*Ikulu, ofisi ya CAG washangazwa kuachiwa
*Uamuzi uliofanywa na DPP wazua maswali
Kuachiwa kwa mwanasiasa Iddi Simba, ambaye hivi karibuni alikuwa akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kabla ya Mkurugenzi wa Mshitaka nchini (DPP), kuamuru awe huru, kumeibua mgongano mkubwa serikalini.
Moja ya mashitaka yanayomkabili Simba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ni kuingizwa kwenye akaunti yake binafsi Sh milioni 320 kutoka kwa mnunuzi wa shirika hilo. Alikiri kupokea fedha hizo akisema zilikuwa ni malipo kutokana na ushauri (wa kuuza UDA?) aliompatia mnunuzi, kampuni ya Simon Group.
Ripoti ya Ukaguzi Maalum ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilibaini ubadhirifu wa kupindukia katika UDA na kupendekeza Simba na wenzake washitakiwe, akisisitiza kuwa upo ushahidi wa kutosha wa kuendesha kesi hiyo.
Hata hivyo, katika hatua iliyowashtua wengi, kesi ya uhujumu uchumi iliyofunguliwa dhidi ya watuhumiwa hao, ikafutwa kwa uamuzi wa DPP.
Mgongano wa wazi umejitokeza kati ya Ofisi ya DPP, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Katiba na Sheria, na Ikulu.
Habari za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali zinasema umekuwapo mvurugano wa wazi kati ya DPP na Takukuru. Takukuru wamekasirishwa na uamuzi wa DPP wa kumwachia Simba anayekabiliwa na tuhuma za kuuza hisa za UDA kwa bei ya kutupa, na hivyo kuisababishia hasara ya shilingi zaidi ya bilioni saba.
Kwa upande mwingine, Ofisi ya DPP nayo inawalalamikia Takukuru kwamba hawakuipatia ushirikiano, na ndiyo maana ukafikiwa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo.
Kwa upande mwingine, chanzo cha habari kimedokeza kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amenukuliwa akieleza mshangao wake juu ya kuachiwa kwa Simba licha ya kuwapo ushahidi unaojitosheleza.
Mmoja wa maofisa katika Ofisi ya AG amenukuliwa akisema, “AG nimemsikia akisema kufutwa kwa kesi hiyo ni embarrassment (maudhi, aibu)…ametumia hilo neno embarrassment akionesha kutoridhishwa na kilichofanywa na DPP.”
Hata hivyo, Jaji Werema alipoombwa na JAMHURI aweze kueleza msimamo wake juu ya jambo hilo, alijibu kwa kifupi, “Sasa tupo Dodoma, ngoja turudi Dar es Salaam, kwa sasa sina taarifa zozote zaidi ya kusoma kwenye magazeti kuwa kesi imefutwa.” Alipoombwa afafanue kama kuachiwa kwa Simba ni aibu, alijibu kwa ukali kidogo, “Nasema ngoja nirudi Dar es Salaam.”
Chanzo cha habari kutoka Ikulu kinasema kuachiwa kwa Simba kumeishtua Ikulu ambayo mara kadhaa imewahakikishia Watanzania kwamba imedhamiria kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Kauli hiyo inazima tetesi zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuachiwa kwa Simba ni shinikizo la ofisi hiyo kubwa nchini, hasa kutokana na ukaribu wake na Simba ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kabla ya kushinikizwa kujiuzulu kutokana na kashfa ya minofu ya samaki.
Hivi karibuni, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam iliwaachia huru Simba na wenzake wawili – Salum Mwaking’inda, aliyekuwa Mkurugenzi wa UDA na Meneja wa shirika hilo, Victor Milanzi.
Juni 18, mwaka huu, kesi hiyo ilifikishwa Kisutu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, lakini Wakili wa Serikali, Awamu Mbangwa, aliwasilisha hati chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Mashauri ya Jinai (CPA), kwa niaba ya DPP akiomba kesi hiyo ifutwe kwa sababu hana nia ya kuendelea kuwashitaki watuhumiwa.
Baada ya kuwasilisha hati hiyo, Hakimu Mugeta alikubaliana na ombi hilo na kuifuta. Mmoja wa mawakili wanaowatetea washitakiwa hao, Alex Mgongolwa, alisema hawana pingamizi la kufutwa kwa shauri hilo ingawa walitaka waelezwe sababu za hatua hiyo.
Mgongolwa alisema walitaka kujua sababu hizo kwani walikuwa na wasiwasi kuwa wateja wao wangeachiwa huru na kukamatwa tena baada ya muda mfupi na kupandishwa kizimbani. Waliiomba Mahakama iowape kinga.
Akiifuta kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 3/2013 na kuwaachia huru washitakiwa hao, ambao, Hakimu Mugeta alisema maombi ya upande wa mashtaka yamekubaliwa.
Akizungumzia uamuzi huo wa DPP wa kuwafutia kesi wateja wake, nje ya viwanja vya mahakama hiyo, Wakili Mgongolwa alisema, “DPP anapoona hana mashahidi thabiti wa kuja kujenga kesi yake anatumia kifungu hicho kufuta kesi kwani kuendelea kuwa na kesi za jinai mahakamani, ambazo anaona kabisa hana mashahidi thabiti wa kuwaleta mahakamani ni matumizi mabaya ya sheria na kuisababishia Serikali gharama pamoja na mrundikano wa kesi mahakamani.
Aprili 30, mwaka huu, upande wa mashitaka uliifuta kesi ya awali ya matumizi mabaya ya madaraka iliyokuwa ikimkabili Simba na wenzake wawili, na kisha kuwafungulia kesi nyingine ya mashitaka sita ya rushwa na uhujumu uchumi. Katika kesi hiyo namba 3/2013, washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kughushi. Walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Mei 29, 2012 kujibu mashitaka ya kulisababishia shirika hilo la umma hasara ya Sh bilioni 8.4.
Walidaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, walikula njama za kutenda kosa la vitendo vya rushwa, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Pia walidaiwa kufanya vitendo vya rushwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010 kwa kukubali kupokea Sh milioni 320 kama ushawishi wa kuiuzia Simon Group hisa za UDA ambazo zilikuwa hazijagawiwa.