Ufuatao ni uchambuzi wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaonyambua majukumu atakayofanya Dk. John Magufuli endapo Watanzania watampa ridhaa ya kuongoza nchi hapo Oktoba 15, mwaka huu.
Inaeleza wa kifupi malengo ya CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2015 – 2020) yenye dhamira ya kuinua maisha ya Watanzania popote walipo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Malengo ya Ilani ya uchaguzi ya CCM yamegawanyika katika makundi makubwa manne:
Kuondoa umasikini na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hususan kwa vijana; Kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; Kuboresha huduma za jamii na Kuendelea kudumisha umoja, amani, ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao.
Kuondoa umasikini na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hususan kwa vijana.
Serikali ya CCM katika kipindi cha 2015 – 2020, itajenga uchumi imara kwa kuwekeza kwenye sekta zinazotoa ajira zaidi, kukuza kipato na kupunguza umasikini.
Kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi zilizopo nchini; Kuboresha sekta za miundombinu na huduma za kiuchumi na kuwezesha wananchi kiuchumi na kukuza sekta binafsi.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa (ya mwaka 2025) ambayo inalenga kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuitoa Tanzania kutoka kwenye kundi la uchumi masikini na kwenda kwenye kundi la kati, ifikapo mwaka 2020.
Sera na kanuni za uendeshaji uchumi zimerekebishwa, miundombinu ya barabara na mawasiliano vimeimarishwa na ushiriki wa sekta binafsi katika nyanja mbalimbali umeongezeka.
Hata hivyo, kama Taifa, bado tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anakuwa sehemu ya mageuzi ya kiuchumi yanayokusudiwa.
Serikali ijayo ya CCM itahakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa pamoja na endelevu ili kumfanya Mtanzania wa kawaida ayaone mabadiliko ya kukua kwa uchumi wan chi yetu kwa vitendo.
CCM itatilia mkazo sekta ambazo zinatoa fulsa za ajira zaidi, kukuza kipato na kupunguza umasikini; kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi zetu; kuongeza uwezo wa Tanzania kushindana katika uchumi wa ulimwengu kwa kuboresha sekta za miundombinu na huduma za kiuchumi;na kuwezesha wananchi kiuchumi.
Uchumi wa pamoja na endelevu
Kuwekeza kwenye sekta zinazotoa ajira zaidi, kukuza kipato na kupunguza umasikini. Kilimo, uvuvi, ufugaji, utalii, mafuta na gesi asilia na madini.
Kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi zilizopo nchini kama vile viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, viwanda vya pembejeo na viwanda vinavyotumia malighafi chuma.
Kuboresha sekta za miundombinu na huduma za kiuchumi ardhi, nyumba na makazi, usafiri na uchukuzi, nishati, rasilimali watu na masailiano, sayansi na teknolojia.
Uwezeshaji wananchi kiuchumi na uimarishaji wa sekta binafsi kama vile urasimishaji wa mali za wanyonge, kuwezesha vijana kujiajiri, kuwezesha wanawake kujiajiri na kukuza sekta binafsi.
Kuwekeza kwenye sekta zinazotoa ajira zaidi, kukuza kipato na kupunguza umasikini katika maeneo ya kilimo na ushirika.
Serikali ijayo ya CCM itaweka utaratibu mpya na bora zaidi wa kusimamia kilimo ili kiwe cha kisasa na cha kibiashara; chenye tija na ambacho mazao yatakuwa yameongezwa thamani.
Tutawaunganisha wakulima wote katika vikundi vya ushirika ili iwe rahisi kuwafikia kwa huduma za ugani, masoko, mikopo ya riba nafuu kutoka kwenye Benki ya Maendeleo ya Kilimo na taasisi nyingine za fedha.
Tutaimarisha taasisi za utafiti wa kilimo za ndani na kuziunganisha na wakulima ili wazalishe kwa tija na kulingana na masoko.
Tutaweka mkakati mahsusi wa uendelezaji wa kilimo na wakulima wa mazao makuu ya biashara (Pamba, korosho, kahawa, tumbaku, chai, karafuu na mkonge), na ya nafaka na mazo mchanganyiko (mahindi, mpunga, ufuta, na alizeti) , mboga na matunda ili kuwawezesha kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao.
Tutasimamia uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao ya wakulima kwa kushirikiana na vyama vya ushirika pamoja na sekta binafsi.
Tutatenga masoko ya kimkakati katika maeneo ya mipaka ya nchi ili kuwapa wakulima fursa ya kuuza mazao yao nje ya nchi.
Tutaongeza kasi ya upimaji ardhi ili kuondoa mgogoro ya ardhi nchini, kuhakikisha usalama wa miliki kwa kuwapatia wakulima hati miliki ambazo zitatumika kama dhamana ili kupata mikopo.
