Jumuiya ya kimataifa pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wanasubiri kuona mageuzi makubwa yatakayoletwa na Rais Dk. John Magufuli, ambaye ndiye mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo.

Tayari katika hotuba yake ya kukubali majukumu yake hayo, ameainisha mambo ambayo atayapa kipaumbele katika kipindi chake cha mwaka mmoja wa uenyekiti wake wa SADC. Mambo hayo ni pamoja na kuimarisha uchumi wa jumuiya, suala la vikwazo vya Zimbabwe pamoja na sekretarieti.

Katika masuala ya uchumi, Rais Magufuli amesema kama hakuna jitihada kubwa zitakazofanywa na sekretarieti itakuwa vigumu kufikia lengo husika.

Katika mkutano huo Magufuli amesema changamoto kubwa ni uchumi, kwamba nchi wanachama zinapaswa kutumia mafanikio ya kisiasa kufikia mafanikio ya kiuchumi.

“Malengo ilikuwa kufikia asilimia saba ya ukuaji uchumi kwa nchi husika, lakini tupo mbali na malengo yetu kiuchumi. Kuna sababu nyingi uchumi wetu kudorora. Mei mwaka huu nilitembelea nchi tano za SADC, kwa bahati mbaya tatu kati yake zilikuwa zimekumbwa na njaa na zilikuwa kwenye mchakato wa kuagiza chakula kutoka nje.

“Wakati huo Tanzania ilikuwa na tani milioni 2.5 za chakula cha ziada. Matatizo mengi kama haya sekretarieti inafaa kuyaangalia na itusaidie, naamini tungepata majibu kutoka kwao kwa nini miaka 10 uchumi wa pato la ndani unashuka,” amesema Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameipa changamoto Sekretarieti ya SADC kuhusu kufanya miradi ambayo itaifanya taasisi hiyo yenye nguvu ndani ya Bara la Afrika na kusini kuwa karibu zaidi na wananchi. Ametoa mfano wa SADC walau kujenga hospitali moja ambayo itawahudumia wananchi.

“Ninadhani ni wakati mwafaka sasa sekretarieti ifikirie namna ya kuwa karibu zaidi na wananchi kwa kufanya miradi ambayo inawagusa wananchi wa jumuiya…hizo warsha, semina na mambo mengine kama hayo hayatusaidii. Katika kipindi changu nitapenda kuona jumuiya tukiipeleka kwa wananchi.

“Mfano, ujenzi wa kituo cha afya unagharimu takriban dola za Marekani 200,000 (zaidi ya Sh milioni 400), hivi tunashindwa hata kujenga walau vituo vya afya vya mfano katika nchi wanachama?” amehoji Rais Magufuli.

Kuhusu suala la vikwazo vya kiuchumi vya Zimbabwe, Rais Dk. John Magufuli amesema vikwazo hivyo vimedumaza uchumi wa nchi hiyo huku vikidumaza pia maendeleo ya SADC. Rais Magufuli amesema nchi za SADC ni kama mwili wa binadamu, kinapoumia kiungo kimoja mwili unadhoofu.

 “Zimbabwe wamekuwa kwenye vikwazo kwa muda mrefu, hiki kifungo tunaathirika sisi wote, napenda kupendekeza kupitia mkutano huu kuziomba jumuiya za kimataifa ziiondolee vikwazo Zimbabwe, na nawaomba wanachama wote tulisemee hili.

“Kuhusu Zimbabwe, tumekubaliana kuwa tuendelee kufanya mawasiliano na jumuiya za kimataifa ili kuwezesha kuondolewa kwa vikwazo kwenye nchi hiyo, ikiwamo kupitia balozi zetu pamoja na jumuiya mbalimbali.

