Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es Salaam
WANACHAMA wa Jumuiya za Nchi Kusini Mwa Afrika (SADC), sekta ya Umeme wamesema watahakikisha wanaweka mikakati endelevu na kujadiliiana ili kufufua vyanzo vya nishati hiyo kwa lengo la kufanikisha kusafirisha na kusambaza kwa wateja wa ukanda huo.
Akizungumza katika mkutano huo, uliojumuisha Wanachama wa SADC sekta ya Umeme leo Oktoba 15,2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme, Dkt Khatibu Kazungu , amesema wataalamu wa umeme kutoka Jumuiya hiyo wamekutana leo kwa lengo la kujadili na kutatua changamoto wanazokutananazo ili wafikie malengo mahususi.
“ Mkutano huu wa wataalamu wa umeme wa Jumuia ya SADC ni kuweka mikakati madhubuti ya kutumia vyanzo vilivyopo kushirikiana kwa pamoja katika kufua umeme, kusafirisha na kusambaza kwa wateja.
“Sisi kama Serikali tuna mradi unaoitwa TAZA, wenye lengo la kuunganisha miundombinu ya umeme hapa Tanzania na Zambia na tunapokutana katika vikao kama hivi tunapitia mikakati yetu na hatua ambayo tumefikia kisha kuangalia kwa kina changamoto zinazotukwamisha kufikia malengo tuliyojiwekea , ” amesema.
Dk Kazungu ameongeza kwa kusema kuwa, mahitaji ya umeme wa ndani uko vizuri kutokana na kuwepo kwa mradi wa Bwawa la Nyerere ambalo kwa sasa linauwezo wa kuzalisha megawati 700 na siku chache zijazo litazalisha megawati 900.
Sambamba na hayo amebainisha kuwa tofauti na Bwawa la Nyerere pia kuna vyanzo vingine kikiwemo cha mradi wa Umeme wa Jua, ambao kwa sasa una uwezo wa kuzalisha megawati 600 na kupitia Joto Ardhi nako kunazalishwa umeme megawati 5000 na kufanya Tanzania isiwe na tatizo la uzalishaji wa umeme hivuo kinachotakiwa ni kujipanga vizuri kama Serikali kwa kuongeza vyanzo vingine.
“Serikali pia ina mradi mwingine wa umeme unaoitwa Green Imara ambao ni mahususi katika kuboresha miundombinu ya umeme na kuongeza vyanzo vingine na kuunganisha nishati hiyo katika mikoa ya pembezo mwa nchi ambayo Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara hadi mwisho wa mwaka huu itakuwa imeeinguzwa katika gridi ya Taifa,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji uzalisahi umeme TANESCO, Mhandisi Costa Rubagumya, amesema Tanzania iko katikati ya ‘East Africa Powe Pool’ ambako inapatikana Kenya na kwa upande wa ‘Southern African Power Pool’ inapatikana Zambia.
“Katika maeneo hayo mawili inatupa uwezekano wa kusaidiana katika nyanja ya umeme ikiwa nchi mojawapo inapokuwa na shida ya nishati hiyo, mfano eneo la Kariba kwa sasa lina ukame na kusababisha Zimbabwe na Zambia kupitia katika kipindi kigumu na kutokana na kuwepo kwa ushirikiano huu unatoa fursa ya kusaidiana na kutuweka salama katika nyanja ya umeme,” amesema.