Ufugaji
Kwenye sekta ya ufugaji, Serikali ya CCM itapima na kumilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji nchini ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima ili sekta hii itoe mchango stahiki kwenye kukuza uchumi.
Tutaimarisha miundombinu ya mifugo, na kuanzisha mashamba darasa katika kila Halmashauri ya Wilaya ili wakulima wapate elimu ya ufugaji kwa vitendo.
Tutahamasisha wafugaji wajiunge kwenye vikundi vidogo ili iwe rahisi kuwapatia huduma za ugani na mikopo yenye masharti nafuu. Tutaishirikisha sekta binafsi katika kuanzisha viwanda vya nyama na mazao mengine yatokanayo na mifugo ili kuyaongezea thamani.
Uvuvi
Katika kipindi cha 2015- 2020, Serikali ya CCM itaboresha uvuvi kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira (Fish Aggregating Devices) ili iwe rahisi kwa wavuvi kuyafikia maeneo yenye samaki wengi kwa urahisi zaidi. Tutaimarisha huduma za ugani na mafunzo, kuongeza mapambano dhidi ya uvuvi haramu.
Tutaimarisha vikundi vya ushirika vya wavuvi wadogo wadogo ili iwe rahisi kuwakopesha vifaa vya uvuvi kama nyavu, injini na boti. Majokofu pamoja na huduma za mikopo kutoka katika taasisi za kifedha.
Tutajenga bandari kubwa mbili za uvuvi (Zanzibar na Bara) ili kuhakikisha Taifa linanufaika na raslimali za baharini na tutashirikiana na Mashirika ya Umma yenye dhamana ya uvuvi nchini ili kuwavutia wawekezaji kuanzisha viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
Utalii
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM itahakikisha miundombinu inayohusiana na utalii inaongezeka na kuimarika ili kuwavutia watalii zaidi.
Tutaongeza msukumo kwenye utalii wa historia kwa kuboresha miundombinu kwenye maeneo ya malikale na kuyatangaza maeneo hayo.
Tutaimarisha mafunzo ya hoteli na utalii ili kuongeza ubora wa watumishi wa huduma za ukarimu na utalii.
Tutashirikiana na wadau wa utalii katika kuboresha mazingira kwa watalii wa ndani na nje na kuweka mipango ya pamoja iliyopimika ili kupata watalii milioni mbili kwa mwaka ifikapo mwaka 2020.
Tutahakikisha Watanzania wengi zaidi wanaajiriwa katika sekta ya utalii na wananufaika nayo, na sekta hiyo inaongeza mchango wake katika pato la Taifa.
Maliasili
Katika kipindi cha 2015-2020, Serikali ya CCM itaweka utaratibu wa wazi utakaowawezesha wananchi wanaoishi jirani na hifadhi kunufaika na raslimali za maliasili inayowazunguka.
Tutaanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori ambayo itasimamia uendeshaji wa raslimali hiyo. Tutapambana na ujangili wa wanyamapori wakiwemo tembo na faru.
Mafuta na Gesi Asilia
Kwa kuzingatia ugunduzi wa kiwango kikubwa cha gesi asilia na matarajio ya upatikanaji wa mafuta, Serikali ijayo ya CCM itahakikisha kuwa sekta hii inakuwa na manufaa kwa Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo kwa kufanya yafuatayo:
Itawezesha na kusimamia ujenzi wa miundombinu muhimu ya gesi asilia na mafuta nchini pamoja na kukamilisha mpango kabambe wa matumizi ya gesi asilia (Natural Gas Utilisation Master Plan).
Itaweka mfumo utakaofanya shughuli nyingi zinazoendana na utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi zinabakia chini ili kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania kiuchumi katika eneo hili kupitia sekta binafsi.
Katika eneo hili, tutahakikisha wananchi wanaopakana na miundombinu ya gesi na ambako bomba la gesi linapita wanashiriki na kunufaika na gesi.
Itaendelea kusomesha vijana wa kitanzania katika ngazi mbalimbali za vyuo vikuu na vya ufundi kulingana na mahitaji ya raslimali watu katika Sekta ya Gesi na Mafuta.
Itaweka mfumo unaounganisha sekta ya gesi na mafuta na sekta nyingine za uzalishaji ili kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda na kuifanya Tanzania ifikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Itahakikisha hifadhi za kimkakati zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya mafuta kwa nchi yetu na nchi jirani zinajengwa Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar.
Itaendeleza mradi wa kugeuza gesi kuwa katika hali ya vimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) ili kuwezesha mauzo ya gesi asilia ndani na nje ya nchi.