“SADC kwa pamoja viongozi wote kwa kauli moja tunatamka tuko pamoja na Zimbabwe na hatutaiacha,” amesema Rais Dk. Magufuli.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imechagizwa na tamko la pamoja la mkutano lililotolewa na Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax, ambaye amesema suala la Zimbabwe limepata msukumo mpya na kwamba jumuiya sasa inalivalia njuga kuhakikisha kwamba linapatiwa ufumbuzi wa kudumu ambao ni kuiondolea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimedumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Akizungumza wakati wa hotuba ya kuhitimisha mkutano huo, Rais Dk. John Magufuli amesema wakuu wa nchi wamekubaliana kuendelea kufuatilia hali ya usalama nchini Congo (DRC) lakini pia wameiagiza sekretarieti kuharakisha chombo cha kukabiliana na majanga kitakachosaidia nchi wanachama kukabiliana na majanga kama vile njaa, mafuriko, vimbunga, magonjwa ya mlipuko na mengineyo.

Amesema wakuu wa nchi walipitia hali ya uchumi katika eneo la jumuiya, ambapo uchumi wa nchi hizo ulishindwa kukua kama ulivyotarajiwa kwa asilimia saba na kushuka hadi asilimia 3.1, hivyo wamekubaliana kuwekeza kwenye miundombinu, kwa kuwa ni mojawapo ya kikwazo cha kukua kwa uchumi kwenye Bara la Afrika zikiwamo nchi za SADC.

“Kwa pamoja tumekubaliana kuondoa viwazo vya kibiashara, ukiritimba katika maeneo ya mipakani na rushwa. Tumekubaliana kuboresha mazingira ya ukuaji wa uchumi na fedha katika nchi zetu.

“Masuala mengine tuliyojadili ni upatikanaji wa mapato, suala la ombi la Burundi kujiunga na SADC pamoja na suala la vikwazo kwa Zimbabwe,” amesema Rais Dk. Magufuli.

Kuhusu suala la Burundi kujiunga na jumuiya hiyo, amesema bado haijakamilisha vigezo katika baadhi ya maeneo ambapo sekretarieti ya jumuiya hiyo imeagizwa kuwaelekeza na kisha kutuma tena maombi hayo, na kuhusu Zimbabwe, amesema wamekubaliana kuifuatilia jumuiya ya kimataifa ili iwaondolee vikwazo.

Pamoja na mambo mengine, amesema mkutano huo pia umepitisha mpango wa kuongeza mapato kwa SADC, ambapo nchi wanachama zitakuwa na hiyari ya kuchagua njia bora ya kuchangia.

Uchumi nchi za SADC

Akizungumza katika mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo, Rais John Magufuli amesema kama hakuna jitihada kubwa zitakazofanywa na sekretarieti itakuwa vigumu kufikia lengo husika.

Katika mkutano huo uliofanyika  katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Magufuli amesema changamoto kubwa ni uchumi, kwamba nchi wanachama zinapaswa kutumia mafanikio ya kisiasa kufikia mafanikio ya kiuchumi.

Rais Magufuli amesema hayo wakati akikabidhiwa uenyekiti wa SADC na mtangulizi wake, Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob, wadhifa ambao ataushikilia kwa mwaka mmoja.

 “Tunaahidi kushirikiana na nchi zote wanachama wa SADC kuhakikisha kupitia mkutano huu ndoto na mawazo ya Baba yetu wa Taifa pamoja na viongozi wengine waanzilishi wa jumuiya hii yanaendelea kutekelezwa kwa vitendo,” amesema Rais Magufuli akipokea uenyekiti huo.

Makubaliano mengine

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk. John Magufuli, ambaye ni Rais wa Tanzania ametaja mambo kadhaa yaliyopitishwa katika kikao cha wakuu wa nchi 16 wa jumuiya hiyo kilichofanyika Jumamosi Agosti 17, 2019 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kilele cha mkutano wa wakuu wa nchi hizo, Rais Magufuli amesema wameiagiza Sekretarieti ya SADC kuanzisha chombo cha kukabiliana na majanga ili kuzisaidia nchi wanachama zitakapokumbwa na mafuriko, njaa na magonjwa ya mlipuko.

Mkutano wa wakuu wa nchi ulifanyika Agosti 17 na Agosti 18, 2019 na ulitanguliwa na maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda yaliyoanza Agosti 5 hadi 8, 2019 na baadaye ikafuata mikutano ya kamati ya wataalamu pamoja na Baraza la Mawaziri wa SADC.

“Kwanza wakuu wa nchi wamewapongeza viongozi waliomaliza muda wao kutumikia SADC, walipitia hali ya uchumi na kuangalia changamoto ya majanga,” amesema Rais Magufuli.

Pia, wakuu hao wamekubaliana kuhakikisha kila nchi inaendelea kutilia mkazo uwekezaji wa miundombinu kwa kuwa ndio chanzo cha kufanikisha mkakati wa viwanda na uchumi wa SADC.

Nchi hizo pia zimekubaliana kuimarisha mazingira ya taasisi za fedha. Magufuli amesema kikao hicho pia kimepitisha mpango wa kuongeza mapato ya SADC, kila nchi itaangalia namna ya ushiriki katika uchangiaji.

Itifaki nne zasainiwa

Rais Dk. John Magufuli  amewaongoza wakuu wa nchi 16 za jumuiya hiyo kusaini marekebisho katika itifaki nne.

Itifaki zilizosainiwa ni kuhusu maendeleo ya viwanda, kubadilishana watuhumiwa na wafungwa na masuala ya jinai. Sekretarieti ya SADC itafuatilia utekelezaji wake kwa nchi zote zilizotia saini.

Makubaliano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).

Tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 1992, kutoka kwenye ile ya mwanzo iliyokuwa na ‘C’ mbili (SADCC), itifaki 33 zimekwisha kusainiwa na wakuu wa nchi wanachama.

Hata hivyo, si lazima kwa nchi kusaini itifaki zinazopitishwa na mtangamano huo hadi pale nchi husika itakapojiridhisha au kuwa tayari kusaini.

Kiswahili rasmi SADC

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye pia ni Rais wa Tanzania, John Magufuli, ametangaza Kiswahili kuwa lugha ya nne itakayotumika katika nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.

Wiki iliyopita baraza la mawaziri la jumuiya hiyo lilipitisha mapendekezo kuwa Kiswahili kianze kutumika kama lugha ya nne pamoja na kuwasilisha hoja nyingine 107 ili kujadiliwa, lugha zilizokuwa rasmi kabla ya Kiswahili ni Kiingereza, Kifaransa na Kireno.

Akizungumza wakati wa kuahirisha mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi, Rais Magufuli amesema katika kikao cha marais wa nchi wanachama kilichofanyika mwishoni wa wiki Ikulu, jijini Dar es Salaam, wakuu hao kwa pamoja wamekubaliana lugha hiyo ianze kutumika.

 Kuanzia sasa Kiswahili kitatumika katika mikutano ya jumuiya hiyo pamoja na machapisho yake mbalimbali.

“Baada ya hotuba yangu kusoma kwa Kiswahili, waheshimiwa marais wameiteua kuwa lugha ya nne SADC, mimi na wenzangu tumefurahi sana,” amesema Magufuli.

Rais Magufuli amepongeza uamuzi huo akisema ni hatua ya kumuenzi kwa vitendo muasisi wa SADC na Taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Dk. Stergomena Tax, amesema Mkutano huo wa 39 wa SADC umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi wanachama, ambapo wameweza kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na maendeleo ya nchi hizo.

Dk. Tax alisema kuwa katika mkutano huo pia viongozi wa jumuiya hiyo waliweza kufanya uamuzi wa kuchagua viongozi wa ndani katika jumuiya hiyo, ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ndani ya jumuiya hiyo (TROIKA), iliyokwenda kwa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.