaisha mwisho wa msimu wa mwaka 2026/27, kwahiyo ulikuwa ni mkataba wa misimu mitatu, mpaka sasahivi huu mkataba ni hai na hakuna chombo chochote chenye mamlaka kimevunja huu mkataba”
Aidha mwanasheria simon ameeleza kuwa siku chache baada ya kumalizana na Kagoma, walipokea barua kutoka Singida FG ikiwaomba kufidia Milioni 30 waliyotoa kumsajili Kagoma kwenye malipo ya Nickson Kibabage ambaye alikuwa Yanga kwa mkopo akitokea kwao.
Jambo ambalo Yanga hawakukubaliana nalo na badala yake Julai 06, 2024 wakatoa Milioni 30 nyingine na kuwalipa Singida FG ya ada ya kumnunua Kibabage bila kuingiliana na usajili wa Kagoma ambao tayari ulishakamilika.
“Septemba 05, uongozi wa mchezaji na mchezaji mwenyewe waliufata uongozi wa klabu ya Yanga, kuomba tumalize hili suala nje ya kamati na wakaandika kwamba wangetamani tuwe na makubaliano ya kutoa shauri kwenye kamati na waombe radhi , lakini hakuna kilichofanyika, kwa sababu Singida wameshainjoi hela ya wanachama wa Yanga, na mchezaji ameshasaini mkataba na Yanga ina maana mchezaji Yusuph Kagoma ana mikataba na klabu mbili”