Itahakikisha inatekeleza sera na sheria za kusimamia mapato yanayotokana na gesi asilia na mafuta ili kuhakikisha fedha zinatumika kwa manufaa ya wananchi wa kizazi kijacho.
Madini
Serikali ijayo ya CCM itaweka na kusiamia mfumo thabiti wa kukagua shughuli za migodi, kukusanya takwimu za madini na kufuatilia maduhuli yatokanayo na madini kwa malengo mapana na kuongeza mapato ya Serikali.
Tutaweka utaratibu mzuri wa kisheria wa kuwatambua wachimbaji wadogo wadogo na kurahisisha upatikanaji wa mafunzo, teknolojia na mikopo ya riba nafuu.
Tutasimamia na kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongozi thamani madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.
Tutahakikisha migodi yote inanunua huduma na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha kuridhisha.
KUKUZA VIWANDA
Katika kipindi cha 2015 -2020, Serikali ya CCM itajenga viwanda mama na kuimarisha viwanda vilivyopo kwa kuhakikisha kwamba:
Ifikapo 2020, mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa unaongezeka toka asilimia 9.9 za sasa hadi asilimia 15, na sekta hiyo inachangia asilimia 40 ya ajira zote nchini.
Tutatekeleza mpango thabiti wa kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha viwanda vikubwa na vya kati na kuweka utaratibu wa kuvilinda dhidi ya bidhaa zisizo na ubora zinazoingizwa nchini kinyume na utaratibu.
Tutajenga mazingira rafiki yatakayowezesha kupunguza gharama za uwekezaji na uendeshaji wa viwanda.
Tutaanzisha viwanda vya msingi vinavyotumia malighafi ya chuma na makaa katika maeneo ya Liganga na Mchumchuma.
Tutaendeleza kasi ya ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati hasa vinavyosindika mazao na kuhakikisha Benki ya Rasilimali (TIB) inapanua wigo wake ili kutoa huduma katika maeneo yote nchini ikiwemo Zanzibar.
Kuboresha sekta za miundombinu na huduma za kiuchumi
Chama Cha Mapinduzi kinatambua kwamba miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji ni muhimu katika kuchochea ukuwaji wa shughuli za kiuchumi ambazo zitawezesha kuongeza ajira nchini na kukuza Pato la Taifa kwa jumla.
Katika miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM, itafanya yafuatayo:
Ardhi, Nyumba na Makazi
Tutajenga mfumo utakaorahisisha umilikishwaji wa ardhi na uhifadhi wa kumbukumbu za ardhi kwa kukamilisha ujenzi wa Mfumo wa kumbukumbu za Ardhi (Intergated Land Management Information System).
Tutaanzisha Baraza la Taifa la Ushauri la Ardhi (National Land Advisory Council) lenye lengo la kufanya ardhi itumike kwa ufanisi.
Tutaanzisha Mamlaka ya udhibiti wa Biashara ya Nyumba na utozaji wa kodi za nyumba.
Tutaongeza viwanda vya vifaa vya ujenzi (Saruji, nondo na mabati) na kupunguza kodi katika vifaa hivyo ili kumpunguzia mwananchi gharama za ujenzi na kuwezesha wananchi wengi zaidi kumiliki nyumba zao.
Usafirishaji na Uchukuzi
Barabara; tutaimarisha Mfuko wa barabara kwa kuongeza vyanzo vya mapato, kuboresha mfumo wa ufuatiliaji na kuanzisha wakala utakaosimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za miji, majiji na halmashauri ambazo ziko chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Tutamalizia ujenzi wa barabara kuu za lami zenye urefu wa kilometa 2,358 na kujenga barabara mpya za lami zenye urefu wa kilometa 3,419 zitakazounganisha Mikoa na Wilaya zote.
Tutashirikisha kikamilifu vikundi vya wananchi katika kazi za matengenezo madogo madogo ya barabara na kuwashirikisha wakandarasi wadogo wadogo wa kitanzania wanaoonesha nia ya kushiriki kazi kubwa za ujenzi wa barabara ili kuwajengea uwezo na kuwapatia fursa za kushiriki katika sekta ya ujenzi.
Reli; tutashirikiana na sekta binafsi kuanzisha ujenzi wa reli zifuatazo kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge)
Dar es Salaam – Tabora – Mwanza/Kigoma
Uvinza – Msongati (Burundi)
Isaka – Kigali (Rwanda)
Mtwara – Songea –Mbambabay (na matawi ya kwenda Mchuchuma na Liganga)
Tanga – Arusha – Musoma
Kaliua – Mpanda – Karema
Tutajenga uwezo wa Mashirika yetu ya reli ya TRL na TAZARA ili yatoe huduma bora za usafiri wa reli.
Usafiri wa Majini
Tutaimarisha miundombinu ya usafiri wa majini kwa kuimarisha miundombinu katika bandari za Zanzibar, Dar es Salaam, Mtwara, Mafia ,Mwanza, Kigoma, Tanga, Bukoba, Kyela, Musoma na kunua vyombo vya usafiri vya abiria namizigo katika Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Usafiri wa Anga
Tutashirikiana na sekta binafsi kuandaa mipango kabambe ya usafiri wa anga, kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege Dar es Salaam, Zanzibar, Kigoma, Shinyanga, Dodoma, Mwanza, Lindi, Tanga pamoja na kuvifanyia ukarabati viwanja vya Iringa, Njombe, Simiyu, Musoma na Moshi.
Tutahakikisha kunakuwa na ushirikiano na sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuimarisha shirika la ndege la Taifa.
Nishati
Nishati ya umeme – Kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na usambazaji wa umeme vijijini ili asilimia 60 ya Watanzania wawe na umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2020 na waweze kumudu gharama za kuunganisha umeme.
Nishati ya Gesi – Tutahimiza matumizi ya gesi ya petrol (Liquified Petrolium Gas – LPG) na gesi asilia katika matumizi ya nyumbani na viwandani ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa hivyo kuhifandhi mazingira.
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia
Tutaimarisha miundombinu ya TEHAMA ili iweze kutumiwa na wananchi wengizaidi na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.
Tutahakikisha huduma za mawasiliano ya simu za viganjani zinapatikana kwa wananchi wote kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote katika vijiji vyote Tanzania Bara na Visiwani.
Tutawalinda watumiaji wa simu za viganjani dhidi ya dhuluma, wizi na uhalifu wa mitandao.
Uwezeshaji wananchi kiuchumi
Chama Cha Mapinduzi kitawawezesha wananchi kiuchumi kwa kuhakikisha kuwa:
Tutatenga kiasi cha shilling million 50 kwa kila kijiji kama mfuko wa mzunguko (Revolving Fund) kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS) katika vijiji husika.
Tutatenga maeneo mahsusi katika kila Halmashauri kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo, kuondoa kero za ushuru na kodi zinazotozwa, kurasimisha biashara, na kuwaunganisha na asasi za fedha zinatoa mikopo kwa masharti nafuu.
Tutaanzisha mamlaka ya Usimamizi wa Biashara Ndogo na za Kati, Mfuko wa Kimataifa wa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kwa kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na tutazitaka Halmashauri zitenge asilimia 30 ya manunuzi yake kwa ajili ya zabuni kwa kampuni ndogo zinazomilikiwa na vijana na wanawake katika Halmashauri husika.
Tutahamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji kwa kusimamia utekelezaji wa sheria ya ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma na kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kuendesha biashara.
Urasimishaji mali za wanyonge
Katika kipindi cha 2015 – 2020, Serikali ya CCM itafanya mambo yafuatayo;
Itaanzisha chombo chenye nguvu ya kisheria kitakachoratibu shughuli za urasimishaji mali za wananchi kama vile umiliki wa ardhi ili waweze kutumia kama dhamana ya kupata mitaji.
Itatekeleza mpango wa Taifa wa matumizi bora ya ardhi kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mpango ya Matumizi Bora ya Ardhi, Halmashauri za Miji, na Wilaya ili kukamilisha kazi ya upimaji miji, vijiji, mashamba na kuwapatia wananchi Hati Miliki za Serikali na HATI Miliki za Kimila.
Itaanzisha Mfuko maalumu wa kugharamia shughuli za urasimishaji utakaoziwezesha Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji kukopeshwa kwa masharti nafuu (Bank Guarantee Scheme).
Itahakikisha kwamba Halmashauri zote nchini zinaendelea kutenga, kurasimisha, kupima na kuyawekea miundombinu maeneo maalum ya vijana kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali hususan kilimo, ufugaji, madini, viwanda vidogo, uvuvi, mawasiliano na biashara.
Itaziwezesha SACCOS za vijana katika Halmashauri zote nchini kupata mikopo kutoka benki na taasisi nyingine za fedha.
Itawawezesha vijana wanaohitimu elimu ya juu na vyuo vya ufundi kuunda makampuni kulingana na fani zao kwa lengo la kuwapatia mitaji na nyenzo kupitia taasisi za fedha na mifuko mingine ya uwezeshaji.
Itahakikisha kwamba Halmashauri zote nchini zinaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa Vijana kwa mujibu wa sheria ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu.
>>ITAENDELEA