Mkutano wa pamoja wa EAC-SADC kuhusu mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeitaka M23 na makundi mengine yasiyo ya kiserikali kujumuishwa katika mazungumzo na majadiliano yanayoendelea kwa lengo la kutatua mgogoro wa mashariki mwa Congo.

Mkutano huo pia umesisitiza umuhimu wa kuondolewa kwa vikundi vya kigeni, kutokomeza kundi la waasi wa Kihutu, Forces Démocratiques pour la Libération du Congo (FDLR), linaloendesha shughuli zake mashariki mwa DRC, pamoja na kuondolewa kwa hatua za ulinzi za Rwanda na vikosi vya Rwanda kujiondoa DRC.

Wakuu wa majeshi kutoka nchi wanachama wameagizwa kukutana ndani ya siku tano ili kuandaa mpango wa usalama wa Goma na maeneo jirani, pamoja na kujadili ufunguzi wa Uwanja wa Ndege wa Goma na njia kuu za usafirishaji, ikiwa ni pamoja na kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu mashariki mwa DRC.

Viongozi wa nchi wametaka kusitishwa mara moja kwa mapigano, kutangazwa kwa usitishaji wa mapigano rasmi, na kurejeshwa kwa huduma muhimu kama vile maji, chakula, na bidhaa nyingine za msingi.

Wamesisitiza kuwa suluhisho la kisiasa na kidiplomasia ndilo njia endelevu zaidi ya kutatua mgogoro wa mashariki mwa DRC.

Mkutano huo umeagiza mchakato wa mazungumzo yanayoendelea (Luanda na Nairobi) kuunganishwa kuwa mchakato mmoja wa Nairobi-Luanda ili kuimarisha ushirikiano.