Na Tatu Mohamed JamhuriMedia, Dodoma

MKURUGENZI Mtendaji wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kw kuendelea kutoa ufadhili katika miradi mbalimbali hususani ya kilimo.

Ametoa Shukrani hizo jana jijini Dodoma mara baada ya Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle kutembelea banda kubwa la wafanyabiashara wa zao la parachichi katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ambayo yanaendelea kwenye Viwanja vya Nzuguni.

Amesema kuwa, sehemu kubwa ya mafanikio yaliyopatikana Nyanda za juu Kusini sio uzalishaji bali hata katika suala la miundombinu ambapo ametolea mfano barabara ya Morogoro ambayo inaenda kwenye mto Kilombero.

Amefafanua kuwa hiyo ni sehemu ya mafanikio ambayo Tanzania na Wakulima wameyapata kupitia ufadhili Shirika la USAID na Ubalozi wa Marekani hapa.

“Jambo la muhimu ni kuendeIea kushirikiana kati ya nchi yetu na nchi ya Marekani lakini jambo la msingi ambalo ni muhimu sana sasa hivi ni kuendeleza biashara kati ya nchi yetu na Marekani

“Sasa hivi tumeanza kuuza zao la korosho katika soko la Marekani lakini pia Balaozi Dk.Battle ameweza kuongea na baadhi ya wafanyabiashara wanaoongeza thamani mazao na mafuta ya parachichi hivyo mahusiano ya biashara ni muhimu kwa kuwa tunaendelea kuwasaidia wakulima wetu na wafanyabiashara,” amesema.

Amebainisha kuwa, kwa mujibu wa Balozi Dkt.Battle wanakiu ya kupata matunda ya parachichi na mengine kutoka nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla na kwamba hiyo ni fursa ya kuweza kupeleka bidhaa kwenye soko la Marekani.

Hata hivyo, Balozi Dkt. battle ameahidi
ameahidi kuendelea kufadhili shuguli za kilimo, kuongeza dhamani ya bidhaa zitokanazo na mazao mbalimbali, kusafirisha bidhaa hizo na mazao ya Tanzania nchini Marekani sambamba na kufadhili shuguli zingine za uzalishaji maji na upatikanaji wa ajira.