Kuundwa kwa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) miaka 27 iliyopita ni kitendo cha ukombozi kwa Mwafrika. Ni ukombozi wa kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Unamtoa katika unyonge na umaskini na kumpeleka katika uwezo wa kuwa tajiri na kumiliki njia za uchumi kwa manufaa ya maendeleo yake katika jamii.
SADC ina asili yake. Asili inayotokana na mawazo, mwamko, msimamo na nia iliyojaa uwezo na sababu za kindugu za kuondoa dhuluma na udhalimu uliopata kushamiri enzi za utawala wa kikoloni.
Chama cha siasa TANU (Tanganyika African National Union) baada ya Tanganyika kupata uhuru wa bendera mwaka 1961, kilijibadili na kuwa chama cha ukombozi na kuweka malengo, sera na taratibu zake katika kumkomboa Mtanganyika na Mwafrika.
Suala la uhuru wa Afrika na Umoja wa Afrika lilikuwa muhimu kwa Tanganyika mara baada ya uhuru kwa sababu Tanganyika ilipakana na koloni la Wareno lililokuwa limepakana na tawala dhalimu za ubaguzi wa rangi Kusini mwa Afrika.
Tawala hizi zilinyanyasa sana wananchi wa nchi za kusini mwa Afrika na kuleta hofu katika uhuru na usalama wa nchi yetu. TANU na serikali yake zilitoa nafasi kwa vyama vya ukombozi kusini mwa Afrika kuweka makao makuu na mafunzo kwa wapigania uhuru.
Si hivyo tu, msimamo wa Rais wa TANU, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika suala la uhuru na umoja wa Afrika, alikuwa akipendekeza uhuru na umoja huo uwe na shughuli maalumu, hasa katika uchumi.
Ni dhahiri Umoja na Ukombozi wa Mwafrika una lengo la kumkomboa Mwafrika kutokana na madhila ya ukoloni, ubeberu na ukoloni mamboleo. SADC ni chombo ambacho leo kinafanya kazi hizo za ukombozi wa kisiasa na kiuchumi.
Ni shahiri TANU iliweza kujenga uhusiano na vyama vingine vya siasa katika Afrika. Uhusiano ambao ulisaidia nchi za Afrika Mashariki na Kati na zile za Kusini mwa Afrika kupata uhuru. Mathalani, FRELIMO cha Msumbiji na ANC cha Afrika Kusini.
Kuundwa kwa vyama vya ukombozi na kuanzishwa kwa vyombo vya ukombozi kama vile Umoja wa Afrika, Kamati ya Ukombozi na kadhalika, kumesaidia mno kutengeneza chombo hiki SADC. Chombo hiki na vingine vilivyopo kama vile Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (CEEAC) ni vyombo vya ukombozi.
Kuweko kwa SADC kumedhihirisha fikra na ndoto za viongozi wetu wa Afrika kuwa penye nia pana njia na kuthubutu ni kufaulu. Leo tunajivunia SADC – ni chombo cha kuwakomboa Waafrika kutoka katika hila na mikono ya mabeberu.
Wiki ya viwanda ya maonyesho ya bidhaa mbalimbali ya SADC imetufumbua macho na kutuonyesha mwelekeo wapi Afrika inastahili kuelekea na kujitegemea katika masuala yote ya kisiasa, kiuchumi na mengineyo yanayohusu maendeleo ya Mwafrika.
Haitoshi na wala bado Waafrika kuamini tumevuka mto na kuondoa umaskini. Hapana. SADC imeonyesha sudusi moja ya mafanikio ya Umoja na Ukombozi. Sudusi tano bado ziko ng’ambo gizani. Nuru, kusudi na nguvu ya pamoja zinahitajika kuondoa sudusi tano.
Mabaraza ya mawaziri, makatibu wakuu, watendaji na mikutano ya viongozi wa nchi kwa mujibu wa taratibu na kanuni za SADC, na hasa mkutano huu wa 39, pamoja na kumsimika mwenyekiti mpya wa SADC, utoke na maazimio yatakayotoa dira na changamoto za kupangua sudusi zilizobaki.
Kiswahili kutumika kuwa lugha ya mawasiliano katika shughuli za chombo hiki, utakuwa ufumbuzi mmoja wapo katika harakati za kuimarisha umoja, usalama, uchumi na ukombozi wa Afrika. Jambo hili linawezekana. Twendeni pamoja na Aluta continue.