Sakata la Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, kudaiwa kutoa zabuni ya uchapaji wa nyaraka za Serikali kwa Kampuni ya Yuko’s Enterprises Ltd ya mkoani Pwani bila kufuata taratibu limechukua sura mpya.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Kassian Chibogoyo, kutetea zabuni iliyotolewa kwa Kampuni ya Yuko’s Enterprises Ltd.

Kampuni ya Yukos imepewa kazi ya kuchapa mitihani ya kidato cha pili, darasa la saba na fomu za shule ya msingi namba tisa (TSM 9) bila kutangazwa ambavyo vilikuwa zikichapwa na kampuni tofauti katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Sagini alitoa zabuni hiyo kwa Kampuni ya Yukos kwa mtindo wa zabuni ya chanzo pekee (Single Source) ambayo kwa mujibu wa sheria ya ununuzi ya mwaka 2004 malipo yake hayatakiwi kulipwa kwa zaidi ya Sh milioni 200 kwa kampuni itakayopewa zabuni.

Akizungumza na JAMHURI kwa masharti ya kutotajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji wa Mamlaka ya Ununuzi Serikalini (PPRA) mmoja wa wafanyakazi  wa mamlaka hiyo amesema utetezi huo si sahihi.

“Naweza kusema kilichofanywa na Katibu Mkuu si sahihi kwani kuna wachapaji wengi hapa nchini, sasa sijui kwanini alitumia sheria gani kutoa zabuni bila kutangaza

“Huwezi kusema unatumia chanzo kimoja katika saula la uchapaji wakati wako wachapaji wengi mno hivyo ni lazima utangaze zabuni watu waombe,” amesema.

Amesema kwamba taratibu za ununuzi wa chanzo kimoja mzabuni anaweza kupewa akiwa pekee yake iwapo hakuna washindani wengine.

Amesema hatua nyingine ni zabuni ya chanzo kimoja inaweza kutumuika pia iwapo itatolewa wakati wa majanga kama mafuriko au moto.

Ameongeza kwamba utaratibu mwingine wa zabuni ya chanzo kimoja ni kama itaonekana kwamba vifaa vilivyopo vipo katika muuzaji mmoja.

Amesema kwamba Katibu Mkuu alitakiwa kutangaza zabuni hiyo na wachapaji kushindanishwa na mwisho atakayeshinda apawe kazi hiyo.

Amesema utaratibu wa chanzo kimoja si wa kitaifa bali ni wa kimkoa, hivyo kampuni hiyo haikustahili kupewa zabuni hiyo bali ilitakiwa kufanya kazi za mkoa wa Pwani na kazi nyingine zingefanywa na kampuni nyingine.

Kampuni hiyo kwa mwaka jana ilipewa kazi ya kuchapa fomu za TSM9 kwa kuchapa fomu 868,030 ambazo kwa mwaka jana ziligharimu Sh 3,298,514,000.

Pia ilichapa mtihani wa darasa la nne kwa idadi hiyo hiyo ya wanafunzi na kulipwa kiasi kama hicho cha fedha.

Uchunguzi huo umebaini kwamba kampuni hiyo ilipewa kazi ya kuchapa mitihani wa kidato cha pili 531,457  kwa malipo ya Sh 2,019,536,600.

Hivyo, kampuni hiyo kwa mwaka jana ililipwa Sh 8,616,564,600 kinyume na masharti ya zabuni iliyotolewa ambayo ilitakiwa kulipwa malipo yasiyozidi Sh milioni 